0 0
Read Time:5 Minute, 18 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Jumapili tarehe 19 Septemba, 2021.

Katika pitapita zangu leo nilikutana na watu wakijadili safari za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ikiwemo safari ya leo aliyoenda kwa lengo la kuhudhuria kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Licha ya taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyobainisha wazi kuwa si tu Mheshimiwa Rais Samia atahudhuria kikao hicho cha 76 bali pia Alhamisi tarehe 23 Septemba, 2021 atalihutubia Baraza hilo.

Kwa kuona umuhimu wa kujenga uelewa wa pamoja juu ya safari za Rais nimeona haja ya kuzielezea aina tano za safari za viongozi kama Marais au Mawaziri Wakuu kwa nchi za Kifalme.

Marais wana aina nne au tano za safari, safari hizi ni ziara rasmi ya kitaifa (State Visit), ziara ya kiofisi (Official Visit), ziara ya kikazi (working visit), ziara ya kiofisi na kikazi (official working visit) na ziara binafsi (private visit).

(1) Ziara ya Kitaifa

Hii hufanyika kutokana na mwaliko wa kiongozi wa nchi moja kumualika kiongozi wa nchi nyingine kuhudhuria nchini mwake.

Mfano wa ziara ya aina hii ni pale Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipoalikwa na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kwa ziara rasmi nchini humo tarehe 4 na 5 mwezi, Mei, 2021.

Lakini pia ziara kama hiyo aliifanya nchini Rwanda kati ya tarehe 2 na 3 mwezi Agosti, 2021 kufuatia mwaliko wa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo.

Nadhani pia kati ya tarehe 16 na 17 July, 2021 Mheshimiwa Rais Samia alizuru nchini Burundi kufuatia mwaliko wa Rais Evariste Ndayishimiye

Ziara hii huambatana na kupigiwa mizinga 21, kukagua gwaride rasmi, kupewa zawadi, kuhutubia taifa na dhifa ya kitaifa kufanyika Ikulu ya nchi husika.

Inafaa kujiuliza, je Rais angekataa mwaliko?

Lakini pia tujiulize, kama Rais ana jukumu la kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje hatuoni kuwa atakuwa anakinzana na Sera yetu endapo asipoenda?

Tukumbuke Sera yetu ya Mambo ya Nje ambayo inaelekeza utekelezaji wa misingi ya Sera ya Asili (Traditional Foreign Policy) iliyotolewa kwa Waraka Namba 2 wa mwaka 1964 sambamba na hii ya mwaka 2001 imebainisha kuimarisha ujirani mwema kwa kusema ‘The/Promotion of good neighbourliness’ (Rejea ukurasa wa 4 na wa 10 wa Sera).

Hatuoni kuwa asipotekeleza wajibu huu wa kuimarisha ujirani mwema atakuwa amekiuka Katiba?

(2) Ziara ya Kiofisi

Hii ni ile ziara ambayo Rais huenda kuhudhuria vikao vya taasisi na Jumuiya za Kimataifa. Kwa mfano, kati ya tarehe 17 na 18 Agosti Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alisafiri kuelekea nchini Malawi kuhudhuria kikao cha 41 cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Vikao hivi ni vya lazima kwa mujibu wa Itifaki iliyoanzisha Umoja huu ya mwaka 1993.

Vikao hivi ni kama vile vya Umoja wa Afrika (AU), hivyo kuhudhuria kwake ni sehemu ya majukumu ya Rais ya Kiofisi ndiyo maana safari zake huitwa Ziara ya Kiofisi.

Je tulitaka Rais asihudhurie SADC?

Lakini kuhudhuria kwa Mheshimiwa Rais katika vikao vya SADC, EAC na AU ni kanuni iliyopo katika Sera yetu ya Mambo ya Nje inayoelekeza uimarishaji wa Umoja wa Afrika ama ‘The/Promotion of African Unity’ Rejea Ukurasa wa 4 na wa 10 wa Sera.

Je hatutaki Mhe. Rais atekeleze kanuni hii tuliyojiwekea?

Lakini kipekee Rais anatekeleza lengo la kuongeza kasi ya Ushirikiano wa kisiasa na kijamii na kiuchumi kikanda kama Sera inavyosema ‘To accelerate the political and social economic
integration for the region’ . Rejea ukurasa wa 11 wa Sera ya Mambo ya Nje ya 2001.

(3) Ziara ya Kikazi

Ziara hii ni ile ambayo Rais husafiri kwenda nchi nyingine au kukutana na Rais mwenzake kwa lengo la kusaini mkataba au kufungua jengo au kuzindua mradi fulani.

Kwa mfano, Rais Samia Suluhu Hassan alizuru nchini Uganda mnao tarehe 11 Aprili, 2021 ambapo alikwenda kwa lengo la kutiliana saini juu ya ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoim nchini Uganda mpaka Chongoleani, Tanga, Tanzania. Hivyo kilichowakutanisha ni kazi na ndiyo msingi wa safari za kikazi.

(4) Safari/Ziara ya Kiofisi ya Kikazi.

Hii ni ile ambayo kiongozi anakwenda kwenye mkutano mfano wa SADC halafu ndani yake kuna shughuli anaenda kuifanya baina yake na kiongozi wa nchi mwenyeji wa mkutano huo.

Kwa mfano wakati ule wa Mkutano wa SADC mwezi Agosti mwaka 2019 hapa Tanzania Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ndani ya kipindi cha Mkutano wa SADC alienda kutembelea Chuo cha Sokoine ambacho kilikuwa kikijulikana kama Solomon Mahlangu Freedom College sambamba na kuzuru makaburi ya wapigania ukombozi wa Nchi hiyo tarehe 16 Agosti, 2019.

Hapa tunaona alifanya mambo mawili, alitembelea Chuo cha Sokoine na baadae akahudhuria Mkutano wa Kilele tarehe 19 Agosti, 2019. Hii ndiyo ziara ya kiofisi ya kikazi.

(5) Ziara binafsi

Hii ni aina ya ziara ambayo Rais hufanya pasina kuzihusisha sana mamlaka za nchi nyingine au kupata mualiko huko.

Kwa mfano, marais wastaafu huwa na ziara binafsi katika nchi mbalimbali.

Lakini pia huweza kuwa ile ziara ambayo kiongozi huifanya akiwa katika muda wa mapumziko akaamua kuenda sehemu.

Au ziara ambayo haipo katika ratiba za kiongozi kwa wakati husika kwa mfano, pindi viongozi au Marais wakiwa kwenye mikutano rasmi (Summit) huweza kuwa na ratiba zao binafsi kuzuru sehemu mbalimbali za nchi husika kama mbugani n.k hii huwa ni safari binafsi.

Kwa mfano wa kipekee, safari hii ya kwenda Umoja wa Mataifa inatokana na Sera yetu ya Mambo ya Nje ambayo inaelekeza kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika kutafuta amani, usalama maendeleo duniani kama inavyosomeka; ‘Support for the United Nations in its search for international economic development, peace and
security.’ Ndiyo sababu pia Mheshimiwa Rais atahudhuria mikutano ya kilele ya kujadili mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu yaani SDGs. Hivi ndivyo utekelezaji wa Sera yetu ya Mambo ya Nje unavyoelekeza.

Kwa ufupi ni hayo, hivyo kinachofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo uhalisia wa Uhusiano wa Kimataifa ulivyo.

Lakini pia uhusiano huu una kanuni kadhaa ikiwemo ya ulipaji ama reciprocity hivyo tutarajie pia marais ambao walimualika Rais Samia Suluhu Hassan nao wataalikwa kuzuru Tanzania, ndivyo Uhusiano wa Kimataifa ulivyo.

Kwa mantiki hiyo hakuna ubaya wowote kwa Rais kusafiri pale anapoalikwa na Rais mwenzake, au anapoenda kwenye mikutano kama huu wa Umoja wa Mataifa au anapoenda kushuhudia utiaji saini wa makubaliano katika nchi ya jirani kama tuna mkataba nayo kwenye jambo fulani. Ndivyo uhalisia wa uhusiano wa Kimataifa ulivyo.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %