

VATICAN
Ibada hii ya Misa Takatifu iliandaliwa na Umoja wa Watanzania Wakatoliki Italia pamoja na mambo mengine, ilikuwa ni kwa ajili ya kuombea Amani nchini Tanzania na kuhudhuriwa na Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia Askofu mkuu Protase Rugambwa amekazia umuhimu wa kujikita katika: wema, maisha adili na matakatifu, toba na wongofu wa ndani.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Dominika tarehe 27 Februari 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani ndani na nje ya Tanzania. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya “Corpo e Sangue Di Cristo” Jimbo kuu la Roma. Watanzania wamemwomba Mwenyezi Mungu kuwaangalia watanzania wanaohesabika kati ya Mataifa ya dunia, awajalie kuishi maisha mema kadiri inavyowastahili wana wa Mungu. Awaangaze viongozi wa Tanzania watu sheria zitakazowafaidia kwa mambo mema hapa duniani, zilingane na Sheria za Mungu aliyeuwaumba kwa ajili yake. Awakirimie watu wote paji la imani kwa kutambua uwepo wake endelevu, awaimarishe ili waweze kupambana na maovu yanayoweza kuwafikia kutoka ndani au nje ya nchi. Mwenyezi Mungu awakirimie hekima ya kutafuta ukweli katika mambo yote, na kuishi kwa uaminifu katika Amri za Mungu.