
Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Alhamisi tarehe 30 Desemba, 2021.
Kumekuwa na mijadala mingi kuhusu hali ya deni la nchi na mikopo ambayo Serikali ya Tanzania inapokea kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hivi karibuni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Justino Ndugai aliamsha upya mjadala huo baada ya kutoa maoni yake alipokuwa katika kikao cha mwaka cha jamii ya Wagogo kilichofanyika Jumatatu tarehe 27 Desemba, 2021 jijini Dodoma.
Wengi waliyachukulia maoni ya Mheshimiwa Spika Ndugai kama kupingana na kile kinachofanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hivi sasa.
Spika Ndugai alisema na hapa ninamnukuu;
“Sasa 2025 mtaamua, mkitoa waliopo nayo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo ndiyo namna ya ku-run (kuongoza) nchi. Hivi sasa deni letu ni Seventy (70) trilioni…Kuna siku nchi itapigwa mnada hii.” Mwisho wa kunukuu.
Je ni kina nani hao ambao kazi yao itakuwa kwenda nje ya nchi kukopa? Labda wananchi wengi wanajiuliza swali hili.
Mheshimiwa Spika Ndugai aliedelea…
“Tumeenda Kukopa 1.3 trilioni, tunapiga makofi. tunawapa wazungu trilioni 10 mariba matupu. Wanatufanya sisi mazezeta. Hela yako Mwenyewe, anachukua hela yako, halafu anakupa kidogo unashangilia.” Mwisho wa kunukuu. Je mikopo ina shida gani? Labda tujiulize pia.
Katika kujibu hoja za wale wanaopinga Serikali kukopa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana msimamo wa Serikali Jumanne tarehe 28 Desemba, 2021 aliposhuhudia Utiaji Saini wa Mkataba wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha tatu kutoka Makutupora (Singida) mpaka Tabora chenye urefu wa Kilometa 368, katika tukio lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Rais alisema na hapa ninamnukuu;
“Kwa njia yoyote, kwa vyovyote tutakopa, tutaangalia njia rahisi njia zinazotufaa za kukopa kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani. Ni lazima tutakopa. Kwa hiyo tutakopa ili kukamilisha mradi huu!” Mwisho wa kunukuu.
Kutokana na kupishana huku kwa mitazamo ya kitaasisi nafikiri kuna haja ya kujiuliza, je mikopo ni mibaya? Kwa kiasi gani? Ama shida halisi ya mikopo ipo wapi?
Kutokana na sintofahamu hii, nitajaribu kuitazama mikopo, athari zake na faida zake kama njia ya misaada ya kigeni kutoka nchi au taasisi za Kimataifa ili kupata uelewa wa pamoja.
Tangu kuisha kwa Vita Baridi nchi nyingi zilizoendelea na taasisi zake zimegeuza mtazamo wake wa mahusiano ya kimataifa na sasa zikijikita zaidi kwenye kutoa misaada au mikopo.
Kwa upande mwingine ni dhahiri kuwa licha ya ukuaji unaovutia katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Afrika bado limeendelea kuwa bara linalotegemea sana misaada au mikopo kuliko bara lolote duniani. Rejea Resnick na Welle (2013:1)
Kusaidia na kutoa misaada limekuwa likitazamwa kwa shaka na hisia na tamaduni nyingi hasa kutokana na athari hasi zinazojitokeza kwenye misaada au mikopo hiyo kama ambavyo Riddell (2007) alipata kugusia.
Hisia hii inazua maswali si tu kwa wanaopokea misaada na mikopo bali hata wanaotoa. Kwa mfano, Elon Musk tarehe 31 Oktoba, 2021 alilitaka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (UNWFP) limueleze namna ambavyo litatatua tatizo la baa la njaa ili atoe asilimia 2% ya utajiri wake kwa kuuza Tesla moja atatue tatizo hilo ambalo UNWFP ilisema linahitaji asilimia 2 tu ya utajiri wa Elon Musk kuweza kulitatua.
Hapa tunaona wazi kwamba changamoto ya misaada kwa namna alivyohoji Elon Musk ni namna gani misaada au mikopo hiyo inavyotumika na kwa namna gani inawafikia walengwa.
Nchi zinazotoa misaada au mikopo hiyo mara nyingi pia zimekuwa zikijiuliza; ‘Je nchi masikini/zinazoendelea zina uwezo na nia ya kupokea misaada na kutumia misaada zaidi kwa dhati? Je misaada zaidi haitachochea rushwa, misaada zaidi kwenda kwenye mifuko ya watu wa kada ya juu (elites) na kushindwa kuwafikia wa chini kuwaletea maisha bora wale wenye uhitaji? Rejea Lancaster (2007).
Kutokana na hiki alichobainisha Lancaster tujiulize, je tuliwahi kupima kuona kama misaada au mikopo inachochea rushwa au lah?
Hofu hii juu ya utoaji na upokeaji mikopo inathibitishwa na yale yaliyotokea nchi ya Malawi mwaka 2013 katika kashfa ya Capital Hill Cashgate ambapo serikali ya Malawi ilipokea mkopo wa zaidi ya Dola za Marekani Milioni 250 kutoka IMF lakini fedha hizo zikielezwa kuliwa na watu wachache. Je hili si tatizo?
Kwa upande wa nchi zinazopokea misaada au mikopo nako mara nyingi wamekuwa wakijiuliza, ‘ni kwa nini tuendelee kuziamini nchi au taasisi wahisani wanaposema wana nia ya dhati ya kutusaidia kuondoa umasikini na mateso ya binadamu wakati muongo mmoja, miwili, mitatu au minne iliyopita walitoa ahadi kama hizo za kutusaidia na walitumia maneno kama hayo kusema wanatujali na wengi wao hawakutoa? Rejea tena Lancaster (2007) kubaini hili. Nadhani hofu hii ndiyo iliyopo moyoni na akilini mwa Mheshimiwa Spika Job Ndugai.
Riddell (2007) alipata kubainisha kuwa mikopo au misaada siku zote huwa imefungamanishwa na kamba fulani kama mtego (strings attached) au wengine huita diplomasia ya mtego wa deni kama ambavyo Cheryl Payer (1974) alipoichambua IMF dhidi ya madeni ya nchi zinazoendelea katika makala yake ‘The Debt Trap: The International Monetary Fund and the Third World.’
Labda hili la ‘mikopo kuwa na kamba fulani’ ndilo linalompa hofu Mheshimiwa Spika Job Ndugai akiamini kuwa kama tutaendelea kukopa ipo siku Tanzania itapigwa mnada kama ifanyikavyo minada ya nguo na vitu mbalimbali kwenye ule Mnada maarufu wa Dodoma ambao wengi wetu huenda kula nyama za ng’ombe na mbuzi.
Lakini labda Mheshimiwa Spika amesahau kuwa katika Mikopo kuna kitu tunaita DSR ama Ustahimilivu wa Deni ambao Gavana wa Benki Kuu Profesa Florens Luoga aligusia pindi alipofanya mahojiano Clouds Tv katika kipindi cha Power Breakfast Jumatano tarehe 29 Desemba, 2021. Lakini pia kama nchi hatuwezi kufungua kamba hizo ama kuruka vihunzi hivyo tukizingatia kuwa dunia hii tunategemeana? Rejea dhana ya interdependence aliyoeleza McGowan na wenzake (2013).
Kimsingi, dhana hiyo ya kuwepo kwa ‘mtego wa kamba’ ndiyo ambayo inayopelekea wanazuoni kukinzana juu ya madhumuni ya mikopo au misaada katika mahusiano ya kimataifa.
Hili linajidhihirisha wazi kutoka katika hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan siku alipozindua ‘Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete tarehe 10 Oktoba, 2021 ambapo alisema, “Kuna kaujanja kidogo tulifanya.”
Naamini ‘ujanja’ huo aliosema Mheshimiwa Rais ulifanyika kukwepa mitego au kamba hizo anazohofia Mheshimiwa Spika Job Ndugai.
Huenda IMF walitaka pesa hizo tuzitumie katika namna nyingine kabisa ambayo haizingatii mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano. Rejea ibara ya 9 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Hili linatupa picha kuwa ujanja unatakiwa ili kutoingia katika kile ambacho wanazuoni wengi wanakiona kama ‘mtego’ ambao labda unaweza kusababisha nchi kupigwa mnada.
Lakini je kuna uwezekano huo wa nchi kupigwa mnada kifalsafa au kuna malengo mengine nyuma ya mikopo na misaada inayotolewa?
Kwa nadharia za kifalsafa, wapo wanazuoni wanaotafsiri misaada katika mtazamo wa mrengo wa kulia (Realism).
Wao wanaona kuwa kutokana na kwamba nchi zinafanya mambo yao katika mazingira ambayo hakuna mamlaka/serikali kuu iliyo juu yao inayoziongoza ambapo nguvu ya Dola, usalama na uhai wa Dola ni vitu vinavyochukua nafasi ya kwanza hivyo wanaona kuwa misaada au mikopo ni nyenzo ya msingi kwa diplomasia ya kichwa ngumu (hardheaded diplomacy).
Madhumuni ya misaada au mikopo kwa mtazamo wao ni kwamba ni nyenzo ya kuongeza usalama wa nchi inayotoa misaada kwa kupunguza vishawishi (temptations) wa ukomunisti au ugaidi.
George Liska miongoni mwa wanamrengo wa kulia (realist) wa mwanzo yeye alitoa hoja kuwa misaada ilikuwa nyenzo ya kuhanikiza nguvu ya taifa (national power) husika na usalama wake.
Liska hakutofautiana sana na Hans Morgenthau moja wa mababa wa mrengo wa Kulia (Realism) ambaye alisema; ‘Misaada ya kigeni leo na itabaki kwa muda fulani kuwa nyenzo ya nguvu ya kisiasa (political power)’
Hivyo basi, Marekani au taasisi zake za Bretton Woods (IMF na Benki ya Dunia) zinapotoa mikopo au misaada zinalenga kujilinda kwa kuziongezea uwezo wa kujilinda nchi ambazo zipo karibu na vitisho vya usalama kwa Marekani au Washirika wake.
Miaka ya 1970 mpaka 1980 kundi la wanazuoni lilifanya utafiti juu madhumuni ya misaada au mikopo kwa kutazama uhusiano uliopo kati ya kiasi gani cha misaada iliyokuwa ikitolewa kwa nchi fulani na tabia ya nchi hiyo ili kuainisha madhumuni ya misaada. Rejea Lancaster (2007:3).
Hitimisho la tafiti hizo uliotoa mchango kwa ubashiri wa wale wa mrengo wa kulia kwa misaada inayotolewa na nchi moja kwa nchi nyingine kuwa kimsingi inaongozwa na maslahi binafsi ya nchi au taasisi hizo zinazotoa misaada au mikopo.
Kwa mfano Marekani imekuwa ikishawishiwa na hisia za Vita Baridi, Ufaransa imekuwa ikishawishiwa na lengo lake la kuimarisha uga wa ushawishi wake Afrika baada ya kuisha kwa ukoloni.
Ikumbukwe kuwa hata aliyekuwa Mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani Arikana Dkt. Chihombori Quoro aliwahi kuhoji (ingawa hakuwa sahihi kutokana na hadhi ya ubalozi aliyokuwa nayo) mkataba wa Ufaransa dhidi ya nchi za Afrika Magharibi jambo lililopelekea kufukuzwa kazi.
Kwa wanazuoni wa mrengo wa kati wa Marx (Marxist)na wenzao wa dhana yao ya utegemezi (Dependency) na kupinga utandawazi (anti-globalization) wanaamini kuwa mikopo au misaada lengo lake ni kama nyenzo inayotumiwa na mataifa yaliyokamata siasa za dunia kuyadhibiti na kuyanyonya mataifa yanayoendelea. Wao wanajaribu kuthibitisha hili kwa kutoa mifano kadhaa ya misaada ya kigeni inayofungamanishwa na uuzaji wa bidhaa na huduma kutokana nchi wahisani au kupata mwanya wa kununua malighafi kutokana katika nchi masikini/zinazoendelea kwa ajili ya viwanda vya mataifa hayo yaliyoendelea (Lancaster, 2007).
Lancaster aliendelea kuainisha kuwa, kwa upande wa wanazuoni wa mrengo wa kushoto (Liberal internationalists na liberal traditional) katika mahusiano ya kimataifa wanaona misaada kama chombo au kiakisi cha tabia za nchi kushirikiana na kueleza matatizo yatokanayo na kutegemeana na utandawazi kama vile maradhi na uchafuzi wa mazingira.
Lakini kwa upande wa nadharia ya wajenzi (Constructivism) ambayo inatokana na falsafa ya uzoefu na maarifa (Epistemology) wao wanaamini kuwa utaratibu (norm) uliopo katika uzoefu baina ya nchi tajiri na nchi masikini ni kwamba nchi tajiri zinapaswa kuzisaidia nchi masikini katika kuboresha maisha ya watu wa nchi hizo masikini. Wanaotoa mfano wa viongozi wakuu wa nchi zilizoendelea kiviwanda (G8) walipokutana nchini Scotland mwezi Juni, 2005 na kuweka wito wa pamoja wa kufanya ‘Umasikini kuwa Historia’ ambapo waliahidi kuongeza kiwango cha misaada kufikia malengo ya milenia (MDGs) ikiwemo kupunguza umasikini kufikia mwaka 2015.
Mwaka huo wa 2005 jumla ya kiwango cha misaada kilichotolewa na nchi tajiri duniani kilifikia Dola za Marekani Bilioni 100 kwa mara ya kwanza ikikaribia kuzidi kiwango cha Dola Bilioni 52 za Marekani kilichotolewa mwaka 2001 (Riddell, 2007).
David Lumsdane amesisitiza suala hili la norm ndilo linalofanya nchi zinazoendelea kutoa mikopo na misaada kwa nchi zinazoendelea.
Licha ya hivyo bado kuna changamoto sana katika utoaji wa misaada hii rasmi kuwa mara nyingi huwa haitekelezwi kama ambavyo nchi hizo zimeahidi.
Tukitazama nadharia hizo zote kwa pamoja tunaona kuwa zinakosa kiunganishi (element) kimoja pindi zinapojadili mikopo au misaada.
Kiungo hiki ni athari za mikopo au misaada kwenye siasa za ndani za nchi inayotoa au inayopokea mikopo au misaada kama tunavyoona hali hii hapa Tanzania kwa sasa.
Kwa mfano, Brecher na Abbas (1972) walieleza kuwa misaada au mikopo ni nyenzo madhubuti inayotumiwa na nchi au taasisi wahisani kuathiri Sera za kiuchumi za serikali za nchi zinaozopokea misaada au mikopo hiyo.
Misaada na mikopo kama ilivyo kwa diplomasia, propaganda, uchochezi na utumiaji wa jeshi ni chombo cha umahili wa dola katika kusimamia masuala mbalimbali ya serikali, umahiri ambao kwa lugha ya Kingereza huitwa Statecraft.
Sera ya misaada na mikopo imekuwa sehemu ya diplomasia na hatimaye ‘nyenzo ya kisasa ya udhibiti’ dhidi ya sera na mwenendo wa nchi nyingine (Weissman, 1975:11) na walau kuleta ushawishi (McGillivray na White, 1993:2) dhidi ya nchi husika katika maamuzi yake ya kisera. Nadhani hoja hii ndiyo inayomtia hofu Mheshimiwa Spika Ndugai.
Kwa mtazamo huu, misaada ya kigeni inaonekana kama nyenzo pekee ya juu ya kukuza maendeleo ya nchi za dunia ya tatu/zinazoendelea (Baldwin, 1985:325) huku ikiwa na madhumuni ya kuleta na kuongeza ushawishi kwa nchi zinazopokea misaada au mikopo na hivyo kuathiri Sera za nchi hizo dhidi ya wananchi wake na hivyo kuonekana kama nyenzo ya kuvuruga uhusiano baina ya wananchi na serikali zao uliopo kwa mujibu wa Katiba. Rejea ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Hii ndiyo sababu Hans Morgenthau alisema:
“Foreign aid is among the real innovations which the modern age has introduced into the practice of foreign policy.” Morgenthau anajaribu kuonesha namna mikopo na misaada kama ubunifu wa ‘kuwagombanisha’ wananchi na serikali zao ama kufikia malengo ya nchi zinazotoa mikopo au misaada hiyo kwa kufanikiwa kubadili malengo ya nchi zinazopokea mikopo au misaada.
Licha ya ukweli huo, tujiulize, ni lini malengo yetu yalibadilika? Hili nalo ni swali la msingi kujihoji!
Kimsingi, hoja hii imewahi kujibiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika andiko lake Argue Don’t Shout la mwaka 1969 aliposema:
“The goals we pursue do not change and are not matters on which we can compromise. What will change from time to time, and what is subject to compromise and negotiation, is the tactics we use in pursuing the objectives.”
Mwalimu Nyerere amesisitiza kuwa malengo yetu kamwe hayabadiliki na hayawezi kujadiliwa, kinachobadilika kulingana na nyakati ni mbinu tunazotumia kuyaendea malengo hayo.
Muongozo huu ndiyo uliokuwa ukitumiwa na viongozi wote waliopita, je Mheshimiwa Rais Samia ameacha kuutumia au amebadili mbinu kama alivyoelekeza Mwalimu Nyerere? Tukiangalia kwa mfano, uhusiano wa Tanzania na Kenya au hili la IMF tunaona kuwa ni wazi amebadili mbinu kama alivyobainisha kuwa kuna kaujanja Serikali imetumia ili wasibanwe na masharti yaliyomo kwenye zile trilioni 1.3 za IMF.
Licha ya umakini huo wa Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan lakini ni ukweli kuwa misaada na mikopo ni ubunifu wa hali ya juu wa mtego wa madeni ambao nchi na taasisi za kigeni zinatumia ambao nchi za Afrika zinapaswa kuwa makini nao.
JE TUNAWEZA KUACHA KUKOPA?
Mwalimu Nyerere katika Argue Don’t Shout aliweka bayana aliposema;
“There is no getting away from this. It is for this reason that Tanzania must always try to understand the policy objectives of other countries.”
Mwalimu Nyerere anabainisha wazi kuwa hatuwezi kujiondoa kwenye ukweli kuwa dunia hii tunategemeana (kama alivyobainisha McGowan na wenzake, 2013) na hivyo kuna wakati tutahitajika kukopa.
Kubwa ambalo ni la muhimu ni kutambua malengo yetu kama nchi na vilevile kutambua malengo ya wale wanaotukopesha sambamba na mbinu wanazotumia ili kufikia malengo yao.
Hapa sasa tujiulize, je hatujui lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025? Au hatujui malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano 2021/22-2025/26?
Hivyo basi, suala si kupokea mikopo au misaada, bali hoja kuu ni misaada au mikopo hiyo inatumika vipi?
Hili lilibainishwa pia na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Florens Luoga alipofanya mahojiano na kituo cha luninga cha Clouds katika kipindi cha Power Breakfast Jumatano tarehe 29 Desemba, 2021 aliposema:
“Unapokopa mkopo hukopi kwa ajili ya kula unakopa kwa ajili ya kufanya project ambazo zitaendelea kuzalisha na kwa sababu unaendelea kuzalisha uhimilivu wako wa deni unaendelea kuwa mzuri sio kwamba deni linapanda.”
Nafikiri labda kuna haja ya kufafanua nini maana ya deni kuwa himilivu (DSR) ili kuongeza uelewa wa watu wengi.
Lakini kipekee kabisa, hakuna nchi inayotumia fedha zake za ndani katika miradi mikubwa kama zikiwepo basi ni nchi chache sana!
Kwa kukazia hili Profesa Luoga alisisitiza:
“Ukitumia pesa za ndani peke yake utapandisha kodi, utawafanya wananchi wachangie kwa njia nyingine ambayo ni gharama na itachukua muda mrefu. Badala ya kutengeneza mradi kwa miaka 3/4 utautekeleza kwa miaka 20 kwa sababu unategemea uchukue pesa za ndani.”
Kwa mantiki hiyo basi mikopo ni lazima itumike katika miradi ambayo itachochea ukuaji wa uchumi kama ambavyo Serikali inafanya kwa sasa kwa kuelekeza fedha za mkopo kwenye ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambayo pindi ikikamilika itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Labda katika hali nyingine nadhani wale wanaohoji kuhusu mradi huu ambao Serikali imesisitiza itaujenga kwa mkopo wangeanza kuhoji sababu za Serikali kujitoa kwenye mkopo au msaada ambao China ilipanga kuipatia Tanzania katika ujenzi wa mtandao huu huu wa reli na badala yake tukawapa Waturuki huenda labda wangekuwa na mantiki juu ya kuongezeka kwa deni, nasema labda wangekuwa na mantiki!!
Jambo lingine muhimu katika fedha, mikopo na matumizi ya serikali yoyote ile duniani ni uwazi.
Nafikiri tunapaswa pia kushukuru kwa uwazi ambao Serikali inauonesha kwa sababu ripoti nyingi za UNDP, Benki ya Dunia na zile za OECD zinabainisha wazi kuwa tatizo kuu la utawala barani Afrika ni kukosekana kwa uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria mambo ambayo husababisha kukithiri kwa rushwa na ubadhirifu kama ule tulioshuhudia nchini Angola. Rejea Schoeberlein (2020).
Nadhani, kubwa na la muhimu ni kuisisitiza Serikali izidishe uwazi kwani kama alivyosema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan fedha hizi tutakaolipa ni sisi wananchi hivyo ni lazima uwepo uwazi katika matumizi yake ikiwezekana taarifa zibandikwe kila kata au mtaa wananchi wajue fedha za mikopo au miradi kama zile trilioni 1.3 za IMF zinatumikaje katika Kata, Mtaa au Kijiji husika hapo tutakuwa na jamii yenye uelewa wa pamoja.
Wenu:
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).
Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp)
Marejeo:
Baldwin D.A (1985) Economic Statecraft. Princeton University Press New Jersey
Brecher. I and Abbas S.A (1972) Foreign Aid and Industrial Development in Pakistan. Cambridge University Press. Cambridge
Lancaster C (2007) Foreign Aid: Diplomacy, Development, Domestic Politics. The University of Chicago Press. Chicago
McGowan, P.J, Cornelissen. S, Nel, P (2013) eds. Power, Wealth and Global Equity: An International Relations Textbook for Africa. UCT Press, Cape Town
Nyerere, J.K (1969) Argue Don’t Shout: An Official Guide on Foreign Policy by the President. Government Print
Payer C (1974) The Debt Trap: The International Monetary Fund and the Third World. Monthly Review Press
Picard L.A, Groelsema R and Terry F.B (2008) Foreign Aid and Foreign Policy: Lessons from the Next Half Century M.E Sharpe Inc. New York
Resnick D. and Van De Welle N. (2013) Democratic Trajectories in Africa: Unraveling the Impact of Foreign Aid. Oxford University Press Oxford
Riddell R.C (2007) Does Foreign Aid Really Work Oxford University Press Oxford
Schoeberlein, J (2020) National Strategies for Advancing Good Governance in Africa Transparency International Press
Wittkopf E.R, Jones C.M and Kegley Jr, C.W (2008, 2003) 7th Edition American Foreign Policy: Patterns and Process.Thomson Wadsworth Belmont








