
mkali@live.co.uk.
21/07/2023. London
MFANO HAI NI KENYA NA AFRIKA KUSINI
Kenya na Afrika ya Kusini ni mifano mibaya ya namna ya nchi kuwa huru.
# AFRIKA KUSINI.
.
(a) Zama za utawala wa kikaburu ulioitwa Apartheid kati ya 1984 na 1994 idadi ya raia weusi waliokuwa “forcibly removed from their lands” – yaani waliohamishwa kimabavu na makaburu ilikuwa ni laki saba (700,000).
(b) Na kati ya 1994 na 2004, yaani baada ya Apartheid kufutwa na kuletwa hicho kilichoitwa majority rule chini ya urais wa watu weusi jumla ya watu weusi waliohamishwa kimabavu (forcibly removed from their lands) ilikuwa laki tisa (900,000).
(c) Hivi sasa ni Wazungu alfu sitini tu (60,000) ndiyo wanaomilki asilimia zaidi ya 80 ya ardhi huko Afrika Kusini; na wala si Wazungu milioni na nusu waishio nchini humo.
(d) Kuna kaburu aliyewahi kusema: “Ninyi watu weusi umengalitueleza mapema kuwa huu ndiyo uhuru umliokuwa mnaupigania mbona tungeliwapeni tangu zamani.”
Kwa tafsiri huyu kaburu alikuwa anasema kwamba hakuna kilichobadilika. Au kwa maneno mengine:
Majority rule in South Africa is a mirage.
# KENYA.
(a) Asilimia 80 ya nchi ya Kenya ni jangwa; na ni asilimia 20 tu ya wananchi wa Kenya ambao ni “pastrolists” wanaishi hizi sehemu za jangwa.
Hii maana yake ni kuwa asilimia 80 ya wananchi wa Kenya wamebanana kwenye asilimia 20 ya ardhi. Wakati hizo asilimia 20 za ardhi zilihatamiwa na walowezi (Settlers) wa Kizungu na Kiaarabu (kwa zile sehemu za mwambao).
Hii ndiyo hali iliyosababisha Vita Vya kupigania uhuru vya Mau Mau na lile jeshi la Mau Mau lilikuwa linaitwa Land And Freedom Army.
(b) Serikali zote huru za Kenya zimeshindwa kutaifisha ardhi na kuleta mgao mpya na wa haki. Serikali ya kikoloni ilipiga marufuku Chama Cha Mau Mau; marufuku ambayo ilidumishwa na Serikali huru kwa miaka 40 hadi zama za Rais Mwai Kibaki. Yaani hii, mathalani, ni sawa na Frelimo ya Msumbiji, Swapo ya Namibia au MPLA ya Angola zipigwe marufuku baada ya uhuru wao. Inaleta mantiki yoyote?
(c) Zama za kikoloni, Wamasai wa Kenya walilazimishwa kusaini mkataba wa “Kimangungo” uliokabidhi ardhi yao kwa walowezi kwa miaka 99. Mkataba huo ulikwisha 2004. Wamasai walipoandamana kwenda Ikulu kudai ardhi yao; Waziri mwenye dhamana wa Serikali Huru ya Kenya aliwaambia wale waandamanaji kuwa ule Mkataba ulikuwa ni wa miaka 999 na siyo 99.
(c) Kweli ni kuwa hiyo ardhi sasa ilikuwa imehatamiwa na vizazi vya wazungu walowezi; Viongozi Waandamizi waliopo na Waastafu, pamoja na watu wanaoitwa Wawekezaji wa nje na ndani. Hivyo basi Serikali haikuwa tayari kuwarudishia Wamasai ardhi yao.
(d) Wakili wa Kimasai, Solomon Ole Sempeta, alikwenda London na kuchunguza kwenye “colonial records” na kurudi na ushahidi wa kuwa ule Mkataba ulikuwa ni miaka 99 – ndiyo kusema Waziri alisema uongo.
Kwenye “Press Conference” ambayo Sempeta aliifanya baada ya kurudi pia alisema kuwa:
“… Uhuru wa Kenya ni bandia na anao ushahidi wa hilo.”
Wiki hiyo hiyo Sempeta aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake na watu wasiojulikana. Hii si dalili ya nchi kuwa huru au kuwa yenye demokrasia.
HITIMISHO.
Kitu kinachoitafuna nchi ya Kenya; kitu kinachoifanya Kenya iwe na vita ya wao kwa wao isiyokwisha ni umiliki usio wa haki wa ardhi. Siyo ukabila.
Kwa mujibu wa takwimu za 2011 idadi ya watu wasio na ardhi kabisa pamoja na wenye pungufu ya eka moja (ambayo ni sawa na hakuna) ni milioni 33.2.
Hawa wengi wao ni watu ambao hawana namna ya kujikimu. Hawana ardhi, hawana ajira na wala Serikali haitoi ruzuku yoyote, yaani hakuna “Social Security Benefits”.
Wakati huohuo familia moja (jina nalihifadhi) inamiliki ardhi ambayo ukubwa wake ni sawa na jimbo la Nyanza (Nyanza province) na ukubwa wa Nyanza ni sawa na mkoa mzima wa Mtwara.
Hivyo basi, kutegemea amani iwepo katika hali kama hii ni ndoto za ki – Ali Nacha.
Tahadhari.
Jimbo la Afrika Mashariki chonde lisifanye kosa la kuunda kitu kinachoitwa Shirikisho mpaka nchi zote wanachama zitakapotaifisha ardhi nchini kwao na kuleta mgao wa haki; mgao utakao -“guarantee” amani ya kudumu na siyo vita vya wenyewe kwa wenyewe visivyo na mwisho. Nchi ya Rwanda imefanya hivyo, hakuna sababu hizo nchi nyingine zishindwe.
Uhuru na demokrasia ya kweli ni ile inayoleta “broad-based peace and prosperity” katika nchi; na hiyo si hali ambayo inaonekana Kenya na Afrika Kusini.