
Watu 29 wamehukumiwa na mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kwenda jela mwaka mmoja baada ya kukiri kosa la kutoka ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwenda nchini Afrika Kusini bila ya kuwa na kibali. Washtakiwa hao ni Human Jumanne, Michael Audi, James Elias, Juma Hussein, Isiaka Ally, Issa Kumchanya, Mukhsin Maulana, Juma Mpera, Iman Edward, Adam Kitenge, Richard Aliwane, Sadiki Ugaza, Alex Subekeri, Sadick Sangiro.
Wengine ni Hassan Kikome, Said Abdullaman, Salehe Ngwele, Nahid Kubwa, Abdul Mzinga, Ramadhan Mboke, Owen Obina, Khalfan Matibwa, Musa Athuman, Kassim Mbegu, Thomas John, Juma Salehe, Erick Lumbika na Hemed Muhando.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa Novemba 13, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi aliyeeleza mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote wamekubali kosa linalowakabili na hawakuisumbua mahakama hiyo.
Shaidi amesema washtakiwa hao umri wao ni mdogo hivyo wanatakiwa kujenga maisha yao ya baadaye na hakuna binadamu aliyeumbwa kuwa tegemezi.








