0 0
Read Time:9 Minute, 22 Second

Na Abbas Mwalimu(0719258484).

Alhamisi tarehe 10 Juni, 2021.

Jumanne tarehe 8 Juni, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alikutana na wanawake wa Dodoma katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma wakiwawakilisha wenzao wa Tanzania nzima ikiwa ni muendeleo wa utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya jamii nchini.

Katika mkutano ule zilielezwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini na hivyo kuwakosesha haki zao za msingi zilizoainishwa kwa mujibu wa Mkataba wa Haki za Binadamu wa mwaka 1948.

Katika kukabiliana na changamoto hizo Rais Samia alieleza kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ikiwemo CEDAW 1979, Beijing 1995, Mkataba wa Mtoto 1989, Agenda 2063 na Malengo Endelevu yaani SDGs.

Licha ya kuridhiwa kwa mikataba hii sambamba na itifaki ya Maputo ya mwaka 2003 bado juhudi za dhati na za makusudi zinahitajika kumuokoa mwanamke wa Tanzania kiuchumi kama alivyoainisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia ameonesha nia ya dhati kulipigania hili na kuhakikisha serikali yake inaleta usawa wa kijinsia kwa kuahidi kuyalea Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa kuwa kumuwezesha mwanamke si tu kunaleta usawa wa kijinsia kama lilivyoainisha lengo namba 5 kati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) bali pia kunaleta amani na usalama duniani (UN, 2015). Ndiyo maana makala hii inaitazama dhana ya usalama wa taifa la Tanzania katika muktadha wa mkakati wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuondoa umasikini.

Ni ukweli ulio wazi kuwa tukizungumzia umasikini nchini basi huenda wanawake ndiyo masikini wa kweli kabisa wakilinganishwa na wanaume na kwa hiyo changamoto hii ni dhahiri shahiri ni kitisho cha kiusalama.

Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu za mwaka 2002 zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (TNBS) na mapitio ya mwaka 2021 zinaonesha kuwa kati ya watu 59,441,988 wanawake ni 30,309,750 sawa na asilimia 51 ya watu wote.

Asilimia kubwa ya wanawake hawa zaidi ya milioni 30 wamejiajiri katika kilimo kama ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa ya mwaka 2015 inavyobainisha kwamba, sekta ya kilimo Tanzania imeajiri zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu wote na zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya wanawake wote (TNBS, 2015). Licha ya kwamba takwimu hizi ni za miaka mitano iliyopita na labda huenda kukawa na mabadiliko madogo lakini haziondoi ukweli kuwa wanawake wengi wamejiajiri kwenye kilimo hivyo ni sawa na kusema zaidi ya wanawake milioni 24 nchini wamejiajiri kwenye kilimo huku milioni 6 tu kati yao wakiwa kwenye sekta nyingine.

Tafsiri hapa ni nini?

Tafsiri ni kwamba mabadiliko yoyote hasi kwenye sekta kilimo yakisababishwa na vitu kama vile mafuriko na ukame yana athari ya moja kwa moja kwa wanawake na kwa uchumi kwa ujumla na hivyo kuhatarisha usalama wa taifa.

Ili kuona ni kwa kiasi gani kumuwezesha mwanamke kiuchumi ni sawa na kuimarisha usalama wa taifa ni vema kwanza tufahamu kwa ufupi dhana ya usalama wa taifa.

Dhana ya usalama wa taifa kwa miaka mingi ilikuwa ikitazamwa kwa mtazamo kiasili (traditional) na wa kidola (state-centric) unaotokana na mrengo wa kulia (realism) kwamba uwepo wa dola moja ni kitisho cha kiusalama kwa dola lingine na hivyo nchi kutamani zisizungukwe na nchi nyingine zozote pembeni yao (Rejea Wolfer, 1962; Buzan, 1991; Buzan na wenzake 1998; Nnoli, 2006 na Buzan na Stone, 2009).

Kwa hali hiyo nchi ilipaswa kujihakikishia kuendelea kuwepo state survival) kwa kulinda mipaka yake dhidi ya vitisho vyovyote kutoka nje (Rejea Nwozor na wenzake, 2019).

Ripoti ya Maendeleo ya Mwanadamu ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ya mwaka 1994 ilibadili dhana hii kwa kuanisha vitisho vipya vya kiusalama visivyo vya kiasili (non-traditional security threats) ikijumuisha umasikini, njaa na magonjwa (UNDP, 1994) kama tunavyoona sasa ugonjwa wa Covid 19 unavyozitesa nchi nyingi duniani.

Hivyo basi usalama wa taifa unahusisha moja kwa moja usalama wa binadamu, kwa maana nyingine usalama wa mwanadamu ndiyo kitovu cha usalama wa taifa kama walivyobainisha Nwozor na wenzake (2019) na Louw na Lubbe (2017).

Kwa tafsiri hii ya UNDP (1994) tunaona wazi kuwa changamoto zilizoainishwa katika risala ya wanawake iliyosomwa na mwakilishi wa wanawake bi Joyce Kashozi zikiwemo umasikini, umiliki mali na mitaji, kukosekana usawa katika vyombo vya maamuzi, njaa na maradhi ni changamoto za mwanadamu na kwa kuwa wanawake wapo wengi nchini basi changamoto hizi ni kitisho kwa usalama wa taifa letu na kwa hiyo juhudi za dhati zinahitajika kama alivyoainisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %