Na H.Mkali,
London, Uingereza.
“Wakati serikali ya Tanzania ikianisha jinsi itavyotumia mkopo wa zaidi ya shilingi trilioni 1.3, kutoka Shirika la fedha duniani IMF, kumezuka hoja mpya kuhusu deni la taifa linalodaiwa kuendelea kuongezeka.”
Madeni ya taifa duniani (kwa sehemu kubwa) huwa yanasababishwa na mifumo kandamizi ya kifedha na kibenki inayotawala ulimwengu wetu, wala si ukopaji holela wa viongozi.
Lakini kwa mujibu wa miradi mikubwa na huduma nyingi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati John Pombe Joseph Magufuli, hilo deni linalopigiwa kelele na Mheshimiwa Nape ni ndogo sana. (Hii nimechomekea tu, sasa narudi kwenye mada yangu).
1) Mfumo wa kifedha upo hivi: Kama watu wote duniani, Makampuni yote duniani na Mataifa yote yakiwa hayana madeni basi dunia itakaukiwa kabisa na fedha. Kwa maneno mengine hakutakuwa na senti hata moja katika mzunguko. “There will be no money at all in circulation.” Hivyo basi kuwepo kwa fedha kunategemea kuwepo kwa madeni.
Viongozi wanaohubiri juu ya kumaliza kulipa madeni chini ya mfumo wa fedha uliopo basi wanachokifanya ni kukimbiza vivuli vyao wenyewe.
2) Benki Kuu binafsi ndio chanzo kikuu cha madeni ya taifa duniani.
Kitu ambacho watu wengi hawafahamu ni kwamba Benki Kuu zao siyo mali ya umma bali ni makampuni binafsi kwa asilimia zote.
Hivi sasa nchi zenye Benki Kuu ambazo si binafsi ni: North Korea, Iran, Cuba, North Sudan na Syria. Hizi nchi mbili za mwisho kuendelea kwake kuwepo kwenye orodha hii hakuwezi kutabirika kwa usahihi wowote, baada ya Mapinduzi yaliyotokea Sudan hivi majuzi na vita vinavyoendelea huko Syria.
Nchi zingine ambazo Benki Kuu zao zilibinafsishwa baada ya kufunguliwa makopo ya demokrasia kwa mitutu ya bunduki ni: Afghanistan, Iraq na Libya.
3) Benki zinaiingiza vipi mataifa kwenye madeni?
Mataifa yanapotaka kufanya matumizi ya nakisi (deficit spending) huwa zinaomba Benki Kuu zao kuchapisha kiasi cha fedha zinazohitajika.
Baada ya fedha kuchapishwa huwa wanakopesha mataifa husika tena kwa riba ya asilimia sita (6%). Hili ndio deni la taifa nambari moja. Yaani hata nchi ikae mwaka mzima isikope fedha kutoka taasisi au taifa lingine lolote; lakini mwisho wa mwaka nchi hiyo itakuwa na deni la taifa – deni la Benki Kuu linalotokana na kuchapisha fedha.
Sasa naomba tutafakari hili:
Hebu tuchukue fedha zote ambazo JPM alitumia katika miaka yake mitano na miezi mitano, kutekeleza miradi yake – manunuzi ya vifaa na mishahara. Tuchukue fedha zote zilizotumika kulipa mishahara nchi nzima pamoja na malimbikizo ya mishahara ya nyuma. Fedha hizi zote zilichapishwa na Benki Kuu kisha ikakopesha Serikali kwa riba ya asilimia sita. Je, nchi itakosa kuwa na deni kubwa la Taifa?
4) Benki Kuu ndizo zinazozalisha sehemu kubwa ya madeni ya Taifa.
(a) Libya, chini ya Hayati Muammar Gaddafi, Benki Kuu yao ilikuwa ni mali ya umma. Kwa sababu hiyo wakati Mh.Gaddafi anauawa Libya ilikuwa haina deni. Mara tu baada ya kuawa kwa Gaddafi Benki ilibinafsishwa na hivi sasa Libya inaogelea kwenye bwawa la madeni.
(b) Marekani – USA.
Wanaoitwa Founding Fathers huko Marekani walijua udhalimu wa kuwa na Benki Kuu binafsi zenye kuchapisha fedha za nchi. Ndiyo sababu Ibara ya Kwanza ya Katiba ya Marekani imeweka jukumu la kuchapisha na kusambaza fedha nchini kwenye mikono ya Congress (Bunge lao).
Na Rais pekee aliyewahi kulipa deni lote la Taifa la Marekani, alikuwa ni Andrew Jackson, Rais wao wa saba. Na alifanikisha hilo kwa kuua iliyokuwa Benki Kuu ya Marekani ya zama zake.
Hivi leo, baada ya Bankers kutembeza rushwa, Benki Kuu imerudishwa kinyemela; na hii ndio sababu Marekani inaongoza kwa kudaiwa. Kuwepo kwa Benki Kuu yao inayokwenda kwa jina Federal Reserve System kunakiuka Katiba ya nchi hiyo na ndo kunakosababisha nchi kuwa kiranja wa kudaiwa.
(5) Gavana wa Benki kuchaguliwa na Rais.
Mara baada ya kuchapisha makala yangu kwenye gazeti la JAMHURI: Madeni ya taifa na mchakato wake, mdau mmoja alinipigia simu kutoka Dar na kusema : “…. lakini Benki Kuu yetu ni ya umma kwani Rais wetu ndio anamteua Gavana wake.”
Halafu mimi nilimuuliza kuwa si unasadiki kuwa ‘The Federal Reserve System’ ya Marekani ni Kampuni binafsi? Akajibu ndiyo. Halafu nikamueleza kuwa lakini Gavana wake anateuliwa na Rais wa Marekani.
HITIMISHO.
# Sehemu kubwa ya madeni ya Taifa duniani yanaletwa na hii debt-based monetary system niliyoielezea hapo juu, siyo ukopaji holela; ingawa ni sawa kabisa mataifa yajiepushe na huo ukopaji wa kiholela.
# Watu, kama kweli wanataka kujikomboa kutoka kwenye utumwa unaoendeshwa na mabenki hususani Benki Kuu (Central Banks), basi utaifishwaji wa benki kuu zote hauwezi kuepukiki.
# Aidha, Utaifishaji ukiwa ni mgumu, Benki Kuu zipigwe marufuku kwa sababu hakuna kitu chochote Benki Kuu inafanya ambacho Hazina isingaliweza kukifanya.
# Kodi za mapato zote za kila raia (ambayo ni sawa na kazi ya miezi mitatu kila mwaka) inakwenda kulipa hili deni la Benki Kuu. Deni ambalo halina manufaa yoyote kwa raia hao. Huu kama si utumwa mamboleo ni kitu gani?
Hivyo basi, ningalimshauri Mh. Nape alifanyie “homework” ya kina hili suala la madeni ya taifa, kwa sababu kauli yake ni potofu na inaweza kumpaka matope kiongozi ambaye hana hatia.
mkali@live.co.uk.
09/11/2021.