0 0
Read Time:2 Minute, 45 Second

Anaandika MKWERU ZAKARIA MASWALE

Tarehe 09th June 2021 kwenye mahojiano kupitia kipindi cha Agenda kinachorushwa na kituo cha Luninga cha Startv, kinachoongozwa na mtangazaji Alloyce nyanda, mmiliki wa kituo hicho Mhe. Anthony Dialo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza, alimdhalilisha marehemu hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa namna ambayo alimvunjia heshima mjane wa marehemu pamoja na familia kwa ujumla.

Kwenye tukio hili ambalo ni la utovu wa kimaadili uliopitiliza, hatukuona kauli ya Chama cha Mapinduzi kupitia kwa msemaji wake, Katibu Mkuu wake au Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, japo kulaani na kukemea udhalilishaji huo. Watu waliojitokeza kulaani kitendo hicho ni Katibu Mkuu wa UVCCM Kenani Kiyongosi pamoja na mbunge wa Geita Vijijini Mhe. Joseph Kasheku @Msukuma.

Kupitia tukio hili, wengi tulijiuliza ile Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi huwa inachukua hatua kwa matukio yapi ya utovu wa kimaadili kwa wanachama wake, iwapo tukio hili limefumbiwa macho? Tumejiuliza pia, kama halikukemewa na mamlaka, Je, lilikuwa la kupangwa.

Hakuna mtanzania asiyefahamu kuhusu utumishi uliotukuka ulioachwa na hayati Rais Magufuli. Ni kiongozi aliyegusa maisha ya watanzania wa kila kada. Ni Rais aliyepigania rasilimali za nchi yetu kwa uwazi. Ni kiongozi aliyejipambanua kuwa mzalendo kwa taifa lake. Kitendo cha kudhalilishwa kupitia chombo cha habari, na Mamlaka ya Mawasiliano TCRA ikashindwa kukichukulia hatua za kisheria chombo hiki. Hivi mlitaka wananchi wenye hasira waliochukizwa na kauli ya Anthony Dialo wachukuwe sheria mkononi dhidi ya kituo hicho ndicho mjuwe watu walichukizwa?

Tukiachana na tukio hilo, kwa sasa mjadala uliopo nchini ni kuhusu chanjo ya Corona na usalama wake kwa watanzania. Kwa niaba ya Watanzania na waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima ambaye ni kiongozi wa kiroho na mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi, ameonyesha mashaka yake kuhusu usalama wa chanjo hiyo.

Huyu hakuongea kama mbunge wa Kawe wala hakuzungumza kama mwanachama wa Chama cha Mapinduzi, bali ameongea kupitia kofia yake ya kuwa kiongozi wa kiroho, ambapo mojawapo ya majukumu yake ni kuwaongoza waumini wake katika haki na kweli kwa mujibu wa maandiko na mafundisho ya mwenyezi Mungu. Huyu ni kiongozi wa kiroho mwenye haki ya kuwaonya wafuasi wake na wananchi kuhusu mbinu mbali mbali zinazotumiwa na Ibirisi shetani muovu.

Alichozungumza Askofu Josephat Gwajima ni kitu kinachohusu hatima ya maisha yetu ya sasa na kizazi kijacho. Mtu anayetetea uhai wa taifa lake, uhai wa wananchi wenzake dhidi ya njama za kibeberu inawezekanaje atishiwe kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu? Kuna siri gani iliyojificha ndani ya Corona ambayo ni dhambi watu kuhoji?

Tumekuwa tukishuhudia kupitia vyombo mbali mbali vya habari vya ndani, kimataifa, ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusu madhara yatokanayo na chanjo hizo ikiwemo damu kuganda kwa waliochanjwa, na hata kupoteza maisha. Katika baadhi ya nchi, kuongezeka kwa maambukizi licha ya watu kuchanjwa. Ni haki yetu kujadili, na kuhoji kuhusu usalama wa chanjo ya corona, kwa sababu ni kitu kinachogusa uhai na maisha yetu. Hatutaki Chama cha kuwaziba midomo watu bali tunataka serikali itowe maelezo na elimu ya kutosha kwa umma kuhusu usalama wa chanjo.

Nitowe rai kwa Chama cha Mapinduzi kwamba, kabla ya kumchukulia hatua kali za kinidhamu Askofu Josephat Gwajima kwa kuhoji kuhusu usalama wa chanjo ya corona, imchukulie hatua kwanza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza kwa kuidhalilisha familia ya hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %