Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Jumanne tarehe 31 Agosti, 2021.
Serikali ya Denmark kupitia kwa Waziri wake wa Ushirikiano na Maendeleo Mheshimiwa Flemming Moller Mortensen tarehe 27 Agosti, 2021 ilijulisha Tanzania kuwa itafunga shughuli za Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam pindi ifikapo mwaka 2024 kwa kuzingatia muongozo wa ibara ya 43 (a) ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Uhusiano wa Kimataifa unaozitaka Nchi kuzitaka Nchi kuzijulisha Nchi zilizopokea uwakilishi pindi shughuli za kibalozi zinapoelekea ukingoni.
Kitendo cha Serikali ya Denmark kufunga shughuli za Ubalozi itakapofika mwaka 2024 maana yake ni kuwa kuanzia mwaka 2025 mahusiano baina ya nchi hizi mbili yataathirika pale ambapo patahitaji ushiriki wa balozi wa Denmark kwa kuzingatia kazi za balozi zilizoainishwa katika ibara ya 3 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 yaani Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961 ambazo ni uwakilishi wa Denmark hapa Tanzania, ulindaji wa maslahi ya Denmark hapa Tanzania pamoja na ya raia wa Denmark wanaoishi hapa nchini mfano kocha wetu wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu, Kim Poulsen na wadenish wengine waliopo, kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wakuu wa nchi ya Tanzania na kazi ya kutoa ripoti za kibalozi (flash and quarterly reports) juu ya kinachojiri au kitakachojiri ndani ya Tanzania kwa wakati huo.
Kwa maoni yangu ni kuwa shughuli hizi zitaathirika moja kwa moja kutokana na kwamba zinahitaji jicho la kiuchunguzi la kibalozi au uwepo wa Balozi katika ardhi ya Tanzania. Hii ndiyo sababu husemwa kuwa mabalozi ndiyo macho na masikio ya wakuu wa nchi na serikali waliowatuma, na ndiyo sababu pia katika Diplomasia balozi ‘hutumwa’ katika nchi nyingine hapelekwi bali anatumwa ndiyo maana linatumika neno Sending State and Receiving State.
Lakini pia tufahamu kuwa uhusiano wa Kimataifa unaongozwa na misingi mikuu mitatu, lakini hapa nitaitaja miwili kwa muktadha wa kitendo cha Denmark kuweka nia ya kufunga shughuli za ubalozi ifikapo mwaka 2024; misingi hii ni kutegemeana (interdependency) na ulipaji ama reciprocity.
Ni wazi kuwa serikali ya Denmark na hata nchi nyingine zote duniani zinatambua kuwa katika dunia hii nchi haiwezi kuishi kwa kujitenga (in isolation) ni lazima iishi kwa kutegemeana na nchi nyingine (interdependence).
Ndiyo maana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema neno hili mara kwa kuwa “Nchi yetu siyo kisiwa” akiwa na maana kuwa ni lazima itegemee nchi nyingine na pia nchi nyingine ziitegemee Tanzania kwani hata hivyo Visiwa kiuhalisia vinaishi katika mfumo huu wa kutegemeana.
Lakini pia sote duniani tunatambua kuwa katika diplomasia kuna ulipaji ambapo katika diplomasia yenyewe hutumika neno reciprocity, ikiwa na maana ya kwamba anavyokufanyia mwenzako nae anatarajia umfanyie kama ambavyo yeye alikufanyia. Kwa sababu hii basi kwa mfano, tunaona kuwa hata viongozi wetu mfano Rais wetu akialikwa nchi nyingine tutarajie kuwa nae Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ataawalika hao viongozi. Hii ndiyo reciprocity.
Wazaramo wana msemo wao mmoja wanasema; “Adile nguku wa Mbwiga kaja nguku wake”, kwa tafsiri yangu ya Kiswahili ni kwamba aliyekula kuku wa rafiki yake (mbwiga ni rafiki) amekula kuku wake, falsafa iliyopo hapa ni kwamba ukialikwa au ukienda kwa rafiki yako akakuandalia kuku au chakula kizuri sana jua hujakula chakula chake au kuku wake huyo rafiki yako bali umekula chakula chako na kuku wako mwenyewe kwa sababu itakupasa nawe umualike kwako na umuandalie chakula kizuri na umchinjie jogoo wako na huenda ukajikuta unamchinjia jogoo kubwa unalolipenda, je hujakula kuku wako mwenyewe? Hii ndiyo reciprocity katika Uhusiano wa Kimataifa.
Kwa maoni yangu nadhani hapa kwenye reciprocity sisi kama Tanzania tuna changamoto ambazo kuna haja kwa mamlaka za maamuzi kuzifanyia kazi.
Kama alivyosema Waziri Ushirikiano na Maendeleo wa Denmark Mheshimiwa Flemming Moller Mortensen katika mawasiliano yake na Waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Denmark ilifungua Ofisi yake ya Ubalozi Tanzania mwaka 1963. Sasa tujiulize sisi kama Tanzania tulifanya hii reciprocity kufungua ubalozi Copenhagen?
Nimesoma Mkakati wa Denmark ‘The World We Share: Denmark’s Strategy for Development Cooperation’ uliotoka Agosti, 2021 kuna maneno yamenifikirisha mara mbili mbili katika muktadha wa Diplomasia kwa kuwa Diplomasia hutumia maneno ya kificho sana kufikisha ujumbe, si ajabu kwamba Winston Churchill aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza katika vipindi viwili vya Vita Kuu za Dunia aliposema, “Diplomacy is the art of telling people go to hell in such a way that they ask for directions.” Kwa tafsiri yangu isiyo sahihi ni kuwa ‘Diplomasia ni sanaa ya kuwaambia au kumwambia mtu nenda zako motoni kiasi kwamba mtu huyo au watu hao wanakuomba uwaelekeze njia ya kuelekea huko.” Unaweza ukaona diplomasia ilivyo.
Ninajaribu kutazama maneno haya yaliyoandikwa kwenye Mkakati huu wa Denmark yanayosema:
Our efforts will focus on where the needs are greatest.
Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba, ‘Juhudi zao zitaelekezwa kule ambapo mahitaji ni makubwa mno’.
Tujiulize je sisi hatuna mahitaji makubwa ya uwepo wa uwakilishi wao wa kibalozi hapa Tanzania? Tumefanya nini kutimiza reciprocity?
Mbali na hilo Mkakati unaendelea kusema:
“The World We Share” is fundamentally about solving the great challenges of our time together with our partners…Based on our shared Nordic values…We wish to form partnerships with carefully selected partner countries where the needs and challenges are greatest.
Kwa tafsiri yangu isiyo sahihi ni kwamba, Mkakati huu wa Denmark lengo lake kuu ni kutatua changamoto zilizopo kwa kushirikiana na wabia, lakini kwa kuzingatia misingi mikuu mitano (values) ambayo ni uaminifu (Trust), uwazi (openness), usawa wa jinsia (gender equality), usawa wa kiuchumi (economic equality) na uendelevu (sustainability) ya nchi za Nordic ambazo ni Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden; Denmark itajenga ubia kwa kuchagua kwa makini sana nchi wabia kwa kuzingatia pale ambapo mahitaji na changamoto ni kubwa mno.
Hapa tunagundua kuwa neno ‘where needs are greatest’ kwa maana kwamba, ‘pale ambapo mahitaji ni makubwa mno wamelirudia mara mbili. Kimsingi hili linajengwa swali la mwanzo nililojiuliza kwamba wameona kuwa sisi hatuna mahitaji makubwa na uwepo wa shughuli za ubalozi wao hapa nchini?
Swali hili limenirudisha katika mambo makubwa mawili, ni wapi tuna uwakilishi wa moja kwa moja wa kibalozi katika nchi hizo za Nordic licha ya kuwa nchi hizo zina misingi inayofanana kama walivyobainisha katika Mkakati wao?
Ukitazama website ya wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki www.foreign.go.tz sehemu ya Diplomatic Missions Abroad utaona kuwa uwakilishi wa Tanzania katika nchi ya Denmark unapitia katika uwakilishi wetu uliopo pale Stockholm, Sweden.
Balozi wa Tanzania katika kituo cha Stockholm, Denmark anaiwakilisha Tanzania katika nchi nyingine 8 ambazo ni Finland, Norway, Denmark, Estonia, Ukraine, Iceland, Lithuania na Latvia.
Kwa mujibu wa ripoti za Kundi la Washirika wa Maendeleo yaani Development Partners Group kwa kifupi DPG, nchi za Denmark, Finland na Norway ni miongoni mwa nchi wahisani wakubwa hasa kwenye kusaidia Bajeti ya Serikali (General Budget Support), kubaini hili tazama www.tzdpg.or.tz, lakini licha ya umuhimu huo katika kutoa mchango mkubwa kwenye kusaidia bajeti yetu, bado Tanzania hatujawa na uwakilishi wa moja kwa moja katika nchi hizo yaani resident diplomatic mission pale Copenhagen.
Kwa mtazamo wangu nadhani hili linaweza kuwa sehemu ya changamoto ambazo nchi kama Denmark wanajaribu kutuonesha kwa njia ya kidiplomasia kwamba licha ya wao kufungua ofisi ya ubalozi tangu mwaka 1963 lakini sisi bado hatujafungua ofisi ya ubalozi pale Copenhagen, kwa nini?
Huenda pia hili linakuja kutokana na hatua ya Tanzania kufungua balozi mpya katika nchi nane duniani katika nchi za Qatar, Uturuki, Sudan, Cuba, Israel, Algeria, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) na Namibia na kuwasahau wao kama wabia au washirika muhimu wa maendeleo yetu. Rejea ‘Mafanikio ya Kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano’, ukurasa wa 7 wa hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya mwaka wa Fedha 2020/2021 iliyowasilishwa Bungeni na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi. Ukitazama ukurasa wa 171 wa hotuba ile, nchi ya Denmark imetajwa na kushukuriwa kama Mshirika muhimu wa Maendeleo ya Tanzania. Nadhani kuna hoja hapa.
Hoja yenyewe inakuja katika msingi wa swali. Najaribu kujiuliza kwamba, je kwa Tanzania kufungua balozi zetu katika nchi hizo 8 hakuwezi kuwa kumewafanya Denmark waone kuwa labda hatujaona umuhimu wa uwepo wa mwakilishi/balozi pale Copenhagen kwa kuzingatia kuwa Sera yetu mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 ‘Tanzania’s New Foreign Policy’ inayoielekeza nchi katika Diplomasia ya Uchumi imebainisha wazi katika ukurasa wa 12 pale iliposema ‘Promotion of deeper economic cooperation with our development partners’?
Kwa tafsiri yangu isiyo sahihi ni kwamba Sera yetu inaelekeza, ‘Kuendeleza uhusiano wa kiuchumi kwa kina (deeper) na washirika wetu wa maendeleo.’
Huenda hili neno ‘deeper’ Denmark wametazama kama tungeenda zaidi hadi kwenye kufungua kituo cha ofisi ya Ubalozi jijini Copenhagen.
Najaribu kujiuliza, ni kwa kiasi gani tumeimarisha uhusiano hata kwa kufikiria kuwa na vituo cha ubalozi katika nchi ambazo ni wabia au washirika wakubwa wa maendeleo yetu kama Denmark niliowataja lakini pia Finland na Norway ambazo hatuna vituo vya ubalozi na badala yake tunatumia ubalozi uliopo Stockholm, Sweden? Kwa mtazamo wangu nadhani Denmark wanatukumbusha kuhusu reciprocity niliyotaja awali katika uhusiano wa Kimataifa,nadhani ni jambo jema na si baya.
Kwangu ninapata hisia na kudhani kuwa, inawezekana kitendo cha Tanzania kuendelea kufungua ofisi mpya za Ubalozi na kuzisahau baadhi ya nchi wadau/wabia aua washirika wakubwa wa maendeleo yake zimefanya nchi hizo zijifikirie kama kweli mchango wao kwa maendeleo ya Tanzania unathaminiwa. Huu ni mtazamo wangu.