0 0
Read Time:3 Minute, 20 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Ijumaa tarehe 11 Juni, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amefanya mabadiliko madogo ya Wakuu wa Mikoa na kuteua viongozi wapya wengine kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sambamba na marekebisho yake mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Ndugu Jaffar Haniu ni kwamba katika mabadiliko hayo madogo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi amehamishiwa Mkoa wa Mwanza kuchukua nafasi ya Ndugu Albert Chalamila ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ndugu Ally Salum Hapi amehamishiwa Mkoa wa Mara kuchukua nafasi ya Mhandisi Robert Gabriel aliyehamishiwa Mwanza.

Mbali na mabadiliko hayo, Mheshimiwa Rais pia amemteua Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Batilda Salha Buriani kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora huku akimteua Ndugu Zuwena Omari Jiri ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kuchukua nafasi ya Balozi Batilda Buriani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 35.-(1) ni kwamba:

‘Shughuli zote za utendaji za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais.’

Lakini pia ibara ya 36.-(1) na (2) inaeleza wazi kwamba:

‘Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.’

‘(2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi unaofanywa na Rais.’

Kwa nini nimenukuu ibara hizi?

Ninakumbuka wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa akizungumza na wanawake wa Dodoma kwa niaba ya kina wanawake wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumanne tarehe 8 Juni, 2021 aligusia changamoto mojawapo ya kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika nafasi za maamuzi.

Kwa kuliona hilo Mheshimiwa Rais alieleza kuwa katika kipindi chake cha awamu ya Sita ya Uongozi ameanza kulifanyia kazi na kwa kuanzia aliteua majaji 28 kati yao majaji wanawake walikuwa 13 sawa na asilimia 45 ya uwiano wa jinsia.

Lakini pia Mheshimiwa Rais alisema kuwa katika ngazi ya uwakilishi wa Mikoa kwa maana ya Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS) na Wakuu wa Mikoa (RC) katika teuzi 26 alizofanya kuna wanawake 12 ambao ni sawa na asilimia 46.

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hilo eneo la uteuzi wa maRAS na maRC ndilo eneo ambalo amefanya vizuri sana kwa kuweka uwino wa kijinsia kwa mujibu wa Mkataba wa Kuondoa Aina Zote za Ukanyanyasaji na Ukandamizaji Dhidi ya Wanawake yaani CEDAW 1979, ule wa Beijing 1995, Itifaki ya Maputo ya mwaka 2003, Malengo ya Maendeleo Endelevu 17 (SDGs), sambamba na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.

Tukumbuke siku ile alipowaapisha alikuwa akiwasimamisha RC na RAS wake kwa kila Mkoa kuona uwiano wa jinsia ulivyo.

Hivyo basi binafsi ninaamini kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameona ipo haja ya kuweka uwiano kuwa walau 50 kwa 50 kwa kuwateua Balozi Batilda Buriani kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Ndugu Zuwena Omari Jiri kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga badala ya ile asilimia 46 kwa 54 ya awali katika eneo hili ambalo Mheshimiwa Rais ameeleza wazi kuwa amefanya vema katika kuzingatia uwiano wa jinsia.

Tukumbuke nchi za Afrika zilisaini Mikataba hii ya usawa wa jinsia lakini utekelezaji wake uliwa wa kusuasua kwa nchi nyingi, hivyo basi Mheshimiwa Rais anaendelea kutekeleza makubaliano mbalimbali ya Kimataifa, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, sambamba na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolenga kuleta usawa wa jinsia katika nafasi za maamuzi.

Asanteni.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter).

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %