
Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Jumapili tarehe 6 Juni, 2021.
Jumamosi tarehe 5 Juni, 2021 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango alizindua Kampeni ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira pamoja na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Kampeni hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyobeba kaulimbiu ‘Tumia Nishati Mbadala kuongoa Mfumo Ikolojia’.
Ni ukweli uliowazi kuwa kama nchi tunahitaji kubuni njia mbalimbali za kulinda ikolojia kwa manufaa ya viumbehai vyote na uchumi kwa ujumla kwani kuharibiwa kwa mazingira husababisha kupungua kwa pato la taifa kwa asilimia moja kila mwaka kama alivyoainisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mheshimiwa Suleiman Said Jafo.
Wadau wengi waliopata fursa ya kuchangia katika Kongamano lile walisisitiza umuhimu wa kutumia nishati mbadala lakini kwa bahati mbaya, kwa maoni yangu naona namna ya kuwafanya watanzania watumie nishati mbadala kama vile gesi haikuelezwa kwa mapana ama bado hakujawekwa njia bora na rafiki itakayowafanya watu watumie gesi kwa urahisi na kuacha kutumia mkaa ambao ili upatikane ni lazima miti ikatwe na hivyo kuhatarisha mazingira na ikolojia.
Tafiti zilizofanywa na Doggart (2020), Alem na wenzake (2015), Msuya (2011), Benki ya Dunia (2010), Peter na Sander (2009) zinaonesha maeneo kama Dar es Salaam tu peke yake hutumia tani laki tano (500,000) za mkaa kwa mwaka sawa na takribani asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini.
Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ya mwaka 2019 inaonesha kuwa utafiti uliofanyika 2017/2018 kwa kaya mbalimbali unaonesha kuwa maeneo ya mjini na Dar es Salaam utumiaji wa mkaa ni asilimia zaidi ya 60 kama chanzo cha nishati.
Ni wazi kuwa utumiaji wa mkaa ni tishio kubwa kwa uhai wa mazingira na uhai wetu viumbehai vyote nchini kwa maana ya sisi wanadamu na viumbehai wengine kama ndege, wanyama na mimea.
JE TUNAFANYAJE KUEPUKA HILI?
Ni wazi kuwa kuna haja ya kutumia nishati mbadala kama vile gesi zitokanazo na mafuta ghafi ya petroli yaani Liquefied Petroleum Gas (LPG).
Kwa mujibu wa ripoti za EWURA kuanzia mwezi Julai mwaka 2016 zinaonesha kuwa makampuni yanayofanya biashara ya kuagiza LPG yaani LPG Marketing Companies (LMCs) yaliagiza jumla ya metriki tani 120,961 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na metriki tani 107,083 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 13, wakati kwa mwaka 2018 uagizwaji wa LPG ulikuwa metriki tani 142,939 na mwaka 2019 metriki tani 166,436 sawa na ongezeko la asilimia 16 ikiwa ni mchanganyiko wa gesi zote mbili Butane ambayo ni rafiki kwa mazingira ya Tanzania na Propane wakati kuanzia mwezi Julai 2019 mpaka Juni 2020 LMCs yaliagiza metriki tani 189,509 sawa na ongezeko la asilimia 30 kwa kipindi chote.
Ripoti hizi za EWURA zinaonesha kuwa matumizi ya gesi ya LPG kwa watanzania yanaongezeka, naamini ongezeko hili limechangiwa pia na kuondoka kwa ile dhana ya hofu kuwa gesi inalipuka kwani tunaona hata wauza chipsi wengi wanatumia gesi ya LPG kukaangia chipsi, kuku n.k. Lakini je ni kwa namna gani Serikali inatengeneza mazingira ya kufanya utumiaji wa gesi uwe mkubwa? Hili ndilo swali ambalo linapaswa litufikirishe kama watanzania.
Tatizo ninaloliona kwenye utumiaji wa gesi ya LPG si kulipuka bali gharama za gesi hiyo kwa kulinganisha na vipato vya watanzania wengi ambao kwa mujibu hotuba ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoitoa siku alipothibitishwa kuwa Makamu wa Rais pale Bungeni Dodoma alieleza kuwa licha ya kwamba Tanzania kama nchi tumeingia kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati lakini zaidi ya watanzania milioni 14 wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Ni wazi kuwa kwa takwimu hizi tatizo si wananchi kutaka kutumia mkaa bali wengi hawana uwezo wa kutumia gesi kutokana na kutokuwa na vipato vya kununua gesi hiyo kwa mara moja.
Hapa naomba nitoe uzoefu wangu kama mtu aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji wa Mauzo na Masoko (Sales and Marketing Executive) wa miongoni mwa kampuni kubwa za uagizaji mafuta na gesi ya LPG nchini na pia Afisa Mikopo wa benki kwa nyakati tofauti.
Kwa maoni yangu, tatizo lililopo kwenye LPG linasababishwa na ukubwa wa bei ya gesi kwa mtungi ama cylinder ambapo mtungi wa kilo 6 kubadilishwa kwa bei ya sasa hubadilishwa kati ya shilingi za Tanzania 18,000 mpaka 20,000 huku kununua seti nzima (complete set) huwa kati ya shilingi elfu 47 mpaka elfu 50.
Kwa upande wa mtungi wa kilo 15 bei ya kubadilisha huwa kati ya shilingi elfu 45 mpaka elfu 50 wakati kwa seti nzima huwa kati ya shilingi elfu 65 mpaka elfu 80.
Kwa upande wa mitungi ya kilo 38 bei ya kubadilisha ni kati ya shilingi elfu 85 mpaka laki moja wakati seti nzima ni kati ya shilingi 180,000 mpaka shilingi 195,000 ambapo mtu akinunua na jiko la sahani mbili na vifaa vyake hufikia kiasi cha shilingi laki 3.
Kiwango hiki cha bei kinatokana na uchache wa watumiaji wa gesi nchini. Kwa hali hiyo ya uchache wa watumiaji, makampuni ya gesi hulazimika kuingiza gharama za uendeshaji (operational expenses) katika bei ya kununulia gesi na hivyo kufanya bei ya mtungi kuwa mkubwa na hivyo kuwafanya watanzania washindwe kutumia gesi na kuamua kutumia mkaa kutoka na ukubwa wa bei ya gesi.
Ni wazi kuwa kwa bei hizi watanzania wengi hawawezi kumudu kununua kwa mara moja. Mfano ulio wazi katika hili la bei, kwa kuona changamoto ya kipato kununua seti nzima ya gesi kwa mara moja, makampuni mengi ya gesi huwa na utaratibu wa kuwakopesha wafanyakazi wao seti zima jambo ambalo huwapunguzia gharama za maisha kwa kutolipa pesa yote kwa mkupuo.
Tujiulize, kama makampuni haya ya gesi yanaliona tatizo hili, je haiwezekani kwa serikali kuandaa utaratibu kwa watanzania kuweza kukopeshwa gesi na vifaa vyake (accessories) ili kuwapunguzia gharama ya maisha kwa kulipa kidogo kidogo?
Mkakati wa serikali katika hili na hasa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inafaa ujielekeze katika kuyafanya makampuni ya gesi kuwa na wateja wengi (huge customer base) jambo ambalo litapelekea bei ya gesi kupungua kutokana na makampuni ya gesi kuagiza gesi kwa wingi na kuuza kwa wateja wengi (economies of scale) hii ni kanuni ya uchumi inayoeleza wazi kuwa bidhaa (supply) ikipatikana kwa wingi bei yake (price) hushuka na hivyo uhitaji wake (demand) huongezeka kutokana na kushuka kwa gharama za manunuzi.
Lakini pia Serikali itasaidia kuongeza ushindani kwa makampuni tofauti na takwimu za sasa karibuni ambapo kati ya metriki tani 166,436 zinazoagizwa nyingine husafirishwa Rwanda, Kenya na Comoro kutokana na kukosekana kwa uhitaji mkubwa katika soko la ndani.








