
“Magufuli katutenda deni la taifa, trilioni 78 Samia msalabani”
Jamhuri October 26, 2021
Na Deodatus Balile
MAJIBU
Na Clifford Lugabeiya Mushendwa
Muleba, Kagera.
Hivi punde nimemaliza kusoma Makala ya uchambuzi ya SITANII kwenye gazeti la Jamhuri la Oktoba 26, lenye kichwa cha habari-Magufuli katutenda deni la Taifa, trilioni 78 Samia msalabani, na mwandishi Deodatus Balile.
Makala hiyo yenye kichwa cha habari chenye mvuto fulani,huku ikisheheni ushahidi wa takwimu na maoni binafsi ya mhusika ambaye ni dhahiri sasa kwamba hana ubobezi kwenye elimu ya Uchumi, ndiyo hasa imesababisha nishawishike kuandika ukweli halisi wa deni la taifa halisi na siyo vinginevyo.
Kwa vile lilivyo, andiko lile linamtambulisha Balile kwamba ni mchanga mno kwenye fani yake labda ndiyo maana limejaa bashasha hata wakati mwinhine likivuka mipaka ya waziwazi kwamba eti yeye ndiye aliyesababisha ifuatwe Katiba ili Rais Samia aapishwe, kana kwamba watanzania wote ikiwemo wizara inayosimamia sheria na Katiba hawakuweza kutejekeza jukumu hilo.
Kiufupi ni makala inayoupotisha umma kwa hoja dhaifu ambazo kimsingi hazikamilishi uhalali wa kubeza na kukitia kitanzi kivuli cha hayati Magufuli.
Labda kiini cha makala hiyo kilikuwa ni kupuliza parapanda kwa watanzania kwamba katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020, nchi yetu iliingia kwenye mkumbo wa kukopa madeni bila mpango, hali iliyosababisha kuongezeka kwa deni la taifa kufikia trilioni 78, huku kila mtanzania akidaiwa shilingi milioni moja na laki tatu.
Makala hiyo yenye mbwembwe imeonyesha kwamba katika kipindi hicho, serikali ya awamu ya tano ilikopa kiasi kikubwa cha fedha, zaidi ya fedha zilizokopwa kwenye kipindi chote cha awamu ya nne ama fedha zilizokopwa awamu ya tatu.
Mwandishi huyu aliendelea kudai kwamba, huu ulikuwa ukopaji usio na mpango, kwani umejenga mabarabara, madaraja, bwawa la umeme, treni ya umeme na mengine mengi ambayo, kwa maono yake, hayana maana kwenye uchumi wa Tanzania.
Nikaendelea kumsoma namna ambavyo mwandishi Balile aliweka hesabu zake, ili kuthibitisha hoja yake, na kweli alifanikiwa, kwani deni la taifa ni Trilioni 78.
Akasema, kwa hali hiyo, mzigo huu anaubeba Rais Samia Suluhu Hassan, huku akijua kwamba kwa miaka yote mitano alikuwa Makamu wa Rais, kwani mikopo mingi ni ya kibiashara na inalipwa kwa muda mfupi.
Mwandishi huyu Balile hakuishia hapo, aliuponda utaratibu wa kukopa kibiashara, akiuona kwamba ni hatari, kwani uwezo wetu wa kulipa ni mdogo, kwa hiyo tunajitafutia matatizo.
Nikiangalia ripoti za Kuu www.bot.go.tz madeni ya nje hadi kufikia Agost 2021 lilikuwa USD29.5 bilioni kutoka USD23.4 billion Agost 2020 hizi ni takwimu mpya, kiwemo alizotumia Mwandishi huyu wa Jamhuri.
Kati ya deni hilo mikopo ya bei nafuu ni USD11.1 bilioni toka kwa mashirika ya kimataifa, USD2.2 billion toka nchi na taasisi moja moja na USD9 bilioni ni ya kibiashara na USD2.5 bilioni ni mikopo ya mauzo ya bidhaa za nje (export Credit).
Kwa msingi huo, mikopo ya biashara ni asilimia 34.8 ya mikopo yote ya nje huku mashirika makubwa ya kimataifa yakiwa na asilimia 45.5 ya mikopo yote.
Nikashangaa sijui ni kwanini yeye aliamua kumbebesha zigo hili Rais Samia? Je alikuwa tu anataka kumfurahisha Mheshimiwa Raisi au aliandika kwa dhumuni maalum ambalo analijua yeye mwenyewe toka rohoni mwake kwa malengo yake binafsi ama ya kisiasa?
Ikumbukwe kwamba, kila nchi inakopa, na kukopa sio dhambi na kwa miaka yote miradi yetu ya maendeleo inajengwa kwa fedha za mikopo ya muda mfupi na mrefu.
Nimkumbushe kwamba, pamoja na kuwa na mikopo ya kibiashara ya nje, hata ndani serikali inakopa kibiashara toka kwenye benki zetu, ikiwemo moja moja kwa njia ya masoko ya fedha ama muungano wa benki kama ilivyowahi kufanya awamu ya JK ilipokabidhi jukumu hilo kwa Stanbic/ Standard Bank na washirika wake.Rejea kesi ya uhujumu uchumi ya Kitilya na wenzake.
Kwahiyo, nchi yoyote inayoendelea ikiwemo Tanzania, mkopo ni kitu muhimu sana ukizingatiwa kuwa rasilimali za kutengeneza mapato ndivyo zinavyoendelezwa.
Kwanza, ukiangalia kwenye tovuti za benki ya dunia www.worldbank.org/dsa na www.imf.org kwenye debt sustainability assessment zinaonyesha kwamba deni letu la nje bado ni asilimia chini ya 40 ya pato la taifa.
Nchi kama Japan Marekani, Msumbiji, Nigeria nk wao deni la mataifa yao tayari limeshapita asilimia 100 ya pato lao la taifa, na bado hatujawasikia wakitangaza hali ya hatari.
Sina haja ya kuweka takwimu hapa,lakini ukiwa na muda tafuta mwenyewe kwenye tovuti hizo hapo.
Nchi zinazoongoza kwa madeni makubwa duniani wa asilimia ya pato la taifa hadi mwaka jana nni Italy (156), Ureno (146), Ubeligiji (128), Marekani (127), UK (119), Canada (114), Ufaransa (123).
Tanzania ni nchi ya kumi kwa ukubwa wa madeni Afrika kwa miaka mingi. Nchi zenye madeni makubwa Afrika tukianza na ya kwanza ni hizi;Afrika Kusini, Nigeria, Angola, Kenya,Ethiopia, Zambia, Ghana, Sudan na Msumbiji na asilimia 21 ya fedha zilizokopwa zikitolewa na Uchina.Kwa ushahidi zaidi wa kitakwimu tembelea www.statista.com/statistics.
Takwimu nyingine toka www.tradingeconomics.com/country-list/go/governmentdebt ineonyesha kwamba mikopo ya Tanzania ni asilimia 37.8 ya pato la taifa huku nchi kama Sudani ikiwa na asilimia 259, Congo asilimia 102, Sao Tome asilimia 103, Tunisia asilimia 87.6, Uganda asilimia 49.8, Rwanda asilimia 61, Sierra Leone asilimia 71.9 Zambia asilimia 96, Zimbabwe asilimia 77.2 nk nk.Je hapo bado hatuko vizuri?.
Mpaka hapa ninaona mwangwi wa propaganda zisizopendeza kwenye hoja za mwandishi Balile.
Nikinukuu ripoti ya IMF iliyotolewa mwaka huu na www.imf.org ilisema. (The findings of the Debt Sustainability Analysis (DSA) showed that Tanzania’s public debt dynamics are stable, with the country’s risk of external debt distress remaining low.
All debt burden indicators are projected to stabilise at levels consistent with low rollover risk under both the baseline and stressed scenarios.
A draft DSA report, which summarised key findings and recommendations for consideration by senior officials, was produced. Government is expected to use the DSA findings to inform budget formulation for the fiscal year 2021/22 and determine the amount of borrowing that is consistent with medium-term debt sustainability and macroeconomic stability.)
Nashindwa kuelewa tangu lini ndugu yetu Balile alianza kuwa shujaa wa kusambaza propaganda za ajabu namna hii?
Pili, ukiangalia deni letu la taifa liko katika kiwango kizuri sana ikilinganishwa na mauzo yetu ya nje.
Tukumbuke kwamba dhahabu tu inaingiza shilingi trilioni 8 kwa mwaka, bado kuna mazao, madini mengine, bidhaa za viwandani, ambavyo mapato yake yanazalisha kodi ambayo ndiyo inatumika kulipia haya madeni.Mauzo ya nje yanapoongezeka, basi inakuwa rahisi sana kurejesha mkopo.
Tatu, mbali na kuangalia hayo, pia mwandishi wa Jamhuri hakukumbuka kwamba hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wa 2020/2021 kodi kwa mwezi zilifikia trilioni 1.4, hiki ni kiwango kikubwa, na ukuaji wa kodi ndio hamasha ya kuendelea kukopa.
Mbali na sababu hizo, mwandishi Balile pia alishindwa kujua kwamba ile dola milioni moja tuliyokopa mwaka 2000 wakati dola ikiwa 1,000 ilikuwa bilioni moja, lakini hiyo hiyo dola milioni moja kwa leo ni shilingi bilioni mbili na ushee- fedha yetu imedorora mara mbili.
Kwa hiyo usione ule mkopo wa bilioni moja mwaka 2000 ukadhani ni ileile trilioni moja, la hasha, hiyo ni trilioni 2.3 kwa leo hii mwaka 2021.
Bado Balile kwenye andiko lake amekosa uelewa kwamba, mahitaji ya nchi yameongezeka kwa kiwango kikubwa, bajeti la leo ya barabara sio ile ya mwaka 1997 na mshahara wa leo wa mfanyakazi sio ule wa mwaka 1999, mambo yamebadilika na idadi ya watumishi wa serikali wameongezeka mno.
Namkumbusha tu mwandishi Balile kwamba kuwa na deni la taifa sio kigezo cha uchumi kudorora, bali ni ishara ya maendeleo ya kiuchumi kwani matokeo ya madeni hayo tumeyaona, na Rais Samia aliyasimamia akiwa Makamu wa Rais.
Kinsingi huwezi kabisa kumtenganisha Samia na Hayati Magufuli kwa kudai kwamba huyu amembebesha mwingine k, hawa wote walikuwa pamoja na wataendelea kuwa pamoja, kwani anayotekeleza Rais Samia ndiyo waliyopanga na mtangulizi wake kwa ajili ya awamu hii ambayo anaisimamia yeye kwa kuimalizia.
Lakini pia,kuna mahali Mwandoshi amejikwaa kidogo kwa kulipaka tope Baraza la Mawaziri ambalo ndipo hupitisha mikopo na madeni ya taifa,ambalo amewaita ni wapambe wa Rais.
Huko ni kulikosea adabu Baraza hilo kwani waliokuwemo humo bado wako hata sasa na wengine ni wako kwenye nafasi kuwa katika serikali hii kuliko walivyokuwa wakati huo na kimsingi wanapaswa kupewa heshima siku zote kama viongozi.

Na Clifford Lugabeiya Mushendwa
Muleba, Kagera.








