
Budapest HUNGARY
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Mh. Hassani Iddi Mwamweta amewasilisha Hati za Utambulisho (Letters of Credence) kwa Mheshimiwa Dkt. Tamás Sulyok, Rais wa Hungary. Kitendo cha kuwasilisha Hati hizo kinamfanya aweze kutekeleza rasmi majukumu yake ya Kibalozi nchini Hungary kutokea Berlin, Ujerumani.
Hafla ya kuwasilisha Hati hizo ilifanyika kwenye Ikulu ya Hungary na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi kutoka Ofisi Binafsi ya Rais pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Hungary.
Balozi Mwamweta alitumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za upendo na kheri kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuelezea utayari wa Serikali yake kushirikiana na Serikali ya Hungary kwenye maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na elimu; maji; usafiri wa anga; afya; utalii; biashara na uwekezaji.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Rais Sulyok amempongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia jitihada zake za kutafuta amani kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu hasa DR-Congo na Msumbiji. Amesema Tanzania inaheshimika duniani kutokana na mchango wake wa kutafuta amani na kuifanya dunia kuwa sehemu salama.
Alifahamisha zaidi kuwa Serikali ya Hungary iko kwenye hatua za mwisho kufungua Ofisi Jijini Dar es Salaam ili kuchochea mahusiano mazuri ya Kidiplomasia hususan diplomasia ya uchumi baina ya mataifa haya mawili.



