0 0
Read Time:1 Minute, 46 Second

Havana CUBA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameongoza kikao cha Ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliowasili Havana, Cuba kwa ajili ya maandalizi ya ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini humo inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba, 2024.


Kikao cha maandalizi kilichofanyika tarehe 2 Novemba, 2024 ni muendelezo wa maandalizi ya ziara hiyo yaliyoanza na ukaguzi wa maeneo yatakayohusika wakati wa ziara ikiwemo: Maandalizi ya ukumbi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili, na Bustani ya Mashujaa “Heroes Park”, ambayo yalikaguliwa na Waziri Kombo na ujumbe wake mara baada ya kuwasili jijini Havana tarehe 1 November, 2024.

Ziara hiyo pamoja na masuala mengine, itaangazia zaidi ushirikiano wa uwili na changamoto za ulimwengu zinazohitaji suluhisho la pamoja kwa maslahi ya pande zote. Pia, inalenga kuziwezesha Tanzania na Cuba kuendelea kukuza uhusiano wake wa kihistoria na kidiplomasia kuwa wa kimkakati kwa kufungua maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi kiuchumi na kijamii.

Kwa muktadha huo, Tanzania imejipambanua kukuza ushirikiano wake na Cuba mathalani katika maeneo ya afya, elimu, sanaa, michezo, utalii, lugha ya Kiswahili na kuvutia uwekezaji hususan katika eneo la uchumi wa buluu.

Akiwa nchini humo, Mhe. Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. Miguel Díaz-Canel Bermudez, Rais wa Jamhuri ya Cuba tarehe 7 Novemba, 2024.

Vilevile, atapata wasaa wa kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu la José Martí Memorial ikiwa ni ishara ya kumuenzi shujaa huyo wa taifa la Cuba na kuzindua sanamu la Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika eneo maalum la Mashujaa wa Afrika na Waasisi wa Mataifa lililopo jijini Havana.
Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na Mheshimiwa Rais Dkt. Bermúdez watashuhudia utiaji saini wa kumbukumbu za pamoja za ziara, Hati ya makubaliano baina ya Chama cha Mapinduzi na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CDC).
Tarehe 8 Novemba, 2024 Rais Samia atakuwa mgeni rasmi na kufungua Kongamano la Kimataifa la Kiswahili.

H.E. Humphrey Polepole United Republic of Tanzania Ambassador to Cuba
Wajumbe katika kikao cha Mh. Waziri Kombo
Happy
Happy
0 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
0 %
Angry
Angry
0 %
Surprise
Surprise
0 %