
KIONAMBALI
Salum Vuai
NI zaidi ya muongo mmoja sasa tangu hoteli ya Bwawani iache kutumika kwa mapokezi na malazi ya wageni mbalimbali wakiwemo watalii.
Inasikitisha kwamba hoteli hii iliyokuwa na hadhi ya pekee ikimilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, sasa imegeuka magofu yasiyotamanika hata kuwekwa kwenye kumbukumbu ya mambo ya kale kama inavyofanyika kwa majengo mengine ya kihistotria.
Nani asiyefahamu jinsi jina la ‘Bwawani Hotel’ lilivyokuwa mashuhuri kwa shughuli za utalii kote duniani, ambapo liliitangaza vyema Zanzibar na hakuna mgeni ambaye hakutamani kutia mguu na kulala humo, au japo kutembelea kwa kujipatia mlo wa siku na burudani nyengine tafauti.
Sura za bashasha walizokuwa nazo wafanyakazi, unadhifu wao na huduma nzuri ziliakisi ukarimu wa Wazanzibari mbele ya wageni waliokuwa wakipenda kutumia fedha zao katika hoteli hiyo kubwa kuwahi kujengwa na serikali.
Na katika kipindi cha awali kuelekea kufa kwake, serikali iliamua kuhamishia ofisi za baadhi ya taasisi zake ndani ya jengo hilo, na pia jumuiya na kampuni nyengine binafsi zilipewa vyumba kuendeshea shughuli zao humo, ingawa Kionambali haijui kama zilikodishwa au zilikirimiwa tu.
Hata hivyo hoteli ya Bwawani sasa imekuwa ‘Alfola imekufa, imebakia mafupa’, la kusikitisha zaidi ni kutoweka kwa mali zikizokuwemo ndani, kama vile samani, vyombo, ala za muziki vilivyotumiwa na kikundi cha taarab kilichoundwa na uongozi uliokuwepo, majiko, mashine za kufulia (Laundry) na za bekari zote zimefanywa ngawira.
Hata madirisha na milango ukiwemo mkubwa na mzito wa kuingilia hotelini hapo nayo haijulikani ilikopelekwa, labda Idara ya Uhakiki mali iliyopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango inaweza kuwa na majibu mazuri katika hili.
Kitu kimoja tunachoshindwa kukienzi ni nguvu kubwa za wananchi wa Zanzibar zilizotumika kujenga hoteli hii ambapo hata Rais wa kwanza wa visiwa hivi marehemu mzee Abeid Amani Karume alishiriki mara kadhaa kubeba tofali kwa mikono yake ili kuhamasisha uzalendo kwa wajenzi na vibarua waliokuwa wakijenga jengo hilo.
Tunaelewa juhudi zinazochukuliwa na serikali yetu kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuinusuru hoteli hii ingawa hakuna taarifa zinazotolewa kueleza zilipofikia na kinachoendelea kwa jumla japo mara kadhaa tumekuwa tukisikia majina ya watu maarufu yakitajwa kutaka kukabidhiwa.
Tuombe dua atokee mwekezaji atakaekuwa tayari kuifufua hoteli hii na kuwapatia vijana wetu ajira, na pia kuongeza pato la serikali kupitia kodi itakayokusanywa hapo.
Lakini wakati tukisubiri mwekezaji asiyejulikana atapatikana lini, Kionambali haipendezwi na mazingira yanayoizunguka hoteli hiyo kwa sasa, ambapo msitu mkubwa umeachwa kushamiri na kushusha hadhi ya jiji la Zanzibar kama linavyojulikana sasa.
Pori hilo halioneshi taswira nzuri inayohitajika pahala hapo, na Kionambali inaamini kuwa wahalifu wanaweza kulitumia kwa maficho wakivuta bangi na kutumia dawa za kulevya, au kujificha baada ya kutekeleza vitendo viovu ikiwemo kupora na kujeruhi watu.
Wakati wenzetu wanahifadhi mbuga za wanyama zinazotembelewa na watalii wanaoingiza kipato, kwa nini sisi tunatunza vichaka visivyokuwa na tija, tena eneo la mjini ambako katika hali ya kawaida kunatarajiwa kuwa nadhifu.
Hata sanamu la muasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar linalosimama nyuma ya hoteli hii limekosa matunzo huku likizungukwa na kichaka na ndege wa aina mbalimbali wakitua juu yake na kulichafua kwa kinyesi.
Aidha soko la samaki lililoanzishwa kando ya gofu hili, linaongeza maradufu uchafu wa mazingira kwenye eneo hilo unaotokana na uvundo wa matumbo ya samaki.
Ninapowaza juu ya hali hii, huwa ninajiuliza kuna faida gani kupeleka askari wa vikosi vya SMZ kulinda gofu tupu? Kama mali zilizokuwemo zimeshang’olewa na kugeuzwa ngawira hawa wanalinda nini?
Kwa Kionambali haya ni matumizi mabaya ya rasilimali watu, hivyo ni vyema nguvu ya walinzi hawa itumike kulifyeka pori hilo ili eneo liwe safi.
Kabla ya kutafuta mpangaji, kwanza tuhakikishe nyumba yetu tunaifuta mavumbi na kuondoa mabuibui, ili tutakapomfungulia mlango kumkaguza, asipate dosari ya kukimbia.