
WU® MediaPRODUCTION LIMITED
WAZIRI wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ameibuka na kuzungumzia sakata la tozo za benki na miamala ya simu, akikosoa njia zinazotumika katika utozaji wake.
Kitwanga, aliyekuwa Mbunge wa Misungwi kabla ya kuangushwa ndani ya chama katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020, alikosoa kuhusu tozo hizo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
Mfanyakazi huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alimshauri Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, kuachana na masula ya tozo hizo zilizoibua malalamiko na ukosoaji mwingi.
“Jana (juzi), nilimsikiliza kwa makini sana Waziri wetu wa Fedha (Dk. Mwigulu). Tukienda kwenye msingi wa hili, tukianza na walivyosema wananchi wengi washiriki kuchangia, hapa hayuko sahihi.
“Ukianzia kwenye masuala ya kutuma fedha kwenye mitandao, M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na kadhalika, wenye uwezo wa kufanya hivyo tayari ni walipakodi.
“Kwa maana kama mtu anatuma fedha, atakuwa anamtumia ndugu yake, mzazi, ni mfanyakazi au ni mfanyabiashara ambaye ni mkubwa ambaye huwa analipa kodi, lakini mtu wa kawaida kijijini ambaye hana kazi, hawezi kumtumia mtu hivi hivi.
“Tuelewe kwamba wanaoweka (fedha) benki ambako na kwenye fedha zinatozwa tozo ni watu wenye uwezo. Mfanyabiashara, mfanyakazi anaweka fedha benki na huyu anafanya hivyo kwa sababu serikali inamlipa kupitia benki, kwa hiyo analazimika kufungua akaunti.
“Kwa hiyo, fedha zake zinapotoka kwenye mshahara, zinaingia kwenye akaunti yake. Na hata akizichukua zote, bado atatozwa tozo. Lakini hawa tayari fedha zao zimeshatozwa kodi. Sasa unapokuja unazitoza tena tozo, wanaita ‘double taxation’ (kulipisha kodi mara mbili), ni uvunjaji wa sheria,” alifafanua.
Kitwanda, alisema kauli ya Waziri Mwigulu kwamba kutoza tozo hizo ni kupanua wigo wa watu kulipa kodi, haina uhalisia.
“Sasa tunaposema tunapanua wigo wa watu, hatuko sahihi. Tuangalie kwamba ile ‘base’ (chimbuko) ya walipakodi ambao wana namba ya TIN (namba ya mlipakodi) ni wangapi.
“Logic ya waziri au mafikirio yake ya jinsi ya kuangalia ni mbaya, kwa sababu sasa una tozo kwenye ATM, kwenye akaunti yako unapochukua fedha, kwenye M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na kwingineko, yaani kila transaction (mwamala), unayofanya inapigwa kodi, ina maana sasa transactions (miamala) zako za kibenki zinakuwa ghali.
“Badala ya kupunguza ili kupanua hiyo tunayoita financial inclusion, sisi tunakimbiza tunaifinya hiyo, sasa sijui ni uchumi wa wapi huo!” Kitwanga alisema.
Kitwanga, alishauri kuachana na tozo hizo zote na kutafuta njia nyingine za mapato, akitamka: “Mimi ushauri wangu tuachane na hizi tozo zote, tukae na hawa watu wa mitandao ya simu, halafu tuwaulize wanatoza kiasi gani kwa dakika, tuongeze Sh. 60 tu kwenye kila dakika mtu anayopiga, ina maana utakuwa na walipakodi milioni 29, tuwaze kipana, tuwaze mbali, tusiwatese wale wanaolipa kodi.
“Sasa hivi huwezi kuniambia kila mtu analipa kodi, eti umepanua wigo, wigo uko wapi? Anayetuma fedha ni huyo huyo, amezitoa benki ni huyo huyo na anayelipwa mshahara huo huo,” alifafanua na kumkaribisha Waziri Mwigulu kumpa ushauri zaidi wa kiuchumi.
“Ninawashauri waje hapa nitawaeleza, nitawapa ‘facts, I have data’ (ninazo takwimu). Sizungumzi kwa kubahatisha. Kwa mfano, Waziri Mkuu wa kwanza wa Singapole, alikuwa anazungumzia namna walivyoinua uchumi wao, nao walikuwa kama sisi, lakini wako katika top ten (kumi bora) kiuchumi duniani. Tuwaze kwa upana, nchi yetu hii ina watu wengi wenye uwezo sana wa kufikiri, serikali iwatumie, siyo lazima mimi.
“Mimi nimefanya kazi Benki Kuu ya Tanzania miaka 23, kuna PhD nyingi tu. Ni vizuri tukawaza kwamba nchi yetu inahitaji kuendelea, hatuwezi kutegemea tozo, maliasili tulizonazo nyingi namna hiyo, haiwezekani aise!
“Kuna vyanzo vingi mno vya mapato ambavyo hatutaki kuhangaika, tunakwenda kutafuta njia rahisi kupata kodi au tozo . Lakini tunapokwenda huko kwenye njia rahisi, we are killing our economy (tunauua uchumi wetu).
“Transaction na financial transaction ni base ya shughuli ya biashara, sasa kama unaishindilia ‘tax’ (kodi) itakuwaje? Ile ndiyo inayosababisha biashara ifanyike na biashara ikifanyika ndipo unatakiwa utoze tozo na kodi, sasa wewe unatoza kwenye chanzo, biashara itapatikanaje?
“Acha huku usitoze, ‘stimulate’ kuwe na ‘big financial’ na ‘transactions’ nyingi ambazo zitasaidia watu wazalishe na wakizalisha, toza huko, kwenye matokeo badala ya kutoza kwenye matokeo, unatoza kwenye chanzo cha kusababisha matokeo, mimi sijui tunakwenda wapi, lazima Watanzania sasa tuseme.
“Na mimi nimeamua kusema leo (jana) kwa sababu juzi niliposikia Waziri Mwigulu, atazungumza nilitarajia atazungumza namna ya kuondoa hii, ana alternative (mbadala), badala yake anazungumza kutetea, ‘transactions’ (miamala) za pesa ndizo zinasababisha watu washughulike kuzalisha, sasa unaziua, fedha zitafikaje?” alihoji.
Kitwanga, alikumbusha kuwa sheria ya kodi hairuhusu kutozwa kodi mara mbili, lakini anachokiona sasa kuna utozaji wa aina hiyo, jambo ambalo siku chache zilizopita, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, pia alilipinga vikali.
Juzi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu tozo hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, (Dk. Mwigulu), alisema serikali imechukua maoni yote ambayo yametolewa na wananchi kuhusu suala hilo na itayafanyia kazi na hivi karibuni itatoa tamko kuhusu utekelezaji wake.
Waziri huyo pia alisisitiza kuwa uamuzi wa kuweka tozo hizo ulifanyika kwa kushauriana na wananchi.