0 0
Read Time:2 Minute, 27 Second


Thalamaleku Dadi!

Mazungumzo na @⁨AbuLuLuFaJM⁩

NILIRUDI nyumbani jioni baada ya mizunguuko yangu ya kimaisha. Kwa kawaida mwanangu mdogo, Lulufa, hunikimbilia kwa shangwe kuja kunipokea, lakini siku ile nilishangaa alikuwa “kauchuna”. Nikamuuliza: “Lulufa, vipi mwanangu?” Kimya! “Hujambo?” Kimya!

Baada ya kumhojihoji ili kumdadisi nifahamu tatizo lilikuwa nini, alitoa maneno ya ukali akisema: “We thio lafki yangu teena!”

Waliokuwepo waliangua kicheko na kusema tu, “Lulufa bwana!”

Nilimuuliza kwa nini mimi sio rafiki yake, nikagundua sababu. Kumbe nilikuwa nimemkaripia asubuhi kabla sijaenda kazini, kwa sababu alikuwa hataki kwenda shuleni eti kwa sababu alikuwa amechoka sana ile asubuhi.

Nilichokifanya ni kutoa kafuko ambako ndani kalikuwa na vituvitu vya kutafuna, kama ilivyo kawaida nikirudi nyumbani. Nikasema: “Sawa kama mimi thio lafki yako”.

Lulufa alipoona kale kafuko akajua mna vitu. Akawa anatafuta Suluhu. Akaja mbio huku akisema: “Thalamaleku, Dadi!”
Waliokuwepo wakaangua kicheko tena. Bila ya kuwajali waliokuwa wakicheka, alisema: “Nilikuwa nadanganya tu Dadi, wewe ni lafki yangu”.

Kwa nini alifanya hivyo? Alijua kwamba uadui wake kwangu ungemkosesha maslahi, walau kwa kipindi kile kifupi cha neema.

Wengi waliokuwepo waliangua kicheko tu, wakiishia kusema: “Lulufa bwana…! Watoto bwana! Lakini kwa watu wa fasihi kila tukio lina maanisho katika maisha, na vile vile kwa watu wa fasihi maisha yote ni tamthilia, unaweza kuyafanyia uchambuzi.

Nilikuwa nafikiria niandike nini leo, lakini tukio lile dogo kwangu likawa na maanisho kubwa zaidi katika maisha yetu leo kuliko wale waliokuwa wakicheka tu walivyolichukulia.

Miezi kadhaa nyuma vigogo wa vyama vya upinzani haswa wa vyama fulani walikuwa wametuamanisha kuwa serikali hii na chama chake na viongozi wote hawafai kabisa kuingoza nchi.

Wakajitahidi sana kwa udi na uvumba kuwaaminisha Wananchi, kupitia mitandao ya kijamii, uko mkondooni kuna jamhuri kadhaa za mtandaoni.

Kuna mashujaa wa mtandaoni, wanaokesha kwa kuandika kila uchwao kuwa serikali hii ya chama hiki sio na haifai, wapo wachache wanaoamini kuwa wayasemayo ni kweli kwa sababu wanatuhakikishia kuwa wanao ushahidi wa viroba na hata wakifikishwa mahakamani hakuna tatizo kwa sababu ushahidi wanao.

Ajabu ni kwamba serikali hii hii na chama chake na viongozi wake walewale ndio hao hao wanaoendelea kuongoza nchi.

Serikali hiihii ya chama hikihiki, sera ni zilezile, leo wanashangiliwa sana na jamhuri ya mtandaoni kwa nyimbo na vigelegele.

Sasa baadhi ya wananchi tunajiuliza, je wamesalimu amri!?

Hawa mashujaa wa mtandaoni zile hasira zao kwa serikali hii wakati ule zilikuwa za kweli au ilikuwa ni ile ile “we thio lafki yangu teena!”

Ukimkuta mtu utadhani mkali kweli, lakini ngoja vifuko vitolewe. Ona watu watakavyo badilika rangi. Angalia watu watakavyo rudisha kadi na kuomba radhi.

Ukiwa nje ya mchezo ndio unafaidi. Miye sina chama lakini ninapo pa kuegemea. Usiniulize wapi, kwa sababu wenye busara zao wameshatupa uhuru wa kuchagua tunapopapenda.

Nauliza tu wale wanaojidai wana hasira, hasira hizo ni za kweli au ni zile zile za “We thio lafki yangu teeeeeena!” Vifuko vikitolewa tu, “Thalamaleku Dadi!”

Maana keshasema kuwa kazi iendelee, mwendo uleule, walichukuwa na wataendelea kuteuwa kwa kuchua popote pale bila kujali wa wapi au katokea wapi…!

Thalamaleku!

Haya, tunaanza kuyaona!

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %