![](https://www.tzabroad.com/wp-content/uploads/2021/08/SAVE_20210805_102502.jpg)
Tafakuri za ©️Kado Cool
Diaspora na Uraia pacha
Jana wakati nimemaliza kutuma makala inayomuelezea Raia wa Ujerumani mwenye asili ya Tanzania, mwanariadha Malaika Mihambo, nilipokea jumbe nyingi sana zinazolalamika kuwa Taifa la Tanzania linazidi kupoteza vipaji vingi huko nje kutokana na kutoruhusu kuwepo kwa Uraia wa pacha kwa wananchi wake.
Uraia pacha (Dual citizenship) ni hali ya Raia wa nchi moja kuwa na uraia wa nchi nyingine pia kwa wakati huo huo bila kuupoteza uraia wake wa awali. Yaani Mtanzania anaweza kuruhusiwa kuchukua uraia wa nchi nyingine na akaendelea kubaki kuwa raia wa Tanzania. Kwa kifupi Uraia pacha umekuwa ukionekana na baadhi ya watu kama ni Uraia wa fursa.
Kutokana na sheria zetu kutokubali suala hilo kwa mujibu wa Katiba, raia wengi wa Tanzania waishio ughaibuni wamejikuta wakiamua kupoteza uraia wa nchi zao kwa makusudi na kuchukua uraia wa nchi nyingine kutokana na mambo kadha wa kadha, lakini kikubwa zaidi kikionekana kuwa ni wepesi katika kuziendea fursa fulani za kimaisha huko walipo.
Ni ukweli ulio dhahiri kabisa kwamba raia hao hawakufanya uamuzi wa kulazimishwa bali kwa namna moja au nyingine mazingira yaliwafanya wajitafakari kubaki na uraia wa Tanzania na kukubali kubaki na changamoto fulani wakiwa ughaibuni au wachukue uraia wa huko waliko, ili kuweka wepesi wa hali lakini pia kupanua wigo wa fursa wanazoweza kupata huko waliko kama raia.
Pamoja na mazuri mengi yanayoonekana kuwapata baadhi ya Watanzania walioamua kubadilisha uraia wao na kuchukia uraia wa mataifa mengine huko nje, bado hilo haitoshi kufanya Watanzania wengi kuchagiza nchi yetu kukubali suala hilo kisheria ili isiweze kuwapoteza raia wake, kwani jambo hilo limeonekana kuwa na madhara makubwa mno kwa usalama wa nchi endapo litaruhusiwa.
Kwanza kabisa, Uraia pacha unaondoa ile dhana ya uaminifu usiogawika (indivisible loyalty) kwa nchi na Mamlaka Kuu ya nchi. Kama ambavyo mtu hawezi kutumikia wakuu wawili kwa wakati mmoja, vivyo hivyo mtu hawezi kutumikia (kwa maana ya uaminifu na utii) nchi zaidi ya moja.
Uraia pacha pia unaweza kuchangia kudhoofisha usalama wa taifa. Kwa mifano tu, baadhi yetu tunakumbuka miaka michache tu iliyopita kulitokea uvumi kwamba ofisa wetu wa Jeshi la Wananchi, tena mwenye dhamana ya kutunza au kushughulika na taarifa nyeti za kimawasiliano ametoweka.
Sote tu mashahidi kihoro tulichokipata kipindi kile na zaidi uvumi ulipozidi kuwa huenda amekimbilia nchi fulani ya jirani. Tukiwa na uraia pacha, hofu hii itaongezeka maradufu, hasa pale wenye uraia pacha watakapopewa dhamana ya madaraka makubwa na nyeti.
Kwa mfano wapo baadhi ya Watanzania ambao walisomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kuweza kuhitimu na kupewa dhamana na madaraka makubwa na nyeti. Leo hii hawako nasi tena nasi na inasemekana wamekwenda kwenye ile nchi ambayo ni kama ilizaliwa upya na inasemekana inapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Tuchukue mfano mwingine, leo hii Tanzania tuna sera ya kuhudumu katika Jeshi kisheria kwa vijana wetu kama sehemu ya kujenga ushupavu na kuimarisha uzalendo wao. Tukiwa na uraia pacha tujiandae kuwa na Warundi, Wakongo, Wamarekani, Wakenya na Wasomali JKT tukiwafundisha uaminifu, utii na namna ya kuipenda Tanzania kwa moyo wote hata na ikibidi mpaka tone la mwisho la damu yao.
Zaidi ya yote, Uraia pacha unavunja msingi wa haki ya usawa kwa sababu katika taifa moja, raia wanawekwa katika mafungu, wale wenye uraia wa zaidi ya nchi moja, ambao wanakuwa na haki zote nchini na haki zaidi kwingineko dhidi ya wale wenye uraia mmoja, ambao wana haki zote za hapa nchini pekee, lakini wote wako sawa nchini.
Uzoefu wa nchi ya India na Ethiopia ambazo hazina na zimesita kutoa uraia wa nchi mbili kwa sababu za kiulinzi na usalama, lakini zimetoa hadhi maalumu kwa watu wenye asili na nasaba ya nchi hizo, ambao wameacha kuwa raia wa nchi hizo.
Katika Katiba ya India, watu hao wanaitwa ‘Persons of Indian Origin’ na wana hadhi maalumu. Kwa mujibu wa sheria za India, mtu mwenye asili au nasaba ya India hadi kizazi cha nne, atapata hadhi ya ‘Person of Indian Origin (PIO)’, isipokuwa kwa raia wa nchi za Afghanistan, Bangladesh, Bhutan, China, Iran, Nepal, Pakistan na Sri-Lanka.
Watu wenye hadhi ya PIO wanaweza kupata fursa zifuatazo: Kupata kadi ya kitambulisho cha PIO. Hahitaji viza ya kuingia na kutoka India. Anaweza kukaa miezi sita nchini India mfululizo bila kulazimika kujiandikisha uhamiaji. Wana haki sawa ya kupata huduma za kiuchumi, kifedha na elimu kama ilivyo kwa raia wengine.
Wana haki ya kununua, kumiliki, kuhamisha, kuuza mali isiyohamishika isipokuwa kwa mashamba makubwa ya kilimo. Watoto wao wana haki ya kudahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu nchini India. Wana haki ya kupata makazi katika utaratibu unaosimamiwa na Serikali au wakala wake.
Hata hivyo, watu wenye hadhi ya PIO hawana haki zifuatazo: Hawaruhusiwi kupiga kura na hawaruhusiwi kugombea nafasi yoyote ya kisiasa wala kushika madaraka ya utawala.
Ukisoma Kitabu cha taarifa na chenye kumbukumbu (Encyclopedia) cha Chuo Kikuu cha Stanford, kinatafsiri uraia (citizenship) kama uanachama katika jamii ya kisiasa na unaonufaika na haki, pamoja kuwa na wajibu katika uanachama huo. Dhana ya uraia inajumuisha mambo matatu.
(Moja); Kwamba uraia ni hadhi ya kisheria inayotafsirika kwa haki za kiraia, kisiasa na kijamii. Hapa, raia ni mtu anayekwenda kwa mujibu wa sheria na ana haki ya kupata ulinzi wa kisheria. (Mbili); ni raia kama mawakala wa kisiasa wanaoshiriki kikamilifu katika taasisi za kijamii na kisiasa.(Tatu); ni raia kama wanachama wa jamii ya kisiasa inayoakisi aina fulani ya utambulisho.
Utambulisho katika dhana ya uraia ni jambo muhimu sana. Utambulisho huakisi uhusiano alionao mtu au raia moja kwa moja ama kiasili au kinasaba na jamii fulani ya kisiasa.
Ikumbukwe katika suala la uraia, nchi (State), inatafsiriwa kama Mamlaka Kuu (Sovereign Authority), yenye mamlaka kamili ya kutawala watu katika eneo lake linalotambulika. Kama ilivyo mipaka ya kisheria ya nchi inayoonyesha ukomo wa eneo lake, ndivyo dhana ya uraia (citizenship) inavyoonyesha na kutambulisha watu walio chini ya Mamlaka ya nchi fulani.
Leo hii nchi siyo tu ni nguvu za dola na taasisi zake mbalimbali, bali pia ni jumuiya ya wananchi kama wanachama. Uraia kwa maana hiyo, ndiyo uanachama katika nchi. Kama ilivyo katika vilabu vya mpira wa miguu, mfano Yanga au Simba, mtu unaweza kuwa mwanachama wa Yanga au Simba, lakini siyo vilabu vyote viwili kwa pamoja.
Tunapopaza sauti kulilia uraia pacha kwa sababu ya kuangalia fursa za kimaendeleo za watu wetu, ni vyema pia tukafahamu kuhusu changamoto zinazopelekea Serikali yetu kuendelea kukataa suala hili kwa maslahi mapana ya taifa kuliko kuangalia faida chache ambazo zinaweza kulitia matatizoni Taifa letu endapo zitaruhusiwa.
©️Kado Cool