WU® MediaPRODUCTION LIMITED
“TUKIBORESHE KILIMO CHA BIASHARA ILI KUPAMBANA KATIKA SOKO LA DUNIA – MHE. OTHMAN“
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud othman, amehimiza Kilimo cha Kisasa kinacholenga kukuza biashara na kuiongezea Nchi pato zaidi, kupitia Soko la Utalii.
Mheshimiwa Othman ameyahimiza hayo leo alipotembelea Maonesho ya Kilimo ya Nane-Nane huko Dole, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.
Amesema kuwa Kilimo hicho ni kile kinachozingatia ujuzi wa kitaalamu katika kuongeza mazao ya biashara yatakayokidhi Soko la Utalii liliopo sasa hapa Nchini.
Akibainisha mazao hayo, Mheshimiwa Othman ametaja Kilimo cha Viungo, Mboga-mboga, Matunda halisi na Uzalishaji wa Vifaranga, kwa kuzingatia matumizi makubwa ya kemikali, ambacho ni rafiki kwa afya za watumiaji wote wakiwemo wageni wanaotembelea visiwa vya Unguja na Pemba.
“Hakikisheni mnawatumia vyema wataalamu wa kilimo cha kisasa na kuwashajihisha wakulima kukifanya kilimo kuwa cha bishara zaidi ili kukidhi soko kubwa la biashara ya utalii iliyopo Zanzibar hivi sasa”, amesisitiza Mheshimiwa Othman akitilia-mkazo wito wake kwa Wizara ya Kilimo hapa Visiwani.
Hivyo ameeleza kuwa wakulima wengi hawajashajihishwa vya kutosha juu ya kilimo chenye tija zaidi, na kwamba Wizara ina wajibu wa kuhakikisha mageuzi katika sekta hiyo, yanayohusisha pia mbinu bora na mikakati makini ya kutokomeza wadudu waharibifu.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Zanzibar, Mhe. Shamata Shaame Khamis, ameeleza kuwa dhamira ya Serikali kupitia Wizara yake hiyo ni kuhamasisha kilimo kinachozingatia uwekezaji wenye tija kinacholenga faida kwa wakulima na Taifa kwa jumla.
Amesema mwelekeo huo ni muhimu katika uzalishaji wa bidhaa za kilimo za aina mbali mbali ili kukidhi mahitaji katika masoko yote ya Zanzibar, na hasa iwapo wataalamu watawajibika ipasavyo.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Othman amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mpya wa Jeshi la Polisi Zanzibar, CP Hamad Khamis Hamad, aliyefika Ofisini kwake Migombani Jijini hapa, kwaajili ya kujitambulisha, kufuatia Uteuzi wa hivi karibuni kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, uliolenga mageuzi ndani ya Mamlaka hiyo ya Ndani ya Nchi.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Agosti 10, 2022.