Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Godfrey Chongolo, akiambatana na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kukagua miradi na shughuli za maendeleo mkoani Dar Es Salaam, amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali wanaohusika na kuidhinisha fedha za miradi ya ujenzi kutofanya hivyo kwa wakati licha ya Serikali kutenga na kuwepo kwa fedha za miradi hiyo.
Katibu Mkuu ameyasema hayo akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa soko la kisasa la Tandale Manispaa ya Kinondoni ambapo ujenzi huo unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 8.7 ulianza tangu mwezi Septemba, 2019 ukiendelea nje ya muda uliotarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2020, jambo linalosabisha kero kwa wananchi kutokana na adha ya kukosa mahali pa kufanyia biashara kama ilivyokuwa hapo awali.