
Na Dr Yahya Msangi
Togo – West Africa
“Dr Yahya Msangi atoa Ushauri kwa Waziri wa elimu Prof. Ndalichako Pamoja na Wazazi”

Vijana wa kitanzania wa hizi zama na hâta baadhi ya wa zamani hawakubahatika kupitia shule zilizo toa kipaumbele kwa elimu ya ujasiriamali. Ujasiriamali hauwezi kuanza mtu akishaota manyoya makwapani au ndevu. Ujasiriamali huanzia utotoni.
Wizara inayopaswa kuwajenga watu wawe wajasiriamali ni Wizara ya Elimu. Wizara inadhani VETA ndio njia sahihi? Hapana. Anayeenda VETA tayari kapita umri wa yéyé kuwa mjasiriamali. Ujasiriamali sio kuwa fundi! Ujasiriamali wenye tija ni mtu awe mbunifu (innovator) au hâta awe anaboresha innovations za wengine. Kuwa fundi mchundo, fundi mekanika, mshona nguo n.k. ni ujasiriamali wa kizamani mnoo. Tutoke huko.
Je tunatokaje?
Lazima kuanzia chekechea watoto waanze kufundishwa ujasiriamali. Na havihitaji mtaji mkubwa sana. Kwa mfano watoto waanze kufundishwa namna ambavyo kikaptura au kigauni alichovaa kinavyotengenezwa kuanzia kikiwa pamba. Mfano watoto wafundishwe pencil, ruler, kikombe, héla, blackboard na vitu vingine vya kawaida vinavyotengenezwa. Tuache kuwapa watoto elimu isiyowasaidia kuwa wajasiriamali wa baadaye. Hii mambo ya kufundisha viungo vya mende, panzi, inzi, jongoo n.k. tuachane nayo.
Sehemu kubwa elimu ya msingi na sekondari wafundishwe kujua vifaa vinatengenezwaje na vinahitaji kuboreshwaje. Wafundishwe ni matatizo gani bado yanatatiza jamii shuleni na yanahitaji teknolojia ipi? Mfano wa matatizo: wizi wa vifutio, utoro, walimu kutongoza wanafunzi, wizi wa mitihani, vikojozi mabwenini, ajali za moto, walimu walevi wa kichaga, ukosefu wa maji na umeme, mbu, inzi, kunguni, funza, n.k. Watoe wajue namna ya kutatua matatizo yanayowazunguka kwa innovations!
Sio jitu halijawahi hâta kujua namna ya kuangamiza mbu unalipeleka VETA! Litakimbilia ufundi gari. Wenzetu watatengeneza magari sisi tutabaki kuwa wapiga nyundo gereji!
Nilikuwa nafundisha watoto ulaya na niliona watoto wa Shule ya msingi wanatengeneza software za kompyuta! Mtoto anatengeneza software ya taa za kuongoza magari mtaani kwao! Mitoto yetu ya shule za msingi kucheza ngoma sanaaa! PE! English Academy kibao lakini Hawajui hâta ruler inatengenezwaje!
Nchini Malaysia nilitembelea Jimbo la Penang. Ni kakisiwa jirani na Sumatra lakini kako Malaysia. Pale niliona Shule inafundisha technologies and innovations kuanzia chekechea hadi sekondari. Hawahangaiki kufundisha panzi, chawa na viroboto wakoje! Wanachofanya wanawapa watoto vifaa wakongolowe. Mfano feni, Saa, play station, tv, radio, drone, camera, simu, n.k. Mtoto anakongoloa! Anatakiwa achunguze chombo kinafanyaje kazi? Mfano feni. Nini inafanya feni izunguke? Nini inafanya tv ionyeshe picha, Nini inafanya simu ifanye kazi? Mpaka afike la 12 huyooo anakopeshwa kuanzisha kiwanda au anaajiriwa na kina Samsung ! Sasa hawa wetu wa kuchora tumbili wataajiriwa wapi?
Mheshimiwa Waziri wa Elimu hebu ibadilishe Wizara! Badilisheni mitaala! Acheni kufundisha watoto kuchora panzi ! Wafundisheni ujasiriamali.
Watanzania wapo wanaoweza kuwaonyesha njia! Tena bila malipo.
Wazazi: na NYIE ni SHIDA! Mpe mwanao moja ya simu zako aikongolea ajifunze innovation! Acha ushamba wa kuzipaki mezani pub watu waone una 3!
Akivunja TV usimbonde. Badili iwe faida. Mpe bisibisi aifungue kabisa ! Mwambie “rudisha ilivyokuwa na iwake”!!! Utakuwa umemsaidia. Badala ya kumpeleka grocery mwambie ” Nikirudi nikute umechora troli la umeme la kusombea taka hapa nyumbani” Mpe kalamu na karatasi nenda zako kalewe.








