0 0
Read Time:10 Minute, 37 Second

Uwanja wa Diplomasia

Na Abbas Mwalimu

23 Mei, 2021.

Tanzania ina historia pana na iliyotukuka katika ukanda huu wa SADC ambayo kamwe haiwezi kufutika.

Wakati huu Tanzania akiazimisha miaka 40 ya Jumuiya hii ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Southern African Development Community-SADC) tangu ilipoanzishwa kuna mengi ya kujifunza juu ya mchango wa Tanzania katika ukombozi, si tu wa nchi za SADC bali Afrika kwa ujumla.

SADC ilianzishwa kama Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern Africa Development Coordination Conference-SADCC) mnamo tarehe 1 Aprili 1980 na nchi 9 za Tanzania, Zambia, Angola, Botswana, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Zimbabwe na Swaziland sasa Eswatini ili kuondoa utegemezi wa kiuchumi na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini (ICG, 2012).

Baadae SADCC ilibadilishwa kuwa SADC mnamo tarehe 17 Agosti 1992 mjini Windhoek, Namibia ambapo Mkataba wa SADC uliopitishwa mwaka 1993. Rejea ICG (2012 na Khadiagala (2018).

Dhima ya SADC ni kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama 16 kupitia mifumo imara ya uzalishaji, kuimarisha utengamano wa kikanda, utawala bora na amani na usalama wa kudumu ili ukanda wa SADC uwe shindani na mshiriki kamilifu katika uhusiano wa kimataifa na uchumi wa dunia (http//:www.sadc.int).

Malengo ya SADC yamejikita katika kuunganisha nguvu za kiuchumi za nchi
wanachama, sambamba na hayo, SADC pia inaongoza nchi wanachama kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama kupambana na matishio yanayoweza kujitokeza katika nchi wanachama (Khadiagala, 2018 na http//:www.sadc.int)

Kama nilivyoeleza awali kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa Jumuiya hii tangu mwaka 1975 ikiwa imeanza kama Nchi zilizo Mstari wa Mbele (Front Line States) wakati huo Mwalimu Nyerere akiwa na Keneth Kaunda wa Zambia waliungana na Sir Seretse Khama wa Botswana, Samora Machel wa Msumbiji, Augustino Neto wa Angola sambamba na Ulesegun Obasanjo wa Nigeria.

Kabla ya hapo, historia ya SADC ilianzia mbali sana, tukumbuke mwaka pia 1958 kuliundwa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika kwa nchi za Mashariki na Kati mwa Afrika (PAFMECA) lakini kutokana na hitajio la kuzikomboa nchi za Kusini na hasa baada ya vyama kama SWAPO, MPLA na MNC kuhitaji kupata nguvu ya kupambana na ubaguzi na ukoloni Kusini sambamba na Ethiopia na Somalia, PAFMECA ilipanuliwa na kuitwa PAFMECSA mwaka 1962 lakini pia PAFMECSA ilivunjwa baada ya kuundwa kwa OAU mwaka 1963 (Rejea Cox, 1964: 2-3) pia rejea Cawthra, de Pisani na Omari (2007:50) katika Security and Democracy in Southern Africa.

Baadae Tanzania na Zambia ziliunda Jukwaa la Majadiliano kwa nchi za Kati na Kusini yaani Conference on East and Central African Countries (CECAC) ili kuziba pengo lililoachwa kutokana na kuvunjwa kwa PAFMECA (Cox, 1964:3 na Cawthra, de Pisani na Omari, 2007).

Baadae yalikuja makubaliano ya Lusaka ya mwaka 1969 na Azimio la Mogadishu la mwaka 1971 lililoamua ulazima wa kutumia majeshi yenye silaha ili kuikomboa Afrika.

Lakini kabla ya Azimio la Mogadishu kulianzishwa pia Mulungushi Club mwaka 1970 iliyohusisha viongozi wa nchi za Tanzania, Zambia, Uganda na Zaire ya wakati ule (sasa DRC). Mulungushi Club ilikufa mwaka 1974 kufuatia kutoamiwa kwa tabia za Mobutu Ssesseko na hivyo kutoa mwanya wa kuanzishwa kwa Nchi zilizo katika Mstari wa Mbele (FLS) ili kupambana na wakoloni (Omari, 1991) na Cawthra, de Pisani na Omari (2007) na hatimaye ikaja SADCC na sasa SADC.

Licha ya kuwa mstari wa mbele, Tanzania iliongoza Kamati ya Ukombozi iliyoratibiwa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wakati ule (sasa Umoja wa Afrika-AU) kamati iliyoongozwa na Marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

Kupitia Kamati ile Tanzania ilivipokea na kuvipa mafunzo vyama vya ukombozi kama vile ANC na PAC vya Afrika ya Kusini, ZANU-PF na ZAPU vya Zimbabwe, MPLA cha Angola, MNC cha Malawi, SWAPO cha Namibia, FLERIMO cha Msumbiji ambacho kilianzishwa Juni 25 mwaka 1962 Dar es Salaam, Tanzania na vyama vingine vingi ambavyo sijavitaja hapa.

Kwa maana hiyo huwezi kutaja Uhuru halisi wa Nchi hizo bila ya kuitaja Tanzania.

Vivyo hivyo kwa ujumla huwezi kuzungumzia ukombozi ama Uhuru wa bara la Afrika pasina kuitaja Tanzania, nchi ambayo kuna wakati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1959 alitamka kuwa, “Uhuru wetu haungekuwa na maana kama nchi nyingine za Afrika zilikuwa bado zipo chini ya utawala wa wakoloni”. Hii ni Tanzania, Tanzania ambayo sauti yake ilikuwa inapenya vilivyo katika masikio ya mabeberu na walowezi waliokuwa Afrika ya Kusini, Msumbiji na Zimbabwe.

Lakini tujiulize, je kwa sasa nafasi ya Tanzania ipo kama kipindi kile?

Kwa nini haipo kama kipindi kile?

Kufikiri sana kunatupeleka karibu na majibu. Nami kupitia makala hii fupi napenda kuwashirikisha jibu nililo nalo.

Wakati huu ambapo dunia inaongozwa na utandawazi na sayansi na teknolojia, suala la weledi linashika hatamu katika uongozi na uendeshwaji wa taasisi mbalimbali kama vile, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na hata Umoja wa Afrika (AU).

NI NINI TANZANIA INAPASWA KUFANYA KUREJESHA USHAWISHI WAKE MKUBWA KATIKA AFRIKA?

Kwanza ninaomba ieleweke kuwa si kwamba Tanzania haina ushawishi mkubwa kwa sasa katika SADC au AU bali ukilinganisha na ushawishi iliyokuwa nao Tanzania miaka ya 1960 mpaka 1980 utaona kuna utofauti kidogo.

Jambo ambalo linaweza kuirejesha Tanzania katika nafasi ya ushawishi iliyokuwa nayo kipindi cha Mwalimu Nyerere ni kurejea alichofanya Mwalimu Nyerere kwa namna mpya.

NI NAMNA IPI HIYO?

Kujikita kwenye tafiti na Maendeleo yaani Research and Development kwa kifupi R&D

Katika dunia hii ya sasa R&D ina nafasi kubwa sana ya kiushawishi wa kisera na kuleta Maendeleo.

Baraza la Taifa la Utafiti la Marekani yaani US National Research Council (2004) lilieleza:

“Recognizing the importance of Research and Development to national prosperity, the United States and other countries have developed systems that conceptualize, define and measure research and development activities so as to understand and to quantify the influence of research and development on the economy”

Kwa tafsiri yangu:

‘Kwa kutambua umuhimu wa tafiti na Maendeleo kwenye ukuaji wa taifa kiuchumi, Marekani na nchi nyingine duniani zimeandaa mfumo wa kuandaa mawazo, kutafsiri na kupima masuala ya tafiti na Maendeleo ili kuelewa na kukamilisha ushawishi wa Utafiti na Maendeleo kwenye uchumi.’

Kwa mtazamo wangu kupitia Utafiti na Maendeleo (R&D) Tanzania itaweza kurejea katika ushawishi iliyokuwa nao kipindi cha Mwalimu Nyerere.

NI VIPI IFANYIKE?

Awali ya yote, jambo kubwa la kushukuru ni kwamba ushawishi wa Tanzania umepatiwa nafasi nzuri kwa sasa, kwa nini?

Kitendo cha Umoja wa Afrika (AU) kuamua kukubaliana na wazo la Tanzania la kuwa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kunaifanya Tanzania kuwa na nafasi tosha kwa kurejesha ushawishi (influence) iliyokuwa nao katika miaka ya 1960 mpaka 1980 kabla ya kuisha kwa Vita Baridi na baadae nchi mbalimbali kujielekeza katika kurekebisha mifumo yake ya kiuchumi na kisiasa.

Ushiwishi huu ambao Tanzania inapaswa kuwa nao si wa kutumia nguvu (hard power) bali ni kutumia maarifa zaidi (soft power).

Na haya si maneno yangu tu bali Joseph Nye (1990:176) alifafanua kwa mapana namna nchi zinavyoweza kutumia maarifa kuongeza ushawishi badala ya mabavu. Nye (2011:11) alitoa tafsiri ya kutumia mabavu na kutofautisha na uwezo wa nchi kutumia ushawishi usio wa mabavu kufikia malengo yake (2004:5) hapa ndipo Nye (2005) alipoeleza namna nchi zinavyoweza kutumia nguvu janja (smart power ) katika kufikia malengo yao katika mahusiano ya kimataifa.

Nasi Tanzania tunapaswa kutumia soft power au smart power ili kurejesha ushawishi tuliokuwa nao Afrika na duniani miaka ile ya 1960 na kabla ya kuisha kwa Vita baridi.

Kupitia Kituo cha Urithi wa Ukombozi (African Heritage) kitakachojengwa Tanzania tunaweza kujifunza kutoka kwa John Kirton, Kirton yeye ni Profesa wa Kikanada ambaye mwaka 1987 baada ya kuona Canada inaweza isiwe na ushawishi mkubwa katika Kundi la Nchi zilizoendelea kiviwanda duniani (G7) ambalo lilizaliwa kufuatia Mkutano wa Wakuu wa Nchi pale Colorado, Denver, Marekani mwaka 1975 aliona kuna haja ya kuhodhi eneo muhimu la taasisi hiyo ambalo ni ‘utafiti’.

Ndipo hapo akaja na wazo la kuwa na Kundi la Utafiti la G7 yaani “G7 Research Group.”

G7 Research Group ni mtandao ulioenea duniani unaohusisha wanazuoni, wanafunzi, na wataalamu katika elimu, utafiti, habari,biashara, taasisi binafsi, serikali na taasisi nyingine za kikanda zinazofuatilia kazi za G7.

Baadae mwaka 1988 Profesa John Kirton aliunda pia G8.

Nchi hizo za G8 ni Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza, Marekani, na Urusi ambayo ilikuja kutolewa kufuatia kulitwaa eneo Crimea mwaka 2014.

Mwaka 1998 Profesa Kirton aliunda G20 Research Group.

Lengo la taasisi hizo (G7/G8 na G20) ni kuwa vyanzo huru na vikuu vya dunia vya taarifa, uchambuzi na utafiti kuhusu G7, G8 na G20.

Taasisi hizi za mkundi ya Utafiti la G7/G8 na G20 yapo chini ya Shule ya Munk ya Masuala ya Kidunia iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Toronto, Canada.

Kwa mujibu wa Steiner (2018: 21) ni kwamba:

Canada ina zaidi ya makundi matatu ya taasisi za kitaalamu yanayofuatilia mambo mbalimbali ya kimataifa kama vile; Taasisi ya Masuala ya Kidunia ya Chuo Kikuu cha Victoria, Taasisi ya Kimataifa ya Ubunifu katika Uongozi ya chuo Kikuu cha Waterloo na Shule ya Munk ya Masuala ya Kidunia ya Chuo Kikuu cha Toronto.

Shule ya Munk ya Chuo Kikuu cha Toronto ambapo Profesa Kirton anapatikana inamiliki taasisi za G7 Research Group, G8 Research Group na G20 Research Group.

Taasisi hizi ndizo zenye mamlaka ya kufanya utafiti, kushauri na kuchapisha masuala yote yahusuyo G7, G8 na G20 kupitia taasisi zao za taarifa (Information Centres).

Hushirikiana pia na B20,BRICS na Umoja wa Mataifa (UN).

Steiner (2018) anaeleza kwa kusema:

“Several academic institutions and engagement groups monitor the G-plus system in some manner.”

Kwamba, ‘Taasisi mbalimbali zataaluma na makundi ya tafiti hufuatilia shughuli za makundi ya G (G7, G8 na G20) kwa namna fulani.’

NAMNA IPI HIYO?

