Mjini Magharibu UNGUJA
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Leo Ijumaa Agosti 09, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.
Ujumbe huo ambao umeongozwa na Waziri katika Wizara hiyo Balozi Mahmoud Thabit Kombo, umefika Ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Migombani, Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja, kwa Lengo la Kujitambulisha, baada ya Mabadiliko ya hivi karibun, aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya Baraza lake la Mawaziri.
Akitoa Salamu zake mbele ya Ujumbe huo, Mheshimiwa Othman amesema ni vyema kwa Taifa kutumia fursa zilizopo katika Muunganiko wa Afrika Mashariki, ili kujiimarisha kiuchumi.
Amesema, Afrika Mashariki siyo Jumuiya tu, bali ni Shirikisho la kufungua fursa nyingi za kiuchumi ambazo zikitumika vyema, zitaleta tija kwa Taifa.
Aidha amewaelekeza Viongozi wanaosimamia Wizara hiyo, pia kuzitumia fursa zilizopo katika Taasisi za Kimataifa ili kuendana na kasi za kimaendeleo Ulimwenguni.
“Zipo Taasisi kama WIPO, zinazobeba fursa nyingi ndani yake, ambazo Mataifa ya Asia na Ulaya wanazitumia vilivyo kujinufaisha, ila kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla bado tupo nyuma sana; tukizingatia hili ni jambo adhimu kwa mustakbali wa maendeleo ya Nchi yetu “.
Aidha Mheshimiwa Othman amewahimiza Wahusika na Watendaji wa Wizara hiyo kutoa elimu, kwa Jamii za Wazawa na hata Wageni, juu ya Mambo ya Msingi yanayoihusu Serikali ya Muungano, na yepi ya Zanzibar, ili kuondoa mkanganyiko, sambamba na kuwajengea uelewa mpana wananchi, katika, kuelewa haki zao, na pia maeneo sahihi ya kupata huduma kwa wakati.
Akieleza suala la Tija kupitia Sekta za Utalii, kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Mheshimiwa Othman amehamasisha kuwepo kwa Kumbi za Mikutano zenye Hadhi ya Kimataifa, ili kuvutia Harakati za Mataifa ya Kigeni, kwa lengo pia la Kulinufaisha Taifa.
Hivyo, Mheshimiwa Othman ameridhishwa na Hatua ya Ujumbe huo, kuja na kubadilishana mawazo, huku akiahidi mashirikiano mema, kwa Maslahi ya Taifa.
Naye, Waziri Mahmoud ameahidi kwamba Wizara yake hiyo Mpya, itafanya kazi kwa karibu na Viongozi Wakuu, pamoja na Watendaji wote waliopo Zanzibar ili kuleta ufanisi, na kuhakikisha wanayafikia Malengo, kwaajili pia kuitangaza zaidi, Nchi katika Jamii ya Kimataifa.
Aidha, Mheshimiwa Mahmoud, ambaye ameshika Wadhifa huo hivi karibuni akitokea kuwa Balozi wa Tanzania Nchi Italia, ameahidi kuitendea-kazi miongozo na mashauri yote aliyopewa, kwa Maslahi ya Taifa.
Viongozi mbali mbali wamehudhuria katika kikao hicho wakiwemo Manaibu Waziri katika Wizara hiyo, Mhe. Cosato Chumi na Mhe. Denis Lazaro; Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji; pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Ndg. Ilyasa Juma Pakacha.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Agosti 09, 2024.