0 0
Read Time:4 Minute, 47 Second

Na Abbas Mwalimu

+255719258484

Ijumaa tarehe 18 Juni, 2021.

Rais wa Kwanza wa Zambia na Baba wa Taifa hilo, Mzee Kenneth Kaunda amefariki Alhamisi tarehe 17 Juni, 2021 katika hospitali ya kijeshi ya Maina Soko iliyopo Mji Mkuu wa nchi hiyo, Lusaka.

Wakati huu Zambia, nchi za SADC na Waafrika kwa ujumla tukiwa katika maombolezo ya kifo cha Hayati Kaunda ni vema jamii ikatambua mchango wa Mzalendo huyu, jasiri na Mwanamajumui wa Afrika yaani Pan-Africanist aliyezaliwa Lubwa, Chinsali tarehe 28 Aprili, 1924 na kufariki akiwa na umri wa miaka 97.

Ni ukweli ulio wazi, popote pale unapozungumzia harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na hasa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuna viongozi watano kamwe hutoacha kuwataja; hawa ni Hayati Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Augustino Neto wa Angola, Sir Seretse Khama wa Botswana, Samora Machel wa Msumbiji na Hayati Kenneth Kaunda wa Zambia.

Hawa ndiyo walikuwa waanzilishi wa SADC tunayoijua sasa kutoka katika uliokuwa Muungano wa Nchi Zilizo Katika Mstari wa Mbele wa Mapambano kwa Kingereza Front Line States na kipekee kwa nchi ya Zambia Hayati Kaunda alikuwa na kariba na tajiriba zilizofanana na Hayati Nyerere kiasi kwamba hata Sera ya Mambo ya Nje ya Zambia kwa kiasi kikubwa enzi za Hayati Kaunda ilifanana na Sera ya Asili ya Mambo ya Nje ya Tanzania (Traditional Foreign Policy) iliyokuwa imetolewa Hayati Julius Nyerere kwa Waraka Namba 2 wa mwaka 1964.

Ili kuona mchango wa Hayati Kaunda maarufu kama KK katika ukombozi wa Afrika na hasa Kusini mwa Afrika basi tutazame kuanzishwa kwa SADC kwa mapana. SADC ilianzishwa kama Mkutano wa Uratibu wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (Southern Africa Development Coordination Conference-SADCC) mnamo tarehe 1 Aprili 1980 na nchi 9 za Tanzania, Zambia, Angola, Botswana, Msumbiji, Lesotho, Malawi, Zimbabwe na Swaziland sasa Eswatini ili kuondoa utegemezi wa kiuchumi na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini (ICG, 2012). Nafasi ya Hayati Kenneth Kaunda katika uanzishwaji wa SADC inajidhihirisha wazi.

Baadae SADCC ilibadilishwa kuwa SADC mnamo tarehe 17 Agosti 1992 mjini Windhoek, Namibia ambapo Mkataba wa SADC uliopitishwa mwaka 1993. Rejea ICG (2012 na Khadiagala (2018).

Miongoni mwa watu waliochangia kuibadili SADCC kuwa SADC ya sasa ni Hayati Kaunda licha ya kuwa mwaka 1992 alikuwa ameshatoka madarakani kumpisha Frederick Chiluba wa MMD baada ya kushinda uchaguzi wa Oktoba, 1991 dhidi ya chama cha Hayati Kaunda UNIP.

Katika kuonesha uzalendo kwa nchi yake, miongoni mwa maneno yatakayokumbukwa na Wazambia wengi ni kauli aliyotoa Hayati Kaunda baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 1991; Hayati Kaunda alisema baada ya matokeo ya uchaguzi ule: “My brother, you have won convincingly and I accept the people’s decision” akimwambia Rais Frederick Chiluba wakati ule kwamba ameshinda kihalali na yeye ameyakubali matokeo. Hapo ndipo tamati ya Hayati Kaunda katika uongozi wa Zambia uliisha baada ya kuiongoza nchi hiyo kupata Uhuru wake mwaka 1964.