Ni kupitia ushawishi wa kisera (policy influence), na hili linathibitishwa na Utafiti uliofanywa na Profesa Kirton na wenzake (2013) kwenye “Compliance Studies” ambalo ushauri uliotolewa na G8 Research Group (2000:5) ulichukuliwa na taasisi hiyo ya G8 (Soma Corporate, Public and Governance cha Kirton na wenzake, 2013).

Ni wazi kuwa weledi wa Profesa Kirton umeiwezesha Canada kuzipiku Marekani na Brookings Institution yake, Uingereza na Chatham House yao na Ujerumani na taasisi yao iliyohodhi sera za Ulaya ya Heinrich Böll Foundation.

Nasi Tanzania hatujachelewa, tunaweza kutumia uwepo wa Kituo cha Urithi wa Afrika kitakachojengwa Tanzania kuathiri sera za kiuchumi hasa kutokana na kwamba lengo mojawapo la Kituo hiki ni kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu ukombozi wa Afrika.

Kutokana na hili la kuwa na nafasi ya kufanya tafiti kuhusu ukombozi wa Afrika ni vema Kituo hicho kikajielekeza pia katika ukombozi wa Afrika kiuchumi baada ya kuwa nchi za Afrika zimeshapata uhuru.

Tukumbuke sera nyingi za nchi za Afrika zilibadilishwa na kujielekeza kwenye ukombozi wa kiuchumi baada ya kuisha kwa vita baridi na pia mwanzoni mwa mwaka 2000. Rejea Sera ya Mpya Mambo ya Nje ya Tanzania ya Diplomasia ya Uchumi ya mwaka 2001.

Hivyo basi Tanzania tunahitaji kufanya tafiti za kina juu ya namna gani ya kuikomboa Afrika Kiuchumi baada ya kuwa Tanzania ilizisaidia nchi nyingi za Kusini na Kati mwa Afrika kupata uhuru wao.

Hivyo basi kupitia kituo hiki cha Urithi wa Ukombozi, Tanzania inapaswa kuwa nchi kiranja katika tafiti za ukombozi wa kiuchumi ili iweze kuhodhi mawazo,fikra, sera a muelekeo wa SADC na Umoja wa Afrika (AU) kupitia vyuo vikuu vyetu mbalimbali nchini.

Hili si jambo la kustaajabisha kwani Urusi wamefanya hivyo kupitia Taasisi ya Tafiti kwa Ajili ya Taasisi za Kimataifa yaani Centre for International Institutions Research (CIIR) iliyo chini ya Chuo cha Taiga cha Uchumi wa Urusi na Utawala yaani Russian Presidential Academy of National Economy and Public Administration (RANEPA).

CIIR inafanya tafiti kwa ajili ya Muungano wa BRICS yaani Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini.

Japan nao hawapo nyuma sana kwani wana taasisi yao ya Ushauri ijulikanayo kama Kundi la Ushauri laJapan yaani Japanese Advisory Group.

Kundi hili ni mahsusi kwenye kutoa ushauri juu ya Japan na Afrika kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kwa Maendeleo ya Afrika yaani Tokyo International Conference for African Development (TICAD).

Wakati huu ambapo Afrika inajielekeza kwenye kuwa na eneo moja la kiuchumi yaani African Continental Free Trade Area (AfCFTA) kama inavyoelekeza ‘Agenda 2063’ hatuoni haja kwa Tanzania kutumia Kituo cha Ukombozi Afrika kuibua mawazo ya kitaaluma kupitia AFCFTA” ili tuhodhi uelekeo wa Afrika kisera na kuongeza ushawishi wa kisera Afrika nzima?

Huu ndiyo muelekeo mpya ambao naamini Tanzania inapaswa kuwa nao na kuusimamia kwa kujielekeza kwenye tafiti na maendeleo (R&D) kupitia Kituo cha Ukombozi Afrika kitakachojengwa Tanzania ili kuweza kuathiri (influence) muelekeo wa Kisera wa Afrika kama alivyoeleza Joseph Nye katika ulinganifu wa kutumia mabavu (hard power) na kutumia maarifa zaidi (soft and smart power). Kwa kuwa Mwalimu Nyerere alielekeza kujenga Hoja na si kupiga kelele katika andiko lake la ‘Argue Don’t Shout’ la mwaka 1969 nami hoja yangu ni hiyo.

Asanteni.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook & Instagram)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook na WhatsApp)

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %