
WU® MEDIA
Na Dk Juma Mohammed
Ikiwa leo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 59 tangu pale wazalendo wa Zanzibar wakiongozwa na Chama cha Afro Shiraz (ASP) walipofanikisha mapinduzi yaliyokata Utawala wa kikoloni.
Si muda mrefu sana, lakini kama umri wa Mapinduzi ungelikuwa ni binadamu basi tungeweza kusema kuwa ni mtu mzima anayeweza kupambanua mema na mabaya.
Sababu kubwa ya kufanyika Mapinduzi yalikuwa ni kupinga dhulma ya aina yoyote, uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji na kubwa zaidi kuweka hali za wananchi sawa,kuondosha ubwana na utwana.
Baada ya Mapinduzi, People’s Republic of Zanzibar chini ya ASP ilitangza huduma za afya bure, elimu bila malipo, kugawa ardhi eka tatu tatu kwa kila mwananchi, kupiga marufuku vitu kuwekwa reheni na yote ya ukandamizaji yaliondoshwa.
Wakati leo tukiadhimisha Miaka 59 ya Mapinduzi ni muhimu kueleza ijapokuwa kwa ufupi sana chaguzi zilizofanyika Zanzibar hadi pale Wazalendo wa Kiafrika walipoamua kufanya Mapinduzi chini ya ASP.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kihistoria, Ameir H. Ameir ameandika katika kitabu cha historia fupi ya Zanzibar kuwa historia ya Zanzibar kati ya karne ya 13 na 19 inakabiliwa na tatizo kubwa la kukosekana kwa ushahidi wa kutosha wa maandishi.
Anasema wanahistoria wengi walioandika kuhusu historia ya Zanzibar kabla ya ukoloni kama vile Sir John Gray, Freeman Grenville na Ingrams, maelezo yao yanajiegemeza zaidi kwenye karne ya 18 na 19 na kufanya upungufu wa masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya wakati wa nyuma.
Tangu kufika kwa wageni katika upwa wa Afrika Mashariki, siasa ya Zanzibar imekuwa ni ya visa na mikasa yenye kuambatana na misuko suko ya kila aina na imekuwa ikibadilika kwa kiwango kidogo sana.
Bila shaka bado Jumuiya hizi mnazikumbuka, African Associaton, Arab Association, Shiraz Association, Hadharamout Association,Comorian Association na Indian Association. Jumuiya hizo ziliundwa katika kutukuza ukabila na utabaka.
Upepo wa mabadiliko ulianza kuvuma Afrika na sehemu nyengine ya dunia walikokuwa wakitawaliwa na wakoloni, kwenye ukandamizaji.
Vyama vya siasa vikaanza kuundwa mwishoni mwa Miaka ya 1950s.
Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichokuwa kikibebwa na Utawala wa Kisultan kilianzishwa mwezi Desemba mwaka 1955. Wahafidhina wengi wa kiarabu walikiunga mkono Chama hicho.
Waafrika wa Zanzibar hawakubaki nyuma, Jumuiya ya Waafrika iliyoanzishwa mwaka 1934 na Jumuiya ya Washiraz iliyoanzishwa mwaka 1938 zikaungana Februari 5 Mwaka 1957 na kuzaliwa kwa Chama cha siasa cha Afro Shiraz Party (ASP).
Siku ya kuunganishwa kwa African Association na Shiraz Association pale Muembe Kisonge, Kiongozi wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere alishuhudia tukio hilo la kuzaliwa kwa ASP.
Baada ya kuanza kwa shughuli za kiaisa, uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwezi Septemba, 1957 na ulishindaniwa na vyama vitatu ambavyo ni ZNP, ASP na Chama cha Kiislamu ambacho wafuasi wake wengi walikuwa ni Wahindi.
Kwa kuwa Zanzibar ilikuwa ikilindwa na Uingereza kama Himaya yake kuanzia Mwaka 1890 wakimlinda Sultan hadi mwaka 1963, Kabla ya kuanza kwa Uchaguzi huo, Uingereza ilimtuma mtaalamu wake, Sir Walter Coutts kufanya kazi ya kuandaa Uchaguzi huo.
Miongoni mwa mapendelezo ya Sir Coutts, Baraza la Kutunga Sheria liwe na Wajumbe 12 kwa upande usio wa Serikali na kati ya hao Wajumbe 6 wawe wa kuchaguliwa na waliobakia wawe wa kuteuliwa ambapo chini ya mapendekezo hayo kuliwekwa masharti ya mtu kuweza kupiga kura na kugombea.
Kulingana na ripoti ya Sir Coutts masharti ya mtu kupiga kura yalikuwa ni magumu sana na kwa sehemu kubwa Waafrika walikuwa wakibanwa na kuwekewa mazingira magumu ya kuweza kushinda kupitia ASP.
Walioruhusiwa kupiga kura walikuwa lazima wawe raia wa Sultan, akina mama walikataliwa, lazima mtu ajuwe kusoma na kuandika Kiswahili, Kiingereza au Kiarabu na pia mpiga kura alitakiwa awe na mali ya thamani ya shilingi 3,000/= au pato la hakika kwa mwezi shilingi 1,500/=.
Katika Uchaguzi huo, ASP ilishinda viti vitano na kimoja kikachukuliwa na mgombea wa kujitegemea aliyeunga mkono ZNP wakati ZNP hawakupata kitu.
Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha katika kitabu kilichoandikwa na Minael – Hosanna Mdundo anasema “baada ya Hizbu kushindwa vibaya katika Uchaguzi huu wa kwanza walianzisha visa na vitimbi mbalimbali ambavyo lengo lake lilikuwa mapambano dhidi ya Afro-Shiraz Party”
Katika masimulizi yake, Sheikh Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa zamani wa ASP anasema kwa kuwa Waarabu wengi ndio waliokuwa Hizbu na wengi ndio waliokuwa wanamiliki mashamba ambako Waafrika wengi walikuwa wanaishi na kulima ambao wengi wao ni wanachama wa ASP walifukuzwa mashambani na makazini.
ASP baada ya kuona watu wake wengi wamekufuzwa mashambani na makazini hasa bandarini waliamua kubuni biashara ya kuuza kahawa kwa wanachama wao “tukatafuta fedha kuwanunulia mdele na seredani na jiko lake vile vile.
“Tukawanunulia seruni kwa kuwa muuza kahawa havai suruali, huvaa suruali kipande na kikoi au shuka juu basi mtu mmoja anapewa seredani moja, seruni moja na vikombe pamoja na buni ratili tatu za kuanzia”anasimulia marehemu Sheikh Thabit Kombo katika maelezo yake.
“Tukapiga marufuku wana –Afro –Shiraz kununua kahawa ya Washihiri au Wamanga tukasema “Gozi zuia fedha” na huo ulikuwa msemo wetu mkubwa siku hizo, anaeleza Sheikh Thabit Kombo.

Hatua hiyo ilikuwa ni kujibu mapigo ya Waarabu waliokuwa wakiwagomea madukani kuwauzia vitu pamoja na mikate katika bekari zao. ASP nayo ilianzisha bekari zake.
Uchaguzi wa pili ulipangwa kufanyika mwaka 1960, lakini kukatolewa hoja kwamba ni muhimu kupatikana kwa maendeleo ya kisiasa na demokrasia, Waziri wa Makoloni Ian Macleod alifika Zanzibar mwezi Desemba mwaka 1959 alipendekeza kuja kwa mtaalamu wa katiba.
Kutokana na hali hiyo Uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika Julai 1960 ukaahirishwa ili kutoa nafasi kwa mtaalamu wa katiba kutoka Uingereza, Sir Hilary Blood kufanya kazi.
Sir Hilary Blood Mei 28, 1960 aliwasilisha ripoti yake kwa Mwakilishi mkazi wa Kiingereza ripoti hiyo maarufu kwa jila la Blood Report ambayo haikuwa na matatizo ASP walikubali kuwa msingi mzuri kwa maendeleo ya katiba, lakini Hizbu-ZNP waliitakaa na kuichoma moto.
Chini ya mapendekezo ya Sir Hilary Blood wanawake waliruhusiwa kupiga kura, umri wa mtu kuweza kupiga ulipunguzwa kutoka miaka 31 hadi kufikia 25, Uchaguzi ukafanyika Januari 1961 ambapo ASP ilishinda viti 10, ZNP viti 9, Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) ilipata viti 3 na ZNP na ZPPP wakachanganya viti vyao na kuunda Serikali ya mseto.
Viongozi wa ZPPP Mohammed Shamte na Othman Shariff walikubali ombi la ZNP, Ali Shariff Mussa alikataa kukiunganisha kiti chake na ASP kwa uamuzi huo ASP wakawa na viti 11 na ZNP vilevile viti 11.
Kwa sababu hiyo, Mwakilishi mkazi wa Kiingereza alipendekeza mzee Abeid Amani Karume aunde Serikali, lakini kwa masikitiko mzee Karume hakuungwa mkono katika Baraza la Kutunga Sheria.
Nini kilifuatia? Mwakilishi mkazi wa Kiingereza akakitaka ZNP chini ya kiongozi wao Ali Muhsin Baruwani kuunda Serikali, lakini kama ilivyokuwa kwa Karume naye akashindwa!
Kutokana na hali hiyo ikapendekezwa ili kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar ni vema kukawepo na Serikali ya mseto ya vyama vyote viwili, Serikali ikaundwa, Chief Secretary wa Serikali ya Kiingereza akateuliwa kushika nafasi ya Waziri Mkuu, yeye aliteua Mawaziri, wawili kutoka ASP na wawili kutoka ZNP.
Uchaguzi wa tatu ulifanyika Juni 1, 1961, ASP kama kawaida yeka ilishinda viti 10, ZPPP viti 3 na ZNP 10, ZNP na ZPPP wakaunganisha viti na kuunda Serikali ya mseto. ASP ilimuomba sana Mohammed Shamte kuunganisha viti vyake, lakini alikataa.
Baada ya Uchaguzi huo uliotawaliwa na vurugu na fujo kumalizika , kukafanyika mkutano wa katiba katika mji wa Lancaster House London Uingereza, katika mkutano huo ZNP walipendekeza kuwepo na Serikali ya ndani na huku Sultan awe Mkuu wa nchi, Uchaguzi ufanyike baadaye kwa madai kwamba ukifanyika Uchaguzi kunaweza kutokea ghasia kama zile za Juni 1961.
ASP walipinga vikali hoja hiyo na wakati wote walikuwa wakisisitiza Uchaguzi kwanza na Serikali au Uhuru baadaye.
Pia ASP ilikataa katakata wazo la Sultan kuwa Mkuu wa Nchi mtawala katika mfumo mpya, aidha, ASP ilikataa pia wazo la kuunda Serikali ya mseto, kutokana na hali hiyo mkutano huo ukamalizika bila mafanikio.
Serikali ya Uingereza ilimteua Sir Robert Arundell kufanya uchunguzi wa matatizo ya kisiasa Zanzibar, Sir Robert alifanya uchunguzi wake mwaka 1962 kati ya mwezi Agosti na Oktoba ambapo na kutoa ripoti yake na kupendekeza mambo kadhaa ikiwemo kuongeza idadi ya majimbo ya Uchaguzi.
Pande zote zikakubali na kufanyika kwa Uchaguzi wa nne mwezi Julai 1963, lakini kwa mshangao wa wengi Uchaguzi huo haukufanyika na kukatangazwa Serikali ya ndani Juni 24, 1963.
Hata hivyo, Uchaguzi wa nne ukafanyika na matokeo ya Uchaguzi huo ni ASP kushinda viti 13, Unguja walipata viti 11 na Pemba viti 2 huku ZNP wakipata viti 12 Unguja na Pemba walipata viti 6 wakati ZPPP waliambulia viti 6 vikiwa vyote kutoka Pemba.
ZNP na ZPPP wakaendeleza uswahiba wao wa kuunganisha viti na kuweza kupata viti 18 na kuunda Serikali Julai 17, 1963 iliyokuwa chini ya Sultan kama Mkuu wa nchi na Mohammed Shamte kuwa Waziri Mkuu.
Baada ya Uchaguzi huo kukafanyika mkutano mwengine wa kujadili katiba na ikakubaliwa kuwa Uhuru wa Zanzibar utolewe Desemba 10,1963, lakini kutokana na mvutano juu ya Sultan kutakiwa na ZNP kuendelea kuwa Mkuu wa nchi, ASP ilipinga Uhuru huo kwa sababu Sultan ni mkoloni ambaye alitakiwa kuondoka kama walivyoondoka Waingereza.
Mume wa Malkia wa Uingereza , Prince Philip alikabidhi Uhuru bandia Desemba 10, 1963 kwa Sultan, kutokana na ukweli kwamba Zanzibar ilikuwa bado mikononi mwa Sultan na vibaraka wake , ASP iliwaongoza wananchi wazalendo kufanya mapinduzi Januari 12, 1964.
Tuna kila sababu leo kutembea kifua mbele kusherehekea Miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Miradi mingi imezinduliwa, kuanzia Skuli, Hospitali za Wilaya na Mikoa na miradi mengine ya maendeleo. Hatua ya maendeleo ni kubwa ukilinganisha na kule tulikotoka katika Utawala wa Kikoloni wa Kisultan.
Mwisho.








