0 0
Read Time:4 Minute, 25 Second

Na: Zain Hamza
Washington DC

Muamba ngoma huvutia kwake!

Uraia pacha ulianzishwa ili kuvutia watu wahamie kwenye nchi za ulimwengu mpya (New World). Wahamiaji hao waliona umuhimu wa kulinda haki zao za kiraia kwa nchi zao za asili. Hapo ndipo likatokea wazo la uraia pacha. Canada pamoja na kuwa na eneo la karibu mara kumi ya Tanzania, ni nchi yenye watu wachache kuliko Tanzania. Uraia pacha ni suala lenye matatizo mengi kwa serikali nyingi duniani. Baadhi ya matatizo hayo ni ukwepaji wa kodi, uhusiano wa kimataifa, kuyumbishwa kwa serikali na hata kufungwa jela kwa wenye uraia pacha.

Kwa Tanzania hasara ya jumla ya uraia pacha ni kuchukuliwa kwa maliasili za Tanzania na wageni. Kenya ambayo ni kigezo kikubwa cha uraia pacha, wana tatizo kubwa sana la ardhi. Wamiliki wakuu 13 wa ardhi nchini Kenya ni wazungu. Ardhi ni bidhaa ghali mno na wenyeji wengi hawana ardhi hata za kuzikana. Kiwanja kidogo cha kujenga nyumba ya kawaida Kisumu ni dola elfu 35. Zaidi ya milioni 80 za kitanzania. Hiyo ni Kisumu, sio Mombasa au Nairobi. Fikiria meli za wazungu wenye uraia wa Tanzania zije kuvua samaki kwenye maji ya Tanzania. Pata picha wamiliki wa migodi kama Acacia wawe na uraia wa Tanzania. Nchi italiwa na wageni mchana kweupe kabisa.

Kuna hasara za rejareja pia zikiwemo zifuatazo;

1. Ongezeko la wageni nchini; uraia pacha hufungua milango sio kwa wazawa wa Tanzania tu, bali hata kwa watu wa mataifa yote duniani. Si Tanzania wala nchi nyingine yeyote ya afrika yenye haja ya kuongeza idadi ya watu wake kwa kualika raia wa kigeni kama ilivyokuwa kwa nchi za bara la Amerika.

2. Ukwepaji wa kodi; watu wenye uraia pacha wataweka pesa zao kwenye mabenki ya kwao ambako wana uraia wa kuzaliwa. TRA itashindwa kuzitoza kodi pesa hizo. Kuepuka tatizo hili Marekani imetunga sheria maalumu inayoitwa Foreign Account Transaction Compliance Act (FATCA) Ni sheria inayopiga marufuku Marekani kufanya biashara na benki zote za nje zinazozuia idara ya kodi ya Marekani IRS isifikie akaunti za raia wa Marekani waliopo nje ya Marekani. Ni changamoto hiyo kwa serikali ya Tanzania ipate utaratibu kama huo.

3. Kupungua kwa wawekezaji; wengi wa wawekezaji wataona ni nafuu kwao wachukue uraia pacha Tanzania ili waepuke kulipa kodi za uwekezaji na kugawana mapato au faida na serikali ya Tanzania.

4. Usalama na uhalifu wa kimataifa; wahalifu na wakimbizi watasepa kirahisi wakiwa na uraia pacha. Bila ya kusahau wahujumu uchumi na watakatishaji fedha. Badala ya kukimbilia Ulaya na Marekani ambako kuna utaratibu mrefu wa kukubaliwa na wa wazi, wahalifu na wakimbizi wenye uraia pacha itawatosha hata kukimbilia Burundi.

