
Madaraka Nyerere

@MadarakaN
Maana ya “trolls”
Kwenye mitandao ya jamii kuna watu wenye tabia mbovu ambao kwa Kiingereza wanaitwa, “trolls”. Ni jina la Kiingereza la viumbe wa kufirikia wa hadithi za watoto ambao wana maumbile yasiyopendeza na tabia zisizopendeza. Kwa kuwa mitandao ya kijamii ni suala geni katika historia ya binadamu, nadhani bado hatujapata neno le Kiswahili kuwatambulisha hawa “trolls” wa kisasa.
Hata hivyo tabia yao unaweza kuwa unaifahamu. Kazi yao ni kutumia lugha chafu na zisizokuwa na staha kwenye mitandao kwa madhumuni ya kuudhi, kukera, na zaidi, wakiamini wanajijengea umaarufu ambao hauna maana hata kidogo.
Kama unatumia mitandao ya kijamii na hutumii lugha chafu, hiyo siyo kinga dhidi yao. Wao watakutukana kujibu hoja zako za kiungwana. Na katika kujibu hoja au maoni ya watu wengine wataburuza ndani watu ambao hata hawakutajwa kwenye hoja ya msingi.
Kimtazamo, na kwa kuzingatia lugha wanayotumia, unaweza kusema kuwa ni watu jasiri. Mimi nadhani ni waoga ambao wanatumia mitandao ya kijamii kuficha woga wao. Inawezekana hawa ni wale watu ambao ukiwakuta majumbani kwenye mazingira ya familia ndiyo wale wasioweza kuongea mbele ya wengine na wanaaminika kuwa wapole wa familia. Mitandao inawapa taswira ya kudhaniwa kuwa Simba wa Serengeti wakati kiuhalisia ni nyau wa vichochoro vya mjini wasiokuwa hata na makucha.
Nawafananisha na baadhi ya watoto wa darasa la kwanza ambao wameanza kujifunza kuandika na kila wakikuta gari lenye vumbi kwenye madirisha wanaandika “nioshe” wakifurahia uvumbuzi wao wa uwezo wa kuandika. Baada ya muda wanahamia kwenye kuta na kuanza kuandika matusi, wakifahamu kuwa si rahisi wapita njia kubaini ni nani aliyeandika. Baadhi ya hawa wa kwenye mitandao hutumia majina bandia.
Kama ilivyo kwa hawa watoto wanaojifunza kuandika, mitandao ya jamii kwa sasa ndiyo imekuwa vioo vyenye vumbi na kuta za kuandika matusi. Isipokuwa wanaoandika kwenye mitandao siyo tena watoto tu bali ni pamoja na watu wazima.
Wapo “trolls” ambao wamejikita pia kwenye kuporomosha lugha za matusi dhidi ya wanaowadhani kuwa na misimamo kinzani ya kisiasa na ya kwao.
Kwa ujumla kuwepo kwa mawazo tofauti ndiyo msingi wa ubinadamu; hatuwezi kamwe kufanana mawazo. Lakini mawazo tofauti yanaweza kuwasilishwa bila kutumia lugha chafu na iliyokosa staha.
Twitter: @MadarakaN
Troll








