
KISWAHILI LUGHA YA KWANZA YA KIAFRIKA KUTAMBULIWA NA UMOJA WA MATAIFA KUADHIMISHWA KIDUNIA KILA JULAI, 7- KONGOLE MHESHIMIWA SAMIA KUENDELEA KUUPIGA MWINGI
Anaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu
Sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mola wetu mtukufu.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Kazi iendelee.
Siku ya jana tarehe 23/11/2021 imekuwa siku ya furaha na imeleta buraha kwa wapenzi wa lugha adhimu na aushi ya Kiswahili kote duniani.
Buraha hii, imekuja kufuatia Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na Utamaduni (UNESCO) kiutangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili Duniani
Taarifa hii njema ilitangazwa jana tarehe 23/11/2021 kwenye makao makuu ya UNESCO mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano Mkuu wa 41 wa nchi wanachama wa Shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa katika ukurasa wa mtandao wa Twitter wa UNESCO AZIMIO maalumu la kuitangaza siku hiyo limepitishwa na wanachama wote bila kupingwa.
Hatua hiyo muhimu inakifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa
Kutokana na hatua hiyo, nikaona niandike makala fupi ya kiuchambuzi kuonesha kwa nini Kiswahili? na hatua hii ina maana ipi katika maendeleo ya Kiswahili duniani.
Kabla ya kuendelea na uchambuzi hu ni vema nikatumia fursa hii kutoa Kongole kwa Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan, yeye pamoja na serikali yake kwa kuhakikisha hatua hii muhimu inafikiwa.
Kama tunakumbuka vema, Mheshimiwa Rais Samia mnamo tarehe 22/04/2021 alipokuwa akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu kuapishwa kwake tarehe 19/03/2021, pamoja na mambo mengine. Aliahidi kuwa serikali yake itaendelea kuhimiza masuala ya utamaduni, sanaa na kuendeleza michezo kwani ni sekta muhimu kwa Taifa. Aidha, alisisitiza kuwa serikali yake ya awamu ya 6 imejipanga kutekeleza shughuli za kidiplomasia kuendana na sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Azma hizo za Mheshimiwa Rais Samia, zimekuwa na tija kubwa katika kuendeleza lugha ya Kiswahili ikiwa ni nyenzo muhimu ya utamaduni na Diplomasia.
Hadi hivi leo tangu aanze utawala wake tumeshuhudia maendeleo makubwa ya lugha ya Kiswahili ikiwa ni mwendelezo wa kazi iendelee tangu kwa mrithi wake hayati J.P Magufuli.
Miongoni mwa mafanikio ya Mheshimiwa Rais Samia katika Kiswahili ni pamoja na kutumika Kiswahili SADC, sheria kutafsiriwa kwa Kiswahili, kutumika Kiswahili katika shughuli za umoja wa Afrika, kuhimiza Matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kutoa hotuba kwa Kiswahili kilichosheheni misemo mbalimbali ya Kiswahili na kubwa ni hili la Kiswahili kuwa na siku mahsusi ya kuadhimishwa duniani.
Tunatumia fursa hii kutoa Kongole kwake na kwa mawaziri na viongozi wote kuendelea kupambania lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

Hali ya Kiswahili sasa Duniani
Kwa muhtasari, nieleze kuwa kwa sasa lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa duniani. Takwimu zinaonesha ina jumla ya wazungumzaji wasiopungua milioni 200, ni miongoni mwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, ni lugha rasmi katika mikutano ya umoja wa Afrika, kinafundishwa katika nchi mbalimbali duniani kama vile Chuo Kikuu cha Helsinki(Ufini), Hankuk (Korea Kusini), Napoli (Italia), Bayreuth (Ujerumani), Leiden (Uholanzi), Osaka na Tokyo (Japan), Beijing (China) Michigan, Indiana, Yale, (Marekani), Lumumba (Russia), Al-Azhar (Misri) kutaja kwa uchache. Pia, Kiswahili kwa sasa kinatumika katika vyombo mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa duniani, Kiswahili ni lugha ya mawasiliano mapana katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini.
