0 0
Read Time:2 Minute, 4 Second

WU®

Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Geita ulioanza kutumika tarehe 09 Januari, 2021 kwa masafa ya Geita-Dar es salaam kwa ndege ya Shirika la Ndege ATCL ndani ya muda mfupi umehudumia zaidi ya abiria elfu tatu na wamekua wakiongezeka kadiri siku zinavyokwenda.

Hayo yamebainishwa leo Januari 26, 2022 wakati wa ziara ya Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Geita ilipotembelea kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja huo uliopo wilayani Chato ambao unatekelezwa na Mkandarasi Mzawa Mayanga Constructions Co. Ltd chini ya Usimamizi wa TANROADS Mkoa kwa Tshs. Bilioni 58 ambapo hadi sasa zimeshalipwa Bilioni 47.7 na ujenzi umefikia 95.

“Uwanja huu ukikamilika kuna mahusiano makubwa ya Kibiashara na Utalii kwenye hifadhi zetu za Rubondo na Burigi Chato pamoja na kupokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuja kwenye matibabu kwenye hospitali ya kanda ya chato hivyo tumsimamie Mkandarasi akamilishe kwa wakati.” Mwenyekiti CCM Mkoa, Mhe. Said Kalidushi.

Mwenyekiti wa Bodi ya barabara Mkoa wa Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiletea nchi maendeleo kwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mbalimbali ya Maendeleo.

“Sisi kama Mkoa tunamshukuru Rais Samia kwani ametupa fedha nyingi sana za miradi ya kimkakati kama uwanja huu ambao una viwango vikubwa sana na upo imara tangu umejengwa haujawahi kupata shida na tunawaomba ATCL waturudishie ruti ziwe tatu kama zamani kwakua abiria ni wengi sana.” Mwenyekiti Bodi ya Barabara Mkoa.

“Ujenzi wa kiwanja hiki ulianza 2016 na zaidi ya asilimia 95 zimefanyika kwa kujenga barabara ya kutua na kuruka ndege ya KM 3 kama sehemu ya kwanza ya mradi na sehemu ya pili ni ujenzi wa jengo la Abiria la VIP na tatu ni barabara ya kuingilia kwenye uwanja huu pamoja na kazi chache zilizobaki kama kusafisha eneo la kutua ndege na kuweka taa kwenye njia ya kuingilia kiwanjani hapa.” Meneja wa Uwanja, Sixbert Aidan.

Mapema, bodi ya Barabara imekagua barabara ya Bwanga- Biharamulo KM 67 ambapo kwa upande wa Geita ina KM 25 iliyojengwa kuanzia 2012 na kukamilika 2019 kwa Bilioni 66.7 huku ikiwa na uwezo wa kubeba tani 56 na kamati hiyo imeitaka TANROAD kuisimamia vizuri kwa kuboresha kasoro ili idumu muda mrefu.

Vilevile, Bodi ya Barabara Mkoa imekagua sehemu ya Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Ntarambe- Vijana-Leahnsabi ya kiwango cha lami zenye KM 02 unaotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 1 fedha kutoka Mfuko wa Barabara ambapo bodi imewaagiza TARURA kutoa Elimu kwa wananchi ili waitunze barabara hiyo.

Paul Zahoro
Geita, RS.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %