Dodoma, TANZANIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax leo amewasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni pamoja na Wizara hiyo kuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia Hadhi Maalum Diaspora wenye asili ya Tanzania na Uraia wa Nchi nyingine.
“Kwa kutambua umuhimu wa Diaspora, Wizara ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia Hadhi Maalum Diaspora wenye asili ya Tanzania na Uraia wa nchi nyingine (Tanzania Non-Citizen Diaspora), Wizara ilikusanya maoni toka kwa Wadau mbalimbali ndani na nje ya Nchi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Diaspora”
“Maoni yameainisha maeneo/masuala yanayopendekezwa kujumuishwa katika Hadhi Maalum, aidha mwezi Machi 2023, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilitoa maelekezo kwa Benki na Taasisi za Fedha Tanzania kuruhusu Raia wa kigeni wakiwemo Diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa Nchi nyingine kufungua akaunti za fedha za kigeni kwa kutumia vitambulisho mbadala vya utambuzi tofauti na hati ya kusafiria ya Tanzania na kitambulisho cha NIDA”
“Nyaraka hizo mbadala za utambuzi ni pamoja na hati ya kusafiria za Nchi ya kigeni, leseni za udereva za Nchi ya kigeni, kitambulisho cha kupigia kura cha Nchi ya kigeni na kitambulisho cha kazi cha Nchi ya kigeni au kitambulisho cha Mwanafujzi cha Nchi ya kigeni, hii itawawezesha Diaspora kuweka fedha zao za kigeni katika benki za hapa nchini”