0 0
Read Time:5 Minute, 19 Second

WU® Media PRODUCTION LIMITED

WATANZANIA JIANDAENI KUPOKEA WATALII NA FURSA TELE.

UCHAMBUZI WA FAIDA 11

Anaaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu

Awali ya yote napenda Niwasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Kazi Iendelee.

Ziara ya Rais Samia Marekani ni kama imenikumbusha misemo kadha ya wahenga inenayo, safari moja huanzisha nyingine au mkaa bure si sawa na mtembea bure au mguu ulotoka mtume kauombea na mgagaa na upwa hali wali mkavu

Hivi ndivyo naweza kuielezea safari ya Rais Samia Marekani na uzinduzi wa makala ya filamu iliyotukuka maarufu kama “Royal Tour” na faida zake kwa nchi yetu ya Tanzania.

Kama tunavyofahamu Mheshimiwa Rais jana tarehe 28/4/2022 alirejea nchini na kuzindua filamu hiyo huko jijini Arusha.

Mheshimiwa Rais Samia anasema: shabaha kubwa ya ziara yake huko nchini Marekani ilikuwa ni kuitangaza kwa dunia na kuujulisha ulimwengu vivutio vilivyopo Tanzania

Mheshimiwa Rais alidhihirisha kuwa ni kweli Tanzania ilikuwa haijulikani vilivyo duniani. Ambapo alifanya uzinduzi wa filamu ya Royal Tour katika miji 2 ya Marekani ambayo ni New York tarehe 8 na Los Angeles tarehe 21. Mheshimiwa Rais amesisitiza tutarajie matunda lufufu na tujitayarishe kupokea wageni kwa kuepusha kutukuwapa usumbufu.

Filamu hiyo ameeleza kuwa itazinduliwa tena Zanzibar na Dar es Salaam na baadaye itarushwa katika vituo anuwai vya runinga vya Tanzania.

Rais Samia ametoa shukrani kwa wote waliofanikisha kukamilika kwa filamu hiyo ikiwamo wafanyabiashara na wadau wengine wa utalii ambao walichangia fedha na michango mbalimbali katika kuandaa filamu hii.

Ufuatao ni uchambuzi wa faida lufufu 11;

Mosi, kuongeza idadi ya watalii nchini Mheshimiwa Rais meeleza kuwa idadi ya watalii itaongezeka zaidi kufuatia ziara hii adhimu kwa Taifa. Mheshimiwa Rais Samia amesema hatahivyo idadi ya watalii kimataifa imeongezeka kwa asilimia 48.6. Sawa na idadi ya watalii laki 2 hadi laki 9 mia 6 na 92. Kifedha ni kutoka dola milioni 714 mwaka 2020 hadi dola milioni 1224 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76. Kwa hatua hii Mheshimiwa Samia amewataka sekta ya utalii wajipange vyema kupokea wageni lufufu kama si sifufu.

Pili, kuimarisha uhusiano na Marekani Samia anaeleza kuwa katika ziara hiyo alikutana na makamu wa Rais wa Marekani Bi.Kamala Harris. Katika mkutano wao walizungumza mengi ya kuimarisha uhusiano wao na nchi yetu ya Tanzania. Kwa sasa amesema hatua kubwa waliyokubaliana na kwenda mbele zaidi sasa na kuwa na uhusiano uwekezaji na biashara kwa hakika hii hatua kubwa sana kwa nchi yetu ukiachilia uhusiano uliozoeleka wa kuombana na kusaidiana ambao Mheshimiwa Samia amesema utaendelea.

Tatu, Udugu wa Jiji la Galaxy na Majiji ya Tanzania katika hatua nyingine walifanya mazungumzo na meya wa jiji la Galaxy huko Marekani juu ya kuwa na uhusiano na majiji ya Tanzania. Ambapo kuna uwezekano mkubwa katika uhusiano au udugu huo kukawa na safari za ndege kuleta watalii kutoka jiji hilo hadi Tanzania moja kwa moja. Kwa kweli huu ni mpango mzuri kwa nchi yetu.

Nne, vituo 200 vya afya kujengwa Mheshimiwa Samia ameeleza kuwa katika ziara hiyo walitembelea taasisi ya utafiti wa mbu na wadudu mbalimbali ya S Johnsons. Taasisi hiyo hushirikiana kwa karibu na taasisi yetu ya Ifakara, NIMRI na kituo cha mambo ya wadudu cha Tanga. Kwa hivyo basi, wamefikia makubaliano kuwa taasisi hiyo itasaidia kuleta vifaa zaidi vya kisasa katika taasisi hizo na kujenga vituo vya afya 200 kwenye mikoa 5 ambayo inasumbuliwa sana na Malaria. Mikoa hiyo ni Ruvuma, Katavi, Geita, Kagera na Kigoma kwa hakika mgagaa na upwa hali wali mkavu. Hizi ndio faida zaidi za ziara hii.

Tano, mikataba yenye thamani ya Trilioni 11.7 imesainiwa Mheshimiwa Rais Samia amedadavua kuwa Wafanyabiashara wa Marekani hasa katika jiji la New York na Galaxy wamesaini mikataba mbalimbali ya biashara na Tanzania. Mheshimiwa Samia ameelekeza kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kwetu kwa watendaji wanaohusika na sekta hizo kujipanga vizuri na kuepusha usumbufu kwa wawekezaji watakaokuja.

Sita, Kazi zaidi ya laki 3 kuja Tanzania Mheshimiwa Samia ameendelea kusema kuwa kazi au ajira zaidi ya laki 3 na ushei zitakuja Tanzania ikiwa mikataba na makubaliano yote yatakwenda kama waliyokubaliana. Alichosisitiza ni kujitahidi kuweka mazingira mazuri kwa wageni hao.

Saba, Fedha kama zile za Uviko kumwagwa tena Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais Samia alikutana na mashirika ya fedha ya kimataifa. Mashirika hayo ni Benki ya Dunia na Shirika la fedha la Kimataifa IMF. Ambapo amesema fedha nyingine kama zile za UVIKO 19 zinakuja. Ama kwa hakika haya ni mafanikio makubwa sana katika ziara hii ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan. Rais ambaye ana uzalendo wa pekee hasa kwa kile kitendo alichoamua cha kuwa mhusika mkuu wa filamu ya kuitangaza nchi yetu. Huu ni uzalendo ulofurutu ada.

Rais wa nchi pamoja na uwingi wa majukumu aliyonayo bado akafanya jambo hili kwa hakika Samia ni shujaa, jasiri na Shupavu. Kongole sana Rais wetu.

Kwa ujumla tunasema kuzinduliwa kwa filamu hii mbali ya haya aliyoyabinisha Mheshimiwa Rais katika sekta ya utalii pia, itachochea zaidi faida nyingine lufufu hasa katika sekta ya utamaduni, sanaa na michezo kama zifuatazo:-

Nane, kutangaza historia na kumbukumbu ya taifa letu hususan mambo ya kale na jinsi maisha ya Ukoloni na hali iliyopo sasa. Hii itasaidia kuonesha hatua iliyopigwa na nchi kiuchumi na kimaendeleo

Tisa, Taifa kujitangaza kwa asili yake hususani katika matumizi ya lugha na mavazi Hili litakuja hasa aidha ukizingatia lugha ya Kiswahili kwa sasa imetamalaki Duniani kote. Hivyo ongezeko la watu wa mataifa mbalimbali kujifunza lugha hii itaongezeka zaidi duniani.

Kumi, Ushawishi katika masuala ya sanaa na michezo FIlamu hii bila shaka itakuwa chachu kwa vijana ambao kwao imekuwa kama ajira rasmi kuhusiana na mambo ya muziki, kucheza mpira, kufanya shughuli za kitamaduni n.k kwani wageni watakapokuja nchini watashuhudia maendeleo pia katika tasnia hizo.

Kumi na moja, Kuongezeka fursa ya kipato kwa wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa vitu mbalimbali vya asili Ongezeko la watalii na wawekezaji mbalimbali nchini utasaidia pia wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa vitu vyetu vya asili ikiwamo vinyago, makawa, mikoba, vikapu, bangili n.k kwa lengo la kuuza ndani na nje ya nchi.

Kwa mintarafu hiyo, hizi ni faida lukuki kama si lufufu za filamu hii ya “ziara iliyotukuka” au “Royal Tour” kama ilivyoasisiwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hakika hizi ni katika kauli zake zinazothibiti matendo yake. Nakumbuka katika hotuba yake kwa bunge aliahidi kuimarisha Demokrasia ya kiuchumi na sasa hiki ndicho kitokeacho.

Kongole sana Rais wetu, twakuombea afya na siha na yote haya uliyoyafanya yatimie kwa vitendo. Amina.

Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi wa Lugha
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere-Kigamboni DSM
0713400079

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
100 %
Surprise
Surprise
0 %