
TUSEME UKWELI ILI KUMLINDA MH RAIS MAMA SAMIA SULUHU HASSAN!
George Michael Uledi.
Kyela,Mbeya.
October 11,2022.
Political strategists na Think Tank wa Chama changu CCM kama kweli bado hawayaoni yanayoendelea Nchini na kuweza kuishauri Serikali kimkakati basi naiona hatari kubwa mbeleni inakuja!
Juzi Makala moja ya hovyo kabisa ilikuwa inatembea kwenye mitandao ya kijamii ikisomeka na kichwa cha habari hiki”Makubaliano ya Fedheha” ikiitaja timu ya majadiliano kuhusu Mgogoro wa Barrick na Tanzania maarufu kama timu ya Makinikia ya Profesa Paramagamba Kabudi Mwaluko kufanya “ziro job”na makala Ile inasema hakuna la maana Serikali ya awamu ya tano ilifanya zaidi ya kupoteza muda tu!
Gazeti la Raia Mwema la Juzi likaendeleza uchochezi zaidi kwa kuandika habari front page”Samia Afunga Duka” huku ikielezea kile kilichoitwa “mradi” wa Serikali ya awamu ya tano kupitia Sheria halali ya Bunge yaani “Plea Bargaining” kwamba ilikuwa unachunguzwa na Ofisa ya CAG!Matukio haya mawili ni wazi kuwa yanaweza kuibua upinzani wa ndani kwa ndani,ndani ya Chama changu pendwa CCM!
Mwenyekiti wangu wa CCM Taifa,Mh Mama Samia Suluhu Hassan hapaswi kuhusishwa kwa namna yoyote na michakato ya kisheria ndani ya ofisi ya CAG!Kama Ofisi ya CAG imeamua kukagua fedha hizo za Plea Bargaining basi itambulike hivyo kwa maana hiyo ni kazi yao ya kila siku”routeen job” na wala Mh Rais asihusishwe kwa vyovyote na maneno ya “kufunga duka” wala “kufungua duka”,hakuna kitu kama hicho!
Mh Rais juzi wakati akiwaapisha Mawaziri watatu Ikulu baada ya kufanya marekebisho madogo kwenye Baraza lake alisisitiza umuhimu wa wateule kuijua kuicheza dhana nzima ya “collective responsibility” kwamba maamuzi ya Serikali hata kama hauyapendi,mteule unapaswa kuyabeba na kuyaimba na ikibidi kuyatekeleza kabisa!
Kwa muktadha huo haiwezekani leo Magazeti fitinishi yaanze kumuhusisha Mama Samia na kazi halali za CAG kwa kumwandika kama ameamua “kufunga Mradi wa Watu fulani” wakati na yeye alikuwa sehemu ya maamuzi hayo wakati wa Serikali ya awamu ya tano!Huku ni kupunguza kura za CCM na kuidhofisha CCM hivyo kuifanya kazi ya kumtafutia kura Mama Samia Mwaka 2025 kuwa ngumu zaidi!
Nitakuwa sijatimiza wajibu wangu kama Kada na kijana wa CCM nikishindwa kuweka sawa rekodi hizi kwani zina athari za moja kwa moja kuelekea kuutafuta ushindi wetu mwaka 2025!Nikiwa mmoja wa wana team ya kutafuta kura za Mama Samia Mwaka 2025 lazima nitoe angalizo kwa Chama changu na Serikali yangu na kusema kuwa,haya yanayoendelea kwenye social media hakika yanatukula sisi wenyewe kwa wenyewe!Ajenda ya JPM haina maslahi yoyote kwa CCM ya sasa!
NIRUDI KWENYE “MNANGO” DHIDI YA TIMU YA PROFESA KABUDI!
Makubaliano hayo yalikuja baada ya Serikali ya Tanzania ya awamu ya tano kuamua kuunda timu ya majadiliano dhidi ya Wawekezaji wa Kampuni ya Barrick kufuatia uwepo wa udanganyifu katika biashara nzima ya Madini ya dhahabu kati ya Kampuni ya Barrick dhidi ya Serikali hasa kwenye usafirishaji wa mchanga wa dhahabu maarufu kama makinikia!
Msingi wa majadiliano hayo tofauti na watu wengi wanavyodhani kwamba labda yalianzia wakati wa Serikali ya awamu ya tano lakini ukweli ni kuwa, majadiliano hayo yanatokana na Kamati mbalimbali ziliwahi kuundwa na Serikali huko nyuma na kubaini hitaji la kurekebisha baadhi ya Sheria zetu katika Sekta ya Madini ikiwemo suala la mchanga wa makinikia!
Baadhi ya Kamati hizo ni Kamati ya CDF Mstaafu, Generali Robert Mboma( 2002),Kamati ya Dkt Jonas Kipokola ((2004),Kamati ya Dkt Enos Bukuku (2005),Kamati ya Ndugu Lawrence Masha (2006),Kamati ya Jaji Bomani(2008),na Kamati ya Profesa Mruma na Profesa Osoro(2017).
Kamati hizo karibia zote zilipendekeza kufanyika kwa mapitio na marekebisho ya msingi ya Sheria mbalimbali katika Sekta Madini lakini labda kulikosekana utashi wa kisiasa mpaka ilipofika Mwaka 2017 baada ya Mh Rais hayati John Pombe Magufuli na Makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan kuamua kwa dhati kabisa kuifumua Sheria ya Madini ya Mwaka 2010(Mining Act ,2010).
Moja kati ya Kamati bora kuwahi kuleta msukumo mkubwa katika mabadiliko katika Sekta Madini Nchini basi si nyingine zaidi ya Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma ambayo ilizama “kijasusi” ndani na Barrick na kuja na taarifa za kutisha na kutosha kuhusu udanganyifu mkubwa ulikuwa unaendelea kwenye Sekta ya Madini kupitia Kampuni kongwe ya Barrick hasa kwenye usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya Nchi!
REPOTI YA PROFESA MRUMA YAWAAMSHA WADAU NA WATANZANIA USINGIZINI.
Repoti hiyo ya Profesa Abdulkarim Mruma ilianisha angalau maeneo makuu mawili matatu kuhusu biashara ya makinikia iliyokuwa ikifanywa na Barrick, kwanza kabisa Repoti ilionyesha uwepo wa (I) Udanganyifu kutaja kiasi cha Madini yanayotajwa kupatikana kutoka kwenye makinikia hayo”under declaration”,(II)Pili ni kufichwa kwa taarifa sahihi kuhusu Madini mengineyo yanayopatikana kupitia makinikia hayo kama Chuma na mengineyo!
Kutokana na udanganyifu huo ulikuwa ukifanywa na Maofisa wa madini wa Serikali na Kampuni ya Barrick kwa Miaka 19,Serikali ya Tanzania ilikuwa imepoteza na inapoteza kiasi kikubwa cha mabilioni ya fedha!
June,2017,Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-WAZALENDO Ndugu Addo Shaibu akiongea na waandishi wa habari kuhusu Repoti hiyo alisema Chama chake kimeipokea Repoti hiyo kwa mstuko mkubwa na kwamba kinaandaa na kushauri uwepo wa mjadala wa kitaifa kuhusu uvunaji wa rasilimali madini Nchini!Alisema Repoti hiyo ni case study ya mgodi mmoja tu kwahiyo Chama chake kilikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba uenda masuala kama haya ya makinikia pia yanaendelea katika migodi mingine Nchini!
May 27,2017, Mwenyekiti wa CDM Taifa Ndugu Freeman Mbowe aliwashutumu waziwazi Mh Rais wa awamu ya tatu hayati Mkapa na Rais wa awamu ya Nne Mh Rais Jakaya Kikwete kuhusika moja kwa moja katika mikataba hiyo!Ona sasa lawama kila kona!Hakuna Serikali duniani ambayo haifanyi makosa katika kutekeleza maamuzi ya maendeleo!Hakuna!
Profesa Haji Semboja alisema “siku zote natofautiana na wengi kuhusu sheria zetu katika umiliki,Ulinzi na uvunaji wa biashara zainazohusu rasilimali za Taifa…tubadili sheria na mfumo wa uvunaji wa rasilimali za Taifa…”.
REPOTI YA PROFESA MRUMA YAZAA VIKOSI KAZI VYA MAJADILIANO KUHUSU FIDIA NA MUUNDO MPYA WA MAPATO KATI YA SERIKALI NA BARRICK GOLD!
Tukumbuke kuwa wakati huo hatukuwa na sheria nzuri sana kwahiyo,Nchi ya Tanzania iliingia kwenye majadiliano haya kwa “ujeuri” tu sababu wakati ule tunaingia kwenye majadiliano haya, hakukuwa na Msingi wowote wa kisheria wa kuweza kuwabana to that extent Barrick lakini angalau tulipata sehemu ya kuanzia!Kusema majadiliano yake yameleta fedheha kwa Taifa ni “ukicha” wa viwango vya juu sababu angalau kwa mara ya kwanza tuliweza kupata kitu kama Taifa lakini zaidi majadiliano yake yalifungua fursa na njia pana zaidi ya kuelekea kwenye marekebisho ya sheria zetu za Madini ya Mwaka 2010 hivyo mpaka sasa Taifa linafaidika na marekebisho hayo ya sheria hizo mpya!
Kabla ya Sheria mpya ya Madini, Tanzania ilikuwa ikipata Tsh. 100+ Bilioni pekee kwa mwaka kutoka kwenye Sekta ya Madini lakini baada ya Sheria ile, Tanzania angalau inapata Tsh 500+ Bilioni kwa Mwaka 2020!Je,huu sio ushindi mkubwa kwenye Sekta husika?
Unyeti wa suala hili lilipelekea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli kukataa kuyaweka wazi majina ya watu wa serikali ambao walikuwa wanaingia kwenye majadiliano dhidi ya Barrick kuhusu namna ya kugawana utajiri wa Madini pamoja na makinikia!Kuonyesha unyeti na uzito wa jambo hilo kwa Barrick,pia nao timu yao iliongozwa na Kamanda wa zamani wa vikosi vya Marekani Nchini Afrighanistan!
I.Majadiliano hayo yaliishia kwa ushindi mkubwa kwa Serikali ya Tanzania baada ya makubaliano ya Tanzania kulipwa mabilioni ya Shilingi ndani ya miaka saba!Mfano,Repoti ya Profesa Mruma ilisema kuwa Tanzania imepoteza Tsh 188 Trilioni katika miaka 19 kati ya Mwaka 1998 mpaka mwaka 2017.
Makubaliano hayo pia yaliifanya Serikali ya Tanzania kuruhusu shehena ya makinikia ambayo yalikuwa yameshikiliwa pale Bandari ya Dar es alaam!(II)makubaliano ya kuanzishwa kwa Kampuni ya pamoja kati ya Serikali na Barrick yaani Kampuni ya Twiga Corperation,(III)Serikali kupewa asilimia 16 ya hisa ndani ya uwekezaji wa Barrick na Barrick kutakiwa kufungua akaunti zake zote za fedha Nchini Tanzania ambayo yote kimsingi yalikubaliwa!
