ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado inahitaji Wawekezaji zaidi kuja kuwekeza nchini kupitia sekta mbalimbali.
Ameeleza kuwa zipo fursa nyingi za Uwekezaji Zanzibar ambazo Wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza katika nyanja mbalimbali na kuishauri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka mkazo katika eneo hilo.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo tarehe: 09 Agosti 2024 wakati alipokutana na Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliefika Ikulu kujitambulisha baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Dk. Mwinyi amesema ni vema Wizara ijikite kutafuta Wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini pamoja na kunufaika Kidiplomasia na Mataifa mengine.
Aidha, Dk. Mwinyi ameishauri Wizara hiyo kuzielekea nchi za Asia na Mashariki ya mbali ambapo bado Zanzibar haijapata watalii pamoja na wawekezaji wa kutosha kutoka Mataifa hayo.
Amesema Serikali imeendelea kuweka Mazingira mazuri ya Uwekezaji na kuimarisha Miundombinu ili kuwavutia Wawekezaji kuja na kutumia fursa hizo.
Naye Balozi Mahmoud amemuahakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa Wizara itafanya kila juhudi kuyafanyia kazi maelekezo yake kufungua milango mipya ya Uwekezaji.
09 Agosti, 2024