
Bunge la ANGOLA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka historia baada ya kuwa Kiongozi mwanamke wa kwanza kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Angola.
Akihutubia Bunge hilo jijini Luanda, Dkt. Samia ameeleza kufurahishwa na fursa hiyo adhimu, akisisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Angola umejengwa juu ya misingi imara ya urafiki, mshikamano, na mshikamano wa ukombozi wa Bara la Afrika.
“Ninajisikia kuheshimiwa sana kuhutubia Bunge hili tukufu la Angola. Hakika ni heshima ambayo siwezi kuisahau. Nawatakia kila la heri katika majukumu yenu ya kuwatumikia wananchi wa Angola,” alisema Rais Samia, huku akipigiwa makofi na wabunge wa Angola.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia amempongeza Spika wa Bunge la Angola, Mhe. Carolina Cerqueira, kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu katika historia ya taifa hilo. Amesema hatua hiyo ni ushahidi wa maendeleo ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nafasi za uongozi Barani Afrika.
Akigusia masuala ya kiuchumi, Dkt. Samia ameeleza kuwa Tanzania na Angola zina fursa nyingi za kushirikiana katika maeneo ya biashara, miundombinu, nishati, kilimo, na utalii. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya sekta binafsi za mataifa hayo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Spika Cerqueira amemkaribisha Rais Samia kwa heshima kubwa, akimtaja kama “mwanamke jasiri na kiongozi wa mfano barani Afrika.” Amesema hotuba yake imeacha alama kubwa kwa Bunge na wananchi wa Angola kwa ujumla.


