Kama nilivyoeleza awali kuwa Zambia ikiwa chini ya Hayati Kenneth Kaunda ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa Jumuiya hii ya SADC tangu mwaka 1975 ikiwa imeanza kama Nchi zilizo Mstari wa Mbele (Front Line States) wakati huo Hayati Keneth Kaunda akiwa na Hayati Julius Kambarage Nyerere waliungana na Sir Seretse Khama wa Botswana, Samora Machel wa Msumbiji, Augustino Neto wa Angola sambamba na Ulesegun Obasanjo wa Nigeria ambaye aliguswa na vuguvugu la wanaukombozi hawa wa Afrika na kuamua kuungana nao kujenga Afrika moja.

Kabla ya hapo, historia ya SADC ilianzia mbali sana, tukumbuke mwaka pia 1958 kuliundwa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika kwa nchi za Mashariki na Kati mwa Afrika (PAFMECA) lakini kutokana na hitajio la kuzikomboa nchi za Kusini na hasa baada ya vyama kama SWAPO, MPLA na MNC kuhitaji kupata nguvu ya kupambana na ubaguzi na ukoloni Kusini sambamba na Ethiopia na Somalia, PAFMECA ilipanuliwa na kuitwa PAFMECSA mwaka 1962 lakini pia PAFMECSA ilivunjwa baada ya kuundwa kwa OAU mwaka 1963 (Rejea Cox, 1964: 2-3) pia rejea Cawthra, de Pisani na Omari (2007:50) katika Security and Democracy in Southern Africa. Kwa muktadha huu, unaachaje kuutambua mchango wa Hayati Kenneth Kaunda katika mapambano ya ukombozi wa Afrika na uanzishwaji wa SADC?

Baadae baada ya kuona kuna changamoto kadhaa katika OAU kufikia azma ya kuiunga Afrika, Hayati Kenneth Kaunda wa Zambia na Hayati Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania waliamua kuunda Jukwaa la Majadiliano kwa nchi za Kati na Kusini yaani Conference on East and Central African Countries (CECAC) ili kuziba pengo lililoachwa kutokana na kuvunjwa kwa PAFMECA (Cox, 1964:3 na Cawthra, de Pisani na Omari, 2007). Bado hatujautambua mchango wa Hayati Kenneth Kaunda?

Baadae yalikuja makubaliano ya Lusaka ya mwaka 1969 na Azimio la Mogadishu la mwaka 1971 lililoamua ulazima wa kutumia majeshi yenye silaha ili kuikomboa Afrika.

Lakini kabla ya Azimio la Mogadishu kulianzishwa pia Mulungushi Club mwaka 1970 iliyohusisha viongozi wa nchi za Tanzania, Zambia, Uganda na Zaire ya wakati ule (sasa DRC). Mulungushi Club ilikufa mwaka 1974 kufuatia kutoamiwa kwa tabia za Mobutu Ssesseko na hivyo kutoa mwanya wa kuanzishwa kwa Nchi zilizo katika Mstari wa Mbele (FLS) ili kupambana na wakoloni (Omari, 1991) na Cawthra, de Pisani na Omari (2007) na hatimaye ikaja SADCC na sasa SADC.

Kimsingi, Nchi zilizo Katika Mstari wa Mbele ama Front Line States ndizo zilizopelekea kuanzishwa kwa SADCC na baadae SADC. Nchi hizi na viongozi wake ni Hayati Julius Nyerere wa Tanzania, Hayati Kenneth Kaunda wa Zambia, Sir Seretse Khama wa Botswana, Augustino Neto wa Angola na Samora Machel wa Msumbiji. Hiyo mchango wa Hayati Kaunda katika Ukombozi wa Afrika na kuanzishwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) haumithiliki.

Huyu ndiyo Kenneth Kaunda; Nyerere wa Zambia, Kiungo wa SADC.

Pumzika kwa Amani Hayati Kenneth Kaunda.

Asanteni.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook & Instagram)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook na WhatsApp)

Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %