
WU®Media PRODUCTION
Ni kupitia ndege zake, abiria Milioni 90.2 kutazama
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ambapo vitaweza kuonwa na abiria wapatao milioni 90.2 wanaosafiri kila mwaka kupitia ndege za shirika hilo.
Aidha, tangazo la vivutio vya utalii vya Tanzania litakuwa likitazamwa na mamilioni ya abiria wa Shirika hilo wakati ndege zitakapokuwa zikiruka (take off) katika viwanja mbalimbali duniani.
Waziri Ndumbaro amebainisha hayo Dubai alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirika hilo ambalo mbali na kusafirisha abiria milioni 90.2 duniani kote pia husafirisha abiria wapatao milioni 20 ambao huunganisha ndege nyingine.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana ziandaliwe makala tano (Documentaries ) za kuelezea vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Zanzibar, Serengeti, Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro.
” Shirila la ndege la Emirates ni Shirika kubwa sana Duniani lengo letu kama nchi ni kuhakikisha abiria wapatao milioni 90.2 wanaviangalia vivutio vyetu kisha wanavipenda halafu wanatembelea Tanzania” amesisitiza Dkt.Ndumbaro
Ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo uongozi wa ndege hizo umeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania kutangaza utalii na ifikapo mwanzoni mwa mwezi wa Mei mwaka huu wataingia makubaliano (MOU) baina ya Tanzania na Shirika hilo
Dkt.Ndumbaro amesema kati ya abiria watakaoangalia vivutio hivyo watavutiwa na hatimaye sehemu ya watu hao waweze kuja kutembelea Tanzania
” Shabaha yetu kubwa kama nchi ni kuhakikisha tunafikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, Tunaamini tutalifikia lengo hilo” amesisitiza Dkt.Ndumbaro
Amesema Tanzania inategemea utalii wake wa Wanyamapori kwa asilimia 100 hivyo kupitia mkakati wa kutangaza vivutio vingine vya utalii kama vile utalii wa fukwe, utalii wa utamaduni pamoja na utalii wa ikolojia itawezesha utalii huo kujulikana dunia kote.