Repoti ya Profesa Mruma na baadae Kamati ya majadiliano ya Profesa Mwaluko Kabudi ilikuja na manufaa makubwa yenye maslahi ya Taifa sio tu katika kipengele cha kodi bali pia katika urekebishaji na wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kuhusu Sekta ya Madini ambayo iliweza kukuza sekta ya madini ndani ya muda mfupi sana!Miongoni mwa mambo makubwa na ya msingi ambayo ni matokeo ya Kamati ya Profesa Kabudi ni kutaka sasa kuweka msingi wa Kisheria kuhusu Ulinzi wa rasilimali za Taifa kwa;
I.Uanzishwaji wa Hifadhi ya vito chini ya Banki Kuu ya Tanzania “Establishment of the National Gold and Gemstone Reserve”(II)Uanzishaji wa maeneo maalum ya Masoko ya dhahabu na (III)Uanzishaji wa maghala ya kuifadhi madini”Government Minerals Warehouses” pamoja na mambo mengine mengi yenye maslahi kwa Taifa ambayo mpaka sasa yanatumika!
JE, HAYA NDIO “MAKUBALIANO YA FEDHEHA??”
Mwandishi mmoja wa Makala inayosomeka “Makubaliano ya fedhaha”,Ndugu yetu Martin Masesa Mtikila,anasema makubaliano ya timu ya Profesa Kabudi na timu ya Barrick Gold yalikuwa ni kiiini macho tu na hakuna la maana lillilofanyika!Upotoshaji huu haupaswi kufumbiwa macho kabisa na Vijana wanajua nini maana ya maslahi ya Taifa!(I)Kampuni ya Twiga Corperation ni zao la timu ya Kabudi,(II)Mh Luhaga Mpina anakiri Serikali tayari imepokea Tsh 700 Bilioni,rejea swali lake Mwezi September,2022 Bungeni (III) Serikali kupewa asilimia 16 ya hisa za Barrick na mengine mengi!Je,huu sio ushindi mkubwa?,kumbuka hapo kabla ya majadiliano, Serikali ilikuwa haina hisa, haipati kiasi chochote kutokana na makinikia na wala hakuna Kampuni ya kizalendo ya Twiga Corperation!
Serikali inaendelea kukiri kupitia Katibu Mkuu wa WIZARA ya Fedha na Mipango, Emanuel Tutuba anasema kama ambavyo walikubaliana kwa kulipa dola Milioni 100 mwaka wa kwanza na nyingine baadae na wamekuwa wanalipa!
” Katika miaka mitano mingine,wamekubali kuwa wanalipa dola Milioni 40 kila Mwaka na wamekuwa wakilipa kila mwaka…” Katibu Mkuu Hazina amenukuliwa!
Ni wazi kuwa Makala ya Ndugu yetu Martin Masesa Mtikila ilikuwa na lengo maalum either kuifurahisha Barrick au kumfedhehesha Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mama Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya manufaa ya Kampuni ya Barrick na labda kutaka “to kill the case” ya madai yetu dhidi ya Kampuni ya Barrick baada ya Mbunge wa kisesa na Spika wa Bunge kusimama IMARA kutaka kujua ukweli kuhusu fedha hizo!
Zaidi makala Ile inaweza kuwafanya watanzania waanze kuhoji kwanini Serikali yao ya awamu ya Sita ya Mama Samia imeamua “kuuwa kesi” kwa kutokusanya madai halali ya Serikali dhidi ya Barrick? na bahati nzuri Mh Rais Samia anajua vizuri story nzima kuhusu makubaliano yale!
Serikali ya awamu ya Sita ya Mama Samia itaendelea kukusanya na kupokea fedha yote kutoka Barrick kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili”mutual agreement” kwa ajili ya maendeleo ya watanzania wote!
Mwandishi ni Kijana na Kada wa CCM,Makamu wa Rais wa zamani,Daruso -IJMC,Ofisa wa zamani,Idara ya Habari-Maelezo,Ofisa Mwanafunzi wa zamani,Chuo cha Maofisa wa Jeshi Monduli Arusha,Mhadhiri Msaidizi wa zamani,Vyuo Vikuu vya Tumaini na Saut na Mtia Nia Ubunge Jimbo la Kyela 2020.
+255746726484.








