
Angola
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano na mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Angola, ikiwa ni sehemu ya ziara yake rasmi nchini Angola.
Hafla ya utiaji saini katika Ikulu ya Rais wa Angola, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwemo pamoja na Rais João Lourenço wa Angola.
Mikataba ya ushirikiano iliyoidhinishwa inahusiana na sekta ya ulinzi, ambapo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, alisaini mkataba na Waziri wa Ulinzi wa Angola, Mhe. Jenerali Mstaafu Joao Ernesto Dos Santos.
Aidha, hati ya makubaliano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Uwekezaji Binafsi, Ukuzaji, Uwezeshaji, na Usafirishaji Nje Angola (Apex) pia ilisainiwa. Hati hii inalenga kukuza uwekezaji wa ndani na wa kigeni, na kujenga ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya pande zote mbili.
Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa mikataba hiyo katika kukuza maendeleo na kutoa fursa mpya kwa wananchi wa Tanzania na Angola. Amesema kuwa ushirikiano huo utaleta faida kwa pande zote na utaimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Rais João Lourenço wa Angola, ametoa pongezi kwa Tanzania kwa uungaji mkono wa ushirikiano huu na ameahidi kuendelea kushirikiana ili kutekeleza makubaliano hayo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.


