Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Ijumaa tarehe 24 Desemba, 2021.
Alhamisi tarehe 23 Desemba, 2021 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi alitoa taarifa kwa umma juu ya kuunda Kikosi Kazi cha Wadau wa Demokrasia ya Siasa ya Vyama vingi waliopewa jukumu la kupitia hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa wadau hao wa tarehe 15 hadi 17 Desemba, 2021 jijini Dodoma.
Kikosi kazi hicho kina jukumu la kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye Baraza la Vyama vya Siasa na kuyawasilisha Serikalini.
Sifa za Wenyeviti na wajumbe wa Kikosi kazi hiki cha watu 23 zinatoa tafsiri kuwa kitakuwa mapendekezo yenye tija kwa mustakabali mwema wa nchi yetu.
Licha ya hivyo bado ninaamini kuwa kuna mambo ambayo sisi wengine kama wadau wa amani tunaweza kushauri pia wayapendekeze.
Pendekezo mojawapo kubwa ninaloona linafaa kuwasilishwa ni kuundwa kwa Baraza la Taifa la Amani na Siasa Nchini ama National Peace and Political Council (NPPC) kwa Kingereza.
Kwa nini Baraza la Taifa la Amani na Siasa nchini?
Tafiti nyingi zinaonesha wazi kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya kuvurugika kwa amani Afrika na masuala ya kisiasa hasa uchaguzi.
Kwa mfano Khadiagala (2018) katika ‘Regional Cooperation on Democratization and Conflict Management in Africa’ na Nordic Institute Africa (2018) katika ‘Peace and Security Challenges in Southern Africa: Governance Deficits’ wamefafanua hili, aidha Albuquerque na Wiklund (2015) katika ‘Challenges to Peace and Security in Southern Africa’ na UNSSC (2011) na katika ‘The Role of Election in Peace Processes’ nao wamebainisha kwa kina juu ya uhusiano wa uchaguzi na vurugu/migogoro Kusini mwa Afrika.
Vurugu hizi au migogoro huathiri sana maendeleo ya ukuaji wa uchumi barani Afrika.
Hivyo ni wazi kuwa kuna uhusiano mkubwa sana baina ya uwepo wa amani ya kudumu, matokeo ya harakati za kisiasa na maendeleo endelevu katika nchi yoyote duniani. Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa namba A/55/985-S/2001/574 ya mwaka 2001 ilibainisha hili.
Kwa mantiki hiyo wakati Kikosi kazi hiki kinaenda kutoa mapendekezo ni vema pia kitazame uhusiano uliopo baina ya amani, siasa na maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kwa kuwa pasipo amani hakuna maendeleo na pasipo maendeleo hakuna amani.
Misingi ya amani ilibainishwa na Taasisi ya Kupima Amani Duniani ama Global Peace Index katika ripoti yao ya mwaka 2007 kwa kutumia viashiria 22 katika nchi 162.
Ripoti hiyo iliainisha misingi minane ya amani ambayo ni uwepo wa serikali inayofanya kazi vema, mazingira mazuri ya biashara na mgawanyo sawa wa rasilimali ama keki ya taifa kati ya walio nacho na wasio nacho.
Misingi mingine ni kukubali haki za wengine, uhusiano mwema na majirani na upatikanaji huru wa taarifa.
Vile vile uwepo wa kiwango kikubwa cha watu walioelimika na uwepo wa kiwango kidogo cha rushwa katika nchi ni mambo yanayoleta amani. Kufahamu haya kwa kina, rejea andiko la Institute for Economics-IEP and Peace lenye kichwa Pillars of Peace: Financing the Attitudes, Institutions and Structures most closely associated with Peace la mwaka 2018.
Kwa mujibu wa IEP (2018) ni kwamba endapo serikali zitafanya kazi kwa kuzingatia mihimili minane ya amani kutakuwa na ustawi mkubwa wa binadamu.
Ustawi mkubwa wa binadamu unamaanisha kuwepo kwa kiwango kidogo cha athari katika biashara, pato la watu kuongezeka, kuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasilimali, kuongezeka kwa imani baina ya wananchi na kuimarisha kwa muingiliano baina ya jamii.
Kutokana na umuhimu na faida za kudumisha amani na misingi yake iliyoainishwa hapo juu nimeona ipo haja kwa Kikosi kazi kushauri kuundwa kwa Baraza la Taifa la Amani na Siasa la Taifa. Kwa nini?
Kwa sababu licha ya ukweli usipingika kuwa Tanzania inafahamika duniani kama kisiwa cha amani lakini naamini kuna umuhimu wa kuifanyia kazi mihimili hii ya amani ili kuzidi kuimarisha amani iliyopo.
Kwa nini nasema hivi?
Kwa sababu mihimili hii inafanya kazi kama mfumo na inapimika kwa kuzingatia mazingira imara na mazuri ya biashara na uwekezaji, usawa wa jinsia, uwazi katika utendaji kazi wa serikali na ujirani mwema.
Ninakiri kuwa haya yote Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inayafanyia kazi kwa makini lakini naamini kuna haja ya kuwa na Baraza la Taifa la Amani na Siasa ambalo litakuwa na kazi ya kufanya tafiti na kushauri juu ya uhusiano wa amani, siasa na maendeleo.
Kwa sasa kama nchi tuna Kamati ya Amani ya Kitaifa ambayo inahusisha zaidi viongozi mbalimbali wa dini.
Naamini kamati hii ni muhimu sana katika kusaidia kuimarisha amani nchini, lakini ni kwa kiasi gani kamati hii ina uwezo wa kutafiti na kushauri juu ya misingi ya amani na njia bora za kudumisha amani iliyopo? Hili ndilo swali la msingi la kujiuliza. Je hakuna uwezekano wa kuipanua kamati hii au kuiboresha kwa kuiunda upya? Hapa ndipo ninapoona hoja ya kukishauri Kikosi Kazi hiki cha watu 23 kishauri kuundwa kwa Baraza la Taifa la Amani na Siasa.
Kwa maoni yangu kuna haja ya kuhama kutoka kwenye Kamati ya Amani ya Kitaifa na kuwa na Baraza la Taifa la Amani na Siasa ama kwa Kingereza National Peace and Political Council (NPPC) ili nchi iweze kuwa na mfumo wa kitaalamu wenye kutafiti, kushauri na kutoa mapendekezo yenye kuleta tija zaidi kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina amani, harakati za kisiasa na maendeleo ya nchi.
Baraza la Taifa la Amani na Siasa lina umuhimu gani nchini?
Tafiti nyingi zinabainisha kuwa kuwepo kwa mfumo rasmi wa kuhanikiza amani husaidia kulinda raia na kuzuia viashiria vya migogoro katika nchi husika.
Kwa kuongezea ni kuwa Mabaraza ya Amani katika nchi hufanya kazi kama mfumo rasmi wa kitaasisi wenye kulinda amani, kuitafsiri migogoro na kuipatia ufumbuzi kwa maendeleo ya taifa. Haya yalibainishwa Tongeren (2011:45) na Hopp-Nishaka (2012) katika makala zao za kitafiti.
Kwa kukazia, nae Gressman (2016:4) anabainisha kuwa ili nchi iweze kuwa na amani ya kudumu mifumo ya kulinda amani inapaswa kuwa na wataalamu mbalimbali wabobezi, uwezo wa kutosha, rasilimali za kutosha kutekeleza majukumu yao sambamba na nyenzo za kutosha ili kujenga uhusiano mzuri baina ya jamii na kuzuia migogoro. Je hatuoni haja ya kuwa na Baraza la Taifa la Amani na Siasa?
Kwa mfano, nchi ya Ghana imefanikiwa sana katika hili la kuwa na Baraza la Taifa la Amani (National Peace Council ama NPC) tangu mwaka 2005 ilipounda Baraza hilo.
Baraza la Taifa la Amani la Ghana lina nguzo sita zinazolipata nguvu, nguzo hizi ni Mahakama, Bunge, Machifu, Tume ya Haki za Binadamu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Asasi za Kiraia.
Sisi kama Tanzania, Baraza letu la Taifa la Amani na Siasa (NPPC) linaweza lisifanane na hili la Ghana lakini linaweza kujumuisha wadau wote wa amani, siasa na maendeleo waliopo serikalini, sekta binafsi na AZAKI nchini ili kulipa upana na kina.
Hivyo nashauri Kikosi Kazi hiki cha Wadau wa Siasa ya Vyama Vingi kilichoundwa na Jaji Francis Mutungi kufuatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kiishauri Serikali kuunda Baraza la Taifa la Amani na Siasa ama National Peace and Political Council (NPPC) ili kama nchi tuweze kuwa na taasisi inayoweza kufanya tafiti mbalimbali, kushauri na kutoa mapendekezo juu ya nini kifanyike kudumisha amani na kuleta maendeleo endelevu nchini.
Wenu:
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Clubhouse|Twitter).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).








