Na Abbas Mwalimu
Ijumaa tarehe 4 Machi, 2022.
Jumatano tarehe 2 Machi, 2022 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio kulaani utumiaji nguvu wa Russia dhidi ya Ukraine.
Azimio hilo namba A/ES-11/L.1 lilinukuu Ibara ya Pili (Article 2) para 4 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1945 unaokataza utumikaji wa nguvu dhidi ya Nchi huru au eneo lolote kinyume na Mkataba huo.
Aidha, Azimio hilo lililopitishwa na wanachama 141 dhidi ya watano huku nchi 35 zikijiuzuia kupiga kura lilinukuu pia Azimio 2623 (2022) la Baraza la Usalama la tarehe 27 Februari, 2022 lililoomba kikao cha dharura na Azimio namba 377 A (V) la Baraza Kuu la tarehe 3 Novemba, 1950 lililoelekeza kuungana kwa amani.
Vilevile Azimio hilo ambalo Tanzania ilijizuia kulipigia kura lilinukuu Azimio 2625 (XXV) la tarehe 24 Oktoba, 1970 na Azimio 3314 (XXIX) la tarehe 14 Disemba, 1974 na Mkataba wa Ushirikiano wa Kiusalama wa Helsinki wa tarehe 1 Agosti, 1975.
Kumekuwa na mijadala mingi sana mitandaoni juu ya sababu za Tanzania ‘kukataa’ au kwa lugha ya kitaalamu “kujizuia” kulipigia kura Azimio hilo.
Makala hii inajaribu kueleza sababu ambazo nchi mbalimbali duniani hujizuia kupiga kura kwenye baadhi ya maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa au hata ya Baraza la Usalama la umoja huo.
Kabla sijaeleza kwa kina juu ya sababu kadhaa zinazosababisha nchi duniani kujizuia kupiga kura (Abstention) ni vema kutambua kwanza kuwa kujizuia kutopiga kura si sawa na kutohudhuria Mkutano (Abstention is not Absenteeism).
Sababu za Nchi Kujizuia Kupiga Kura
Katika kufafanua sababu ambazo baadae nitaziweka bayana makala hii inatumia nadharia mbili, mosi ile ya Kenneth Arrow (Social Choice Theory) na Duncan Black (Committee and Elections Theory) kwa kuziunga pamoja na pili ile ya Anthony Downs (An Economic Theory of Democracy).
Kwa ujumla wake Arrow na Black wanatanabaisha kwamba mtu/nchi hufanya uamuzi wa kupiga kura, kutopiga au kujizuia kupiga kura kwa kuzingatia muunganiko wa mahitaji yake kijamii.
Mahitaji haya huunda jedwali la mahitaji ya mtu/nchi husika na utofauti wa mahitaji hayo dhidi ya wengine na hivyo kutengeneza mtiririko wa kimahesabu wa mtu au nchi kufanya maamuzi katika suala la kijamii. Tunaelewana?
Nadharia ya pili ni ile ya Anthony Downs inayojulikana kama An Economic Theory of Democracy.
Nadharia hii inawakilishwa na kanuni ifuatayo, R=PB-C ambapo:
R inasimama badala ya Matumizi/Faida ya kile ambacho mtu/nchi itakipata kutokana na kupiga kura, kutopiga kura, au kujizuia kupiga kura.
P inasimama badala ya Uwezekano wa Kura ya mtu/Nchi kuwa na Uamuzi katika jambo.
B inasimama badala ya faida itokanayo na kupiga kura, kupinga au kujizuia kupiga kura na,
C inasimama badala ya Gharama za kura ama athari za kura hiyo kwa mtu au Nchi.
Endapo R italeta jawabu chanya basi mtu au nchi itapiga kura kupitisha Azimio lakini ikiwa R italeta jawabu hasi hapo mtu au Nchi huamua kujizuia kupiga kura.
Kwa msingi huo Downs anabainisha namna ambavyo mtu/nchi hupiga kura kwa kuzingatia faida na hasara ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na kufanya uamuzi fulani kama huo wa kupiga kura.
Kwa namna jambo la Urusi lilivyokuwa limesimamiwa kidete na nchi za Magharibi ilionekana wazi kura zitaelekea wapi kwa mantiki hiyo hata kama Tanzania ingepiga kura kura yake isingekuwa na ujazo wowote katika uamuzi ambao tayari ulikuwa unaonekana dhahiri ulishafikiwa hata kabla ya kupigwa kura hivyo kujizuia kupiga kura kuna faida kwa Tanzania.
Hili lilibainishwa pia na Hayden (2010:594) katika andiko lake ‘Abstention: The Unexpected Power of Withholding Your Vote’ alipobainisha kuwa kujizuia kuna madhara tu endapo kundi la wapiga kura ni dogo.
Sasa fikiria katika kura zaidi ya 140 kura ya kati ya wanachama 193 wa umoja huo, kura ya Tanzania ingekuwa na madhara gani wakati ilitakiwa theluthi mbili ya kura kwa mujibu wa kanuni ya 83 ya Kanuni za Mwenendo za Vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa?
Kwa kifupi ni kwamba, kama nchi moja inaweza kufikia malengo yake kwa kupiga kura basi nchi nyengine nayo inaweza kufikia malengo yake kwa kutopiga kura/kujizuia kupiga kura kutokana na mahesabu ya kila nchi.
Lakini pia mzozo wa Urusi na Ukraine umechukua sura tofauti na migogoro mingine kama ule wa Palestine ambao watoto, kina mama na wazee wanauawa kila iitwapo leo lakini Umoja wa Mataifa haujawahi kuchukua hatua ya kuitisha kikao cha dharura kama hiki.
Kimsingi, mgogoro huu una sura ya Vita Baridi ambapo Nchi zimegawanyika kiitikadi baina ya Magharibi na Mashariki hivyo kwa Tanzania kujizuia kupiga kura (Abstaining) kunaifanya itekekeze Sera ya Kutofungama na Upande Wowote (NAM) kiurahisi zaidi kwa sababu mazingira yanajionesha wazi ni ya Vita Baridi (Cold War).
Sambamba na hayo, kikao hiki cha dharura (Emergency Session) kinafanyika baada ya miaka 40 kupita baada ya kile cha mwaka 1982 kujadili mzozo wa Israel na Syria hivyo ni kama kipya kwa kuzingatia wakati na mahitaji ya vipindi, kwa msingi huo Nchi huhitaji kujiridhisha kwa kina ili zifanye maamuzi sahihi.
Hivyo kama wakati wa kujiridhisha ni mfupi nchi huamua kujizuia kupiga kura ili isifanye maamuzi ya mhemko.
Kwa mantiki hiyo kuna sababu kadhaa ambazo husababisha nchi kujizuia kupiga kura zikiwemo:
Mosi, nchi kuona kwamba haina taarifa za kutosha kuhusiana na jambo lililopo ambazo zingeiwezesha kufanya maamuzi kutokana na taarifa sahihi zilizopatikana.
Pili, nchi ikiwa inaamini kuwa kupiga kura katika jambo hilo kutaleta mgongano wa maslahi katika utekelezaji wa Sera.
Kwa Tanzania kwa mfano, huenda athari hizo zingeweza kujitokeza kwenye Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote (Non Alignment Policy).
Tatu, nchi huweza kujizuia kupiga kwa kupinga hatua husika kuchukuliwa kabla ya mashauriano ya kina kufanyika kama alivyolalamika Zhang Jun, Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa.
Lakini kuna wakati kutopiga kura huweza kuchukuliwa kama kuwasha taa ya kijani kwa wale wanaopitisha ama kupinga jambo husika kama alivyobainisha Hayden (2010: 603-604) na hapa ninamnukuu; “In many situations, abstaining is the equivalent to casting a vote weighted in favor of one of the alternatives.”
Hali hiyo Hyden huiita ‘No-Show Paradox’ akibainisha kwa Kingereza kwamba; ‘in some situations, people can make their favored outcome more likely by withholding their votes.’
Hayden anabainisha kuwa kuna wakati watu/nchi hufanya maamuzi ya kutotaka kuonesha uhalisia wa maamuzi yao hivyo huamua kutopiga lakini kutopiga kule huwa na tafsiri ya kuunga mkono upande fulani.
Hapa sasa tunaweza kujiuliza je nchi zote 35 zilizojizuia kupiga kura ni Non-Aligned kama Tanzania?
Wenu:
Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).
+255 719 258 484
Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).








