
Kampala UGANDA
MKUTANO WA 20 WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EASTERN AFRICA POWER POOL (EAPP) WAFANYIKA JIJINI KAMPALA, UGANDA KUJADILI MASUALA YA MAUZIANO NA USAMBAZAJI WA NISHATI YA UMEME
Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri ulioