0 0
Read Time:3 Minute, 36 Second

Mwandishi anadadavua na kijibu kauli ya Mh Mbunge wa Ilala Mussa Hassan Zungu aliyetamka hivi karibuni,kuwa mradi wa bandari ya Bagamoyo uliositishwa na serikali ya awamu ya Tano ilikuwa ni kauli za uongo tu,hivyo lazima uendelee kama ulivyopangwa tokea Serikali ya awamu ya nne”……… Endelea

Na H. Mkali.
London, England
.

Mwanasiasa yoyote, wa cheo chochote wa Tanzania atakayeshabikia kujengwa kwa mradi wa Bagamoyo kwa mkopo/mikopo ya nje, basi mtu huyo ajitafsiri mwenyewe.

Mh.Zungu hapa anaongea akitetea mabeberu wanao tetewa hapa ni Wachina na Wa- Omani ambao wanawinda kututawala Watanzania kupitia mradi huu wa Bagamoyo.

1) Kusitishwa kwa ule mradi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano hakukuwa ni uamuzi wa mtu mmoja.
Serikali iliunda Kamati Maalumu ya Wataalamu wetu wenyewe waliobobea katika masuala ya uendeshaji wa bandari, uchumi, uanasheria nk . Baada ya uchambuzi na tathimini ya kina ya huu Mkataba: ukaonekana kuwa siyo tu ni wa kikoloni bali wa kitumwa.

2) Kamati yetu ya Wataalamu wazalendo wakawapa hao “Wawekezaji” marekebisho ambayo yangeufanya Mkataba uwe “win -win” kwao na kwetu; marekebisho ambayo yatatufanya sisi Watanzania tusipoteze uhuru wetu.
Lakini hao Wawekezaji, ambao mimi sisiti kuwaita washenzi (watovu wa ustaarabu) wakakataa kata kata. Hapo ndipo uamuzi wa kuufuta huu mradi ulifikiwa.

3) Huu Mkataba wa Awali wa Wachina tunao. Hayo Marekebisho yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano yapo. Hawa wanaoshabikia huu Mradi kama kweli wana nia njema na Taifa basi waweke mitandaoni huo Mkataba na Marekebisho yetu ili Wananchi wa Tanzania na Ulimwengu uone nani anasema kweli.

4) a) Malengo na madhumuni ya hii kampuni inayoitwa China Merchants Port Holdings Company Limited na Chartered Companies ni ya kikoloni kama nchi za Ulaya ambazo zilikuwa ndiyo chipukizi (pioneers) wa Ukoloni ni mamoja kabisa. Hamna tofauti.
b) Kupitia Chartered Companies nchi karibu zote za Afrika (isipokuwa Ethiopia) zilikuwa makoloni ya nchi za Ulaya.

c) Kupitia hii kampuni ya China Merchants Port Holdings Company Limited, leo hii:

  • China ina majeshi yake nchini Djibouti;
  • Bandari ya Hambantota nchini Sri Lanka pamoja na pande la ardhi lenye ukubwa wa eka 15,000 sawa kilometa 60 za mraba (60 sq. km) hivi sasa zinamilikiwa na China.
  • Kwa ajili ya Kampuni hiyo hiyo ya China na hii mikataba yake hovyo, hivi leo, China ni nchi ya pili duniani kwa kuuza mafuta, baada ya Saudi Arabia. Lakini hayo mafuta ni ya Angola. Mikataba hovyo ya sampuli ya huu wa Bagamoyo unawadhulumu wananchi wa Angola raslimali yao.
  • Hii Kampuni ya China imefanya leo jeshi la polisi la Zambia liwe na Wachina. Siyo Wazambia wenye asili ya Uchina, bali Wachina wenye uraia wa China wapo kwenye ngazi mbalimbali za jeshi la polisi la Zambia. Katika hali kama hiyo tutasema Zambia ina uhuru wa rangi gani?

5) Suala la kulizingatia kwa juhudi zetu zote ni hili: Mikataba ya hizo nchi zote zilizorejewa hapo juu: Sri Lanka, Djibouti, Angola, Zambia na huu Mkataba wetu wa Bagamoyo ni “identical twins” – ni pacha. Maana yake ni kwamba yanayojiri kwenye hizo nchi ndiyo ambayo yanatusubiri Watanzania kupitia Mradi wa Bagamoyo.

Sasa kiongozi wa ngazi yoyote nchini Tanzania, atakayesimama na kupigia chapuo tutekeleze mradi huu kwa mikopo ya nje tumsome vipi? Kiongozi huyu atakuwa ni wa kwetu au wa kwao?

6) Hebu tukumbushane kwamba Tanzania na Uhuru wa Tanzania siyo mali ya Serikali, siyo mali ya Bunge na wala siyo mali ya Mahakama. Ni mali ya Raia wote wa Tanzania.
Kikatiba yetu 1977, hayupo Rais, Spika wa Bunge au Jaji Mkuu mwenye madaraka ya kuuza nchi au sehemu ya nchi yetu. Aidha hayupo yoyote kati yao mwenye mamlaka ya kutangua uhuru wetu. Tanzania ipo huru milele. (Tanzania is free forever).

7) Mwaka 1968, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Tanzania ni ya Watanzania na Watanzania ni wote.” Ndiyo kusema Rais hawezi kuwa ni ‘wote’; Spika hawezi kuwa ni ‘wote’ na Jaji Mkuu hawezi kuwa ni ‘wote’. Alichokisema kwa tafsiri ni kuwa Viongozi wa ngazi zote ni wadhamini tu siyo wamiliki wa Taifa la Tanzania.
Mwalimu Nyerere aliweza kuuzingatia huu udhamini, lakini wafuasi wake wamekuwa na ‘tendency’ ya kujiona na kutenda kama Tanzania ni mali yao binafsi.

Hili ni lazima likemewe kwa sauti ya juu sana. Tanzania ni Jamhuri siyo Falme.

Mradi wa Bagamoyo hauna manufaa kwa Taifa ukitekelezwa kwa mkopo/mikopo ya nje. Aidha, mradi huu hauna haraka kiuchumi au kisiasa. Tuutekeleze kwa fedha zetu, hata kama itachukuwa muda.

mkali@live.co.uk
20/09/2021

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %