
WU® MEDIA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema CCM, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Ndugu Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa uongozi na kusimamia ili kuhakikisha diplomasia ya uchumi na siasa inaendelea kuiwezesha Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla, kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani na nje ya nchi.
Balozi Dk. Nchimbi amesema mabadiliko mbalimbali ya kisera na mwelekeo, chini ya Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yameendelea kuwa sehemu ya dira ya Tanzania katika kutafuta matokeo chanya ya haraka yanayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa mnufaikaji sawa katika uhusiano unohusisha pande mbili, kila wakati, iwe kati ya nchi na nchi au nchi na taasisi za kimataifa.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Nchimbi ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Mabalozi wa Nchi za Misri na Korea Kaskazini wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, Mhe. Sherif Abdelhanid Ismail na Komredi Kim Yong Su, mtawalia, pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Friedrich-Ebert-Stiftng (FES), nchini, Bi. Elisabeth Bollrich, Ijumaa, Aprili 5, 2024, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Sherif Abdelhanid Ismail amemhakikishia Balozi Dk. Nchimbi kuwa Nchi ya Misri, chini ya uongozi wa Rais Abd el-Fattah Saeed Hussein Khalil el-Sisi, inaichukulia Tanzania kuwa mmojawapo wa washirika wake wa karibu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano katika miradi mikubwa yenye athari chanya kwa uchumi wa pande zote mbili.
