Aliyemuua Rais Museveni mitandaoni anaswa Uturuki
Zamzamnews29@gmail.com
Mwanablog aliyeshukiwa kwa kueneza taarifa kuwa Rais Yoweri Museveni alifariki kwa kuugua virusi vya corona, alikamatwa Uturuki wiki hii.
Maafisa wa usalama mnamo Jumanne walimkamata Fred Lumbuye ambaye mwandani wa Kiongozi wa Upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kwa kuhusika na kueneza habari hizo ambazo zilikuwa za uongo.
Pia inadaiwa alihusika na kutengeneza kisha kusambaza habari kuwa Mfalme wa Buganda Ronald Mutebi alikuwa amefariki dunia.
Maelezo kuhusu jinsi Lumbuye alivyokamatwa hata hivyo yalikinzana. Ripoti kutoka Uturuki ziliarifu alinyakwa alipokuwa akirejea katika makazi yake mnamo Jumanne jioni.
Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka Uturuki zilisema kwamba alikamatwa katika ubalozi wa Uganda alipoenda kurefusha muda wa kutumia pasipoti yake ya usafiri.
Serikali inadai kuwa Lumbuye ambaye ni mfuasi sugu wa Kyagulanyi alieneza habari za uongo ambazo ziliharibia Uganda sifa machoni mwa jamii ya kimataifa.
Anadaiwa kueneza habari hizo kabla na baada ya uchaguzi mkuu mapema mwaka huu.Mnamo Juni na Julai mwaka huu habari zilienea mitandaoni kuwa Rais Museveni alikuwa amefariki kutokana na virusi vya corona na jeshi lilikuwa likipanga kutwaa mamlaka hadi azikwe kisha uchaguzi mkuu mwingine uandaliwe.
Habari hizo zilienea wakati ambapo kiongozi huyo aliweka masharti makali ikiwepo kafyu na kufunga shule kama njia ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo hatari.
Habari hizo zilizoshabikiwa sana na viongozi wa upinzani, zilienea zaidi hata baada ya Rais Museveni kuonekana hadharani katika maeneo ya Munyonyo na Bombo akiwa ameandamana na Naibu Rais wa Kenya Wiliam Ruto wakizindua miradi ya maendeleo.
‘Tunatarajia kwamba atasafirishwa hapa nchini na kushtakiwa kwa kosa la kueneza habari za uongo zilizoharibia nchi sifa. Lazima awe tayari kupata adhabu kali kutokana matendo yake yasiyozingatia sheria,’ akasema Waziri wa Masuala ya Kigeni Okello Oryem jijini Kampala.
“Nilifikiria kama wanahabari mngefurahia kuwa amekamatwa ila ni wazi mnamwonea huruma. Yeye ni nani ashindwe kukabili mashtaka kwa kukosea taifa? Lazima aadhibiwe vikali,’ .
hivyo, chama cha upinzani NUP kimesema Uganda na Uturuki hazina mkataba wa maelewano unaoruhusu Lumbuye kusafirishwa hadi Uganda kushtakiwa.
Ikulu nayo inasisitiza lazima arejeshwe na kushtakiwa katika mahakama ya Uganda.