Tanzania na Burundi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya nchi hizo ulimalizika mkoani Kigoma tarehe 5 Machi 2021.
Makubaliano yaliyofikiwa yamejikita kwenye maeneo kuimarisha sekta za siasa na mahusiano ya kidiplomasia, ulinzi na usalama, maendeleo ya miundombinu, ushirikiano katika sekta ya uchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wa watu wake kupitia jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi nyingine ikiwemo Burundi.
Ameongeza kuwa, Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi na kuinua maisha ya watanzania. Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeendelea kuwekeza na kuboresha sekta mbalimbali pamoja na kujenga miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219.