Bila shaka hatua hii ya kuwa na siku ya Kiswahili duniani imekuja wakati mwafaka kwani Kiswahili kama tulivyoona kimatamalaki dunia nzima.
Kiswahili na UNESCO
Hatua hii ya UNESCO kwa kumbukumbu zangu ni mwendelezo ya Shirika hili katika kuendeleza lugha ya Kiswahili. Mathalan, kwa mujibu wa Jarida la Wizara ya mambo ya nje la Blog katika mtandao wake tarehe 23/Februari/2020 lilibainisha kuwa UNESCO ilikitambua Kiswahili kama lugha itakayosaidia kukuza utangamano barani Afrika. Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa kudumu wa UNESCO, Mh.Samweli Shelukindo alilipigania hili ipasavyo na hatimaye kupitishwa Kiswahili tangu mwaka 2020 kuwa lugha ya itakayosaidia kukuza utangamano barani Afrika. Jana dunia imeshuhudia Kiswahili kupiga hatua nyingine ya kimataifa.
Hatua hii ina umuhimu gani?
Lugha sio tu chombo cha mawasiliano. Bali lugha ni kielelezo cha utamaduni na utambulisho wa amali, maadili na dira za jamii. Lugha husaidia kuchochea utangamano na kukuza biashara na mawasiliano kwa jamii. Hatua hii kwa maoni yangu itasaidia mambo yafuatayo:
Mosi, itasaidia kuendelea kulinda na kukuza utamaduni wa Waafrika
Pili, itasaidia kustawisha tamaduni na kusaidia watu kutangamana kwa manufaa ya kila mmoja.
Tatu, itasaidia kukuza mawasiliano na usemezano wa watu mbalimbali na kuongeza utangamano wenye kuleta heshima na amani duniani.
Nne, kuongeza na kuimarisha uhusiano mwema wa kikanda na kidunia.
Tano, itarahisisha mawasiliano katika usambazaji wa taarifa na mambo yanayohusu Kiswahili.
Sita, itaongeza wigo na njia ya kukikuza na Kukitangaza Kiswahili Duniani.
Nini cha kufanya kufuatia hatua hii?
Kufuatia hatua hii muhimu. Sisi wapenzi, wadau wa Kiswahili na kila asasi ya Kiswahili hapa kwetu Tanzania pengine na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki tunapaswa kufanya yafuatayo:
Mosi, kuongeza mbinu za Kisasa za kukitumia na kukitangaza Kiswahili duniani.
Pili, kuongeza hamasa zaidi ya kukubalika kwa Kiswahili duniani.
Tatu, kusambaza kwa haraka na kwa makini habari zote zihusuzo Kiswahili
Nne,kuongeza ushirikishwaji wa wadau wengi wa Kiswahili katika mambo yanayohusu Kiswahili
Tano,kuhamasisha wadau wa fani nyingine kama vile za Uhandisi, sheria, habari n.k kukipenda Kiswahili na kukitumia katika shughuli zao
Sita, kuandaa makongamano, warsha, matamasha, midahalo siku ya tarehe 7/7 kila mwaka ili kuihanika Sikh hiyo adhimu ya Kiswahili duniani.
Kongole
Kwa mara nyingine tena, napenda kutoa Kongole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu na VIONGOZI wetu wote hususan Mheshimiwa Bashungwa Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo na Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki na VIONGOZI wote wa Mabaraza ya Kiswahili, Vyuo Vikuu, VYAMA vya Kiswahili kwa kazi kubwa na jitihada zao za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Hayati Dkt.Mohamed Seif Khatib aliwahi kusema Kiswahili kina Kesho na Baba yangu Mzee Sovu akaniambia Kiswahili ni Kiafrika sasa naoni kimekuwa cha kidunia.
“Titi la Mama litamu lingine haliishi hamu.“
0713400079
Mhadhiri Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni -Dsm.








