
Rome, ITALY
Waziri Kombo akutana na DG Tume ya EU
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Tume ya Umoja wa Ulaya (EU), Bw. Koen Doens pembezoni mwa mkutano wa Mpango wa Mattei kwa Afrika na ‘EU Global Gateway’ jijini Roma, Italia.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wameangazia namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na EU ikiwa ni pamoja na kuendeleza miundombinu ya Tanzania kwa kukamilisha miradi ya mabasi ya mwendokasi na reli ya kisasa ifikapo 2030
Viongozi hao pia wamejadilia juu ya kushirikiana katika kurekebisha miundombinu chakavu hususan madaraja, ambapo Mhe. Waziri Kombo ameuomba Mpango wa ‘EU Global Gateway’ kutazama uwezekano wa kuwekeza katika miradi hiyo.
Mbali na hayo viongozi hao pia wameangazia ushirikiano katika teknolojia za kidigitali na zao la Korosho ambapo alisema kuwa korosho ya Tanzania ni moja ya mazao yenye ubora.
Vilevile Mhe. Waziri amesisitiza ushirikiano katika uchumi wa buluu eneo ambalo Serikali imeweka msamaha wa kodi kwa uingizaji wa vifaa vya uvuvi.
Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa biashara kati ya makampuni binafsi , sekta binafsi na serikali, pamoja na serikali kwa serikali, na kuwaalika kuja nchini ili kulielewa soko la Tanzania na fursa zake.
Naye, Bw. Doens amesema EU iko tayari kusaidia maendeleo ya mnyororo wa thamani kwa kuziunganisha sekta binafsi na taasisi za kifedha kama Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB), ili kupunguza hatari za uwekezaji.
Pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena katika Jukwaa lijalo la ‘EU Global Gateway’ litakalofanyika Brussels ili kuendeleza mazungumzo kuhusu maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano.