5. Uzalendo wa raia; Wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya kiafrika pamoja na kushinda kombe la dunia wamewahi kushutumiwa na kiongozi mmoja wa nchi hiyo kuwa hawawezi hata kuimba mwimbo wa taifa wa Ufaransa. Karim Benzima amewahi kulalamika kuwa akifunga goli anaitwa mfaransa, akikosa goli anaitwa muarabu. Kama ambavyo watanzania wanachukua uraia wa nje kwa maslahi, basi watakuwepo na raia wa nje watakaochukua uraia Tanzania kwa maslahi.

6. Athari za mila na utamaduni; wageni hasa watakaohamia kwa wingi kama walivyo waspanish nchini Marekani watayumbisha utamaduni wa Tanzania. Moja ya sababu za Marekani kuwa nchi ya ajabu kimaadili ni mkusanyiko wa watu wa aina zote duniani ndani ya nchi.

7. Kudhoofika kwa lugha ya kiswahili; raia wa nje wakihamia kwa wingi Tanzania lugha ya kiswahili haitatosha. Itahitajika lugha ya kimataifa kama kiingereza.

8. Ajira kuchukuliwa na wageni; hili halina mjadala sana. Raia wa kigeni watakaohamia Tanzania ni lazima watanyang’anyana ajira na wazawa. Na watakuwa na kipaumbele hasa kwenye zile ajira zinazohitaji kingereza. Tanzania tayari ina tatizo la ajira kwa watanzania.

9. Udhibiti wa utoaji uraia; kuna wageni watakaotumia rushwa,wizi, na kughushi nyaraka za serikali ili wapate uraia wa Tanzania. Hasa ukizingatia upatikanaji wa uraia wa Tanzania unachukua miaka kadhaa. Kuna watakaokaa Kariakoo siku kadhaa na kujipatia uraia pacha Tanzania. Kwenye hili ni makosa kuiga nchi zilizoendelea ambako taratibu zinafuatwa kikamilifu na hakuna mianya ya kutoa rushwa mambo yaende haraka au kinyume cha sheria.

10. Kupoteza muelekeo wa kuwasaidia wanadiaspora; wakati Hadhi maalumu italazimisha kila mwenye kuipata ahisabiwe na serikali ya Tanzania, hakuna kompyuta duniani inayoweka takwimu za wenye uraia pacha. Watakaofikiwa na serikali ni wale tu watakaojitolea kwa hiari yao wahesabiwe wao pamoja na familia zao. Ni kazi ngumu na haijawahi hata kujaribiwa.

11. Kupoteza wateja wa utalii; raia pacha wa Tanzania hasa kutoka nchi za jirani wanaweza kuwa na kampuni za utalii, wakaajiri watu wa kwao kwenye hifadhi za wanyama Tanzania, wakaalika hata na watalii kwa faida yao na ya nchi za kwao.

12. Wanadiaspora kuzidiwa kete na wageni; ingawaje lengo ni kuwasaidia wanadiaspora wa Tanzania, uraia pacha utawapambanisha na watu wa mataifa mengine ya dunia katika kuwekeza na kupata haki za uraia wa Tanzania.

13. Migogoro ya kimataifa; chukulia mwizi kaiba matrilioni ya pesa Tanzania, akaua watu Kenya halafu akakimbilia Afrika ya Kusini. Ana uraia wa Tanzania na Kenya. Serikali zote mbili zinamtaka, Afrika ya kusini itamrudisha wapi.

Matatizo hayo yote yanajibiwa na maneno mawili tu, HADHI MAALUMU. Kwa kifupi serikali ya Tanzania itagomea uraia pacha lakini itawakumbatia wazawa wake ambao wamechukua uraia nchi za nje. Kwa maana nyingine Tanzania itavuna kutoka kwa wanadiaspora wake na itajilinda isivunwe na diaspora (wageni) kutoka nchi za nje. Ni utaratibu unaotumika hata na baadhi ya nchi zinazoruhusu uraia wa pacha wa masharti Uholanzi ikiwa ni mojawapo ya nchi hizo.

Happy
Happy
25 %
Sad
Sad
25 %
Excited
Excited
25 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
25 %