
UTUMWA WA MWAFRIKA WA MILELE
Na H.MKALI
mkali@live.co.uk
Waafrika leo, wamechukuwa uwezo wao wa kumiliki mbegu na kuuweka kwenye mikono ya makampuni na mataifa ya nje.
Na hizo mbegu hata wakishazinunua kutoka kwa hao wakubwa wa nje, bado haziwi zao – kwani hawaruhusiwi kupeana, kuuziana au kubadilishana kama ilivyokuwa tangu kilimo kianze hapa duniani miaka zaidi ya 10,000 iliyopita.
Leo miaka zaidi ya 50 baada ya Waafrika kujinyakulia uhuru wao; lakini uhuru wa kupanda na kuvuna tunautegemeza kwenye hiyari ya mabeberu kutuuzia mbegu? Huu ni uhuru wa sampuli gani?
Aidha, tunajiweka kwenye utumwa wa milele wa kulipa kitu kinachoitwa “technology surcharge au royalty” kwa mabeberu wamiliki wa hizi mbegu. Waafrika nani katuroga sisi?
Uhuru ambao mliturithisha (mababu na mabibi mliotangulia mbele za haki), baada ya ninyi kuupigania miaka 1950s hadi 1990s hatunao tena.
Kweli ya kuwa anayemiliki mbegu na anayemiliki ardhi ndio anayetawala nchi hata kama halali Ikulu, haizingatiwi tena.
Leo, Afrika kuna mashindano ya nchi gani itatoa ardhi kwa watu wanaoitwa wawekezaji wa nje katika ardhi kwa haraka na kwa bei ya chini zaidi?
Kweli ya kuwa Uhuru ni ardhi, siyo kuwa na wimbo wa taifa, si kuwa na bendera au kuwa na mzawa analala Ikulu haizingatiwi tena.
Tofauti ya Marais wengi wa nchi za Afrika na “colonial governors” ni ndogo. Nasikitika kulisema hili, lakini ni kweli.
mkali@live.co.uk
05/06/2021.









