0 0
Read Time:1 Minute, 30 Second

#WUNews

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mhe. Mahmoud Ali Youssouf amefanya mazungumzo kwa mara ya kwanza na Mjumbe Maalum wa AU wa Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS), Balozi Liberata Mulamula tangu ateuliwe hivi karibuni.

Mazungumzo hayo yalijikita katika majukumu mahsusi ya Mjumbe Maalum ambayo yatapelekea kufikiwa kwa malengo ya kimkakati yaliyowekwa. Mhe. Youssouf alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa majukumu hayo uendane na mipango mbalimbali ya maendeleo ya Bara la Afrika kama vile Agenda 2063 na
Miundo ya Amani na Usalama ya AU (APSA) pamoja na kuzingatia viwango vya kimataifa, ikijumuisha Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325.

Mwenyekiti huyo alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa uongozi wa wanawake katikati ya juhudi za AU katika maeneo yenye migogoro kama Sudan, Sahel, Pembe ya Afrika na Eneo la Maziwa Makuu.

Alimtaka Mjumbe Maalum kujenga ushirikiano imara na juhudi zinazofanywa na vijana na kuhakikisha ushirikishwaji wa wasuluhishi-wanawake na mitazamo ya kijinsia katika michakato yote ya kutafuta amani inayoongozwa na AU.

Aidha, Mhe. Youssouf alibainisha umuhimu wa kuongeza na kuimarisha ushirikiano na Jumuiya za Kiuchumi za Kanda (RECs), Mifumo ya Kanda (RMs), taasisi za AU, Taasisi ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa (UN Women) na asasi za kiraia ili kuhakikisha umoja na kuinua sauti za wanawake.

Kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa ahadi za Nchi Wanachama kupitia Mfumo wa Matokeo wa Bara (CRF) ilielezwa kama kipaumbele kikuu kwa uwajibikaji.

Mwenyekiti alihitimisha mazungumzo yake kwa kumhakikishia Mjumbe Maalum ushirikiano wa kutosha na kusisitiza umuhimu wa vyanzo endelevu vya fedha kwa ajili ya kugharamia harakati za kutafuta amani zinazosimamiwa na wanawake, hasa zile za ngazi ya chini kabisa.

Alielezea matarajio yake kuwa mjumbe maalum huyo ataendesha uhamasishaji unaoonekana, uongozi wa maono, na utoaji wa matokeo yanayopimika ndani ya mwaka wake wa kwanza.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %