
WU® Media PRODUCTION
Na Abbas Mwalimu (0719258484).
Ijumaa tarehe 25 Machi, 2022.
Jumatano tarehe 23 Machi, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alizindua nyumba 644 za waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika uzinduzi huo Mheshimiwa Rais aliagiza na kuonya na hapa ninamnukuu;
“Nataka mtengeneze Kamati ambazo zitasimamia usafi wa nyumba hizi, kivyovyote vile sitegemei watu wapikie kuni ndani ya nyumba hizi na badala yake nategemea wapikie gesi.” Mwisho wa kunukuu.
Kauli hii ya Mheshimiwa Rais ni amri si tu kwa wakazi wa Magomeni Kota bali kwa Wizara ya Nishati na Madini.
Lakini je tatizo la utumiaji mkaa ni la wakazi wa Magomeni Kota peke yake?
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Doggart (2020), Alem na wenzake (2015), Msuya (2011), Benki ya Dunia (2010), Peter na Sander (2009) zinaonesha maeneo kama Dar es Salaam tu peke yake hutumia tani laki tano (500,000) za mkaa kwa mwaka sawa na takribani asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini.
Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ya mwaka 2019 inaonesha kuwa utafiti uliofanyika 2017/2018 kwa kaya mbalimbali unaonesha kuwa maeneo ya mjini na Dar es Salaam utumiaji wa mkaa ni asilimia zaidi ya 60 kama chanzo cha nishati.
JE TUNAFANYAJE KUEPUKA HILI?
Ni wazi kuwa kuna haja ya kutumia nishati ya gesi kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pale Magomeni Kota.
Gesi hii inaweza kuwa ile itokanayo na mafuta ghafi ya petroli yaani Liquefied Petroleum Gas (LPG) au gesi asilia yaani Liquefied Natural Gas (LNG) inayozalishwa kule Mtwara.
Kwa bahati mbaya sina taarifa ya kina juu ya uzalishwaji wa gesi asilia (LNG) na asilimia ngapi ya gesi hiyo inazalishwa na hutumika majumbani licha ya kufahamu kuwa inatumika kwenye baadhi ya maeneo kama kwenye kota za TPDC kule Mikocheni.
Hivyo basi nitatazama zaidi gesi itokanayo na uchakataji wa mafuta ghafi yaani LPG kwa mujibu wa ripoti za EWURA.
Kwa mujibu wa ripoti hizo za EWURA zinaonesha kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka 2016 makampuni yanayofanya biashara ya kuagiza LPG yaani LPG Marketing Companies (LMCs) yaliagiza jumla ya metriki tani 120,961 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na metriki tani 107,083 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 13, wakati kwa mwaka 2018 uagizwaji wa LPG ulikuwa metriki tani 142,939 na mwaka 2019 metriki tani 166,436 sawa na ongezeko la asilimia 16 ikiwa ni mchanganyiko wa gesi zote mbili Butane ambayo ni rafiki kwa mazingira ya Tanzania na Propane wakati kuanzia mwezi Julai 2019 mpaka Juni 2020 LMCs yaliagiza metriki tani 189,509 sawa na ongezeko la asilimia 30 kwa kipindi chote.
Kutokana na ripoti hizi za EWURA zinazoonesha kuwa matumizi ya gesi ya LPG kwa watanzania yanaongezeka, naamini ongezeko hilo limechangiwa pia na kuondoka kwa ile dhana ya hofu kuwa gesi inalipuka kwani tunaona hata wauza chipsi wengi siku hizi wanatumia gesi ya LPG kukaangia chipsi, kuku n.k.
Lakini je ni kwa nini bado asilimia kubwa ya watanzania hawatumii gesi kupikia?
Na ni kwa namna gani Serikali itatengeneza mazingira ya kufanya utumiaji wa gesi uwe mkubwa?
Haya ndiyo maswali ambayo yanapaswa yatufikirishe na kutaka kubaini majawabu halisi na njia sahihi za kutatua tatizo hili la utumiaji wa mkaa kupikia.
Binafsi, kutokana na uzoefu niliopata katika kampuni za kuagiza na kuuza gesi nchini (LMCs) naona tatizo la utumiaji wa gesi ya LPG linatokana na gharama ya gesi hiyo kuwa kubwa ukilinganisha na vipato vya watanzania wengi
Tukumbuke hata Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango alibainisha wazi siku alipothibitishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Bungeni Dodoma alipoeleza kuwa licha ya kwamba Tanzania kama nchi tumeingia kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha chini kati lakini zaidi ya watanzania milioni 14 wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Hii inaonesha wazi namna asilimia kubwa ya Watanzania tusivyo na vipato vya kutosha. Je tutaweza kumudu gharama za gesi ambazo zinapanda kila kuitwapo leo?
Ni wazi kuwa kwa takwimu hizi tatizo si wananchi kupenda kutumia mkaa bali wengi hawana uwezo wa kutumia gesi kutokana na kutokuwa vipato vya kununua gesi hiyo na viambata vyake (accessories) kwa mara moja.
Hili ndiyo tatizo la msingi ambalo binafsi naamini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hakutaka kuliainisha ili wasaidizi wake wapate kusugua vichwa juu ya namna ambayo watawafanya wakazi wa Magomeni Kota na Tanzania kwa ujumla watumie gesi badala ya mkaa ambao kwa kweli unachafua sana mazingira.
Katika hili naomba nitoe uzoefu wangu kama mtu aliyewahi kuwa Afisa Mtendaji wa Mauzo na Masoko (Sales and Marketing Executive) wa miongoni mwa kampuni kubwa za uagizaji mafuta na gesi ya LPG nchini na pia Afisa Mikopo wa benki kwa nyakati tofauti.
Kwa maoni yangu, tatizo lililopo kwenye gesi (LPG) linasababishwa na ukubwa wa bei ya gesi kwa mtungi ama cylinder ambapo mtungi wa kilo 6 hubadilishwa kati ya shilingi za Tanzania 21,000 mpaka 24,000 huku kununua seti nzima (complete set) huwa kati ya shilingi elfu 55 mpaka elfu 60.
Kwa upande wa mtungi wa kilo 15 bei ya kubadilisha huwa kati ya shilingi elfu 50 mpaka elfu 53 wakati kwa seti nzima huwa kati ya shilingi elfu 80 mpaka elfu 93.
Kwa upande wa mitungi ya kilo 38 bei ya kubadilisha ni kati ya shilingi 115,000 mpaka shilingi 120,000 wakati seti nzima ni kati ya shilingi 225,000 mpaka shilingi 240,000 ambapo mtu akinunua na jiko la sahani mbili na vifaa vyake hufikia kiasi cha shilingi laki 4 (Tshs 400,000/=).
Kiwango hiki cha bei za gesi kinatokana na uchache wa watumiaji wa gesi nchini.
Kwa hali hiyo ya uchache wa watumiaji, makampuni ya gesi hulazimika kuingiza gharama za uendeshaji (operational expenses) katika bei ya kununulia gesi na hivyo kufanya bei ya kununua mtungi uliojazwa gesi kuwa kubwa na hivyo kuwafanya watanzania washindwe kutumia gesi na kuamua kutumia mkaa kutokana na ukubwa wa bei ya gesi.
Ni wazi kuwa kwa bei hizo nilizoonesha hapo juu watanzania wengi hawawezi kumudu kununua gesi na viambata vyake kwa mara moja.
Kwa kujua ukweli huu wa changamoto ya kipato cha kununua seti nzima ya gesi kwa mara moja, makampuni mengi ya gesi nchini huwa na utaratibu wa kuwakopesha wafanyakazi wao seti zima jambo ambalo huwapunguzia gharama za maisha kwa kutolipa pesa yote kwa mkupuo.
Sasa tujiulize, kama makampuni haya ya gesi yanaliona tatizo hili, je serikali hailioni?
Na je serikali haiwezi kuandaa utaratibu kwa watanzania kuweza kukopeshwa gesi na vifaa vyake (accessories) ili kuwapunguzia gharama ya maisha kwa kulipa kidogo kidogo kama yafanyavyo makampuni hayo ya gesi nchini?
Naamini hilo linawezekana! Hivyo kwa maoni yangu mkakati wa serikali katika hili aliloagiza Mheshimiwa Rais na hasa kwa Wizara ya Nishati na Madini inafaa ujielekeze katika kuyafanya makampuni ya gesi kuwa na wateja wengi (huge customer base) jambo ambalo litapelekea bei ya gesi kupungua kutokana na makampuni ya gesi kuweza kuagiza gesi kwa wingi na kuuza kwa wateja wengi (economies of scale).
Wachumi wanafahamu kwa mapana kanuni inayoeleza kuwa bidhaa ikipatikana kwa wingi (supply) bei yake (price) hushuka na hivyo upatikanaji wake huwa rahisi kutokana na kushuka kwa gharama za manunuzi ya gesi hiyi kutoka nje ya nchi.
Ninaamini Serikali ikijenga mazingira wezeshi kwa makampuni ya gesi kuweza kuuza gesi kwa wingi itasaidia kuongeza ushindani kwa makampuni hayo tofauti na takwimu za sasa karibuni ambapo kati ya metriki tani 166,436 zinazoagizwa nyingine husafirishwa Rwanda, Kenya na Comoro kutokana na kukosekana kwa uhitaji mkubwa katika soko la ndani.
JE SERIKALI ITASAIDIAJE KUONGEZA WATUMIAJI WA GESI NA KUONDOA UTUMIAJI WA MKAA?
Kuna namna kama tatu za kusaidia kuongeza wingi wa wateja/watumiaji wa gesi ya LPG (customer base) na kupunguza utumiaji wa mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia.
Mosi, Serikali inaweza kuyapa ruzuku makampuni ya gesi ili yenyewe yaweze kuuza gesi ya LPG kwa bei ya chini, hii ni kutokana na kwamba makampuni ya gesi huingiza gharama za uendeshaji (operational costs) katika bei ya gesi hivyo kufanya bei kuwa kubwa.
Ninaamini kwa kuyapa ruzuku makampuni hayo (LMCs) kutayafanya yaache upigaji wa hesabu za uendeshaji kampuni katika bei ya gesi na hivyo kuwafanya watanzania kumudu kununua gesi ya LPG.
Pili, serikali kwa kushirikiana na mabenki nchini inaweza kuandaa utaratibu kwa watanzania kukopeshwa gesi kupitia ofisi za Kata kwa watu kusajiliwa na kutambuliwa wanakoishi kupitia wenyeviti wao wa serikali za mitaa na wajumbe. Kwa bahati nzuri sasa tuna anwani za makazi hivyo ni rahisi kuwafikia.
Watanzania hawa watakuwa wakizilipa kampuni walizokopa gesi hiyo kidogo kidogo kwa kupitia mfumo wa kulipia benki.
Tatu, serikali inaweza kuanza na utafiti mdogo kwa mkoa wa Dar es Salaam ambao ndiyo unaongoza kwa utumiaji wa mkaa (tani laki 5 kwa mwaka) kwa kubaini kaya zote ambazo haziwezi kumudu kulipia gesi hiyo kwa mara moja na kuandaa mpango wa kuzikopesha ambapo kila kaya hizo zitakapoenda kujaza gesi zitakuwa zikiongezea kiasi kidogo cha malipo walau shilingi elfu moja katika bei ya manunuzi ili kulipia deni la kukopeshwa.
Ninaamini kwa kufanya hivyo makampuni ya gesi yataongeza wateja na hivyo kupunguza kugombea wateja wachache waliopo kutokana na wengi kushindwa kumudu bei ya gesi hiyo.
Hivyo ninaamini bei ya gesi itashuka sana kupitia ongezeko la wateja huku wananchi wakimudu kununua gesi kutokana na kupatikana kwa wingi na kwa bei nafuu tofauti na ilivyo sasa.
Kwa kufanya hivyo pia ninaamini kwa asilimia mia moja kuwa mazingira yataweza kuhifadhiwa kutokana na kukosekana kwa soko la mkaa kutakakosababishwa na kushuka kwa bei ya gesi hivyo kulinda mfumo wa ikolojia na maisha ya viumbe hai wote tukiwemo sisi wanadamu na kupelekea uchumi wetu kukua.
Hivyo basi kwa maoni yangu, tatizo la wananchi wengi kushindwa kununua mitungi ya gesi hasa LPG na viambata vyake (accessories) na kukimbilia mkaa linatokana na changamoto ya kipato chao kuwa duni ukilinganisha na bei ya gesi. Kwa msingi huo serikali inaweza kuwasaidia wananchi kwa njia hizo tatu.
Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).
+255 719 258 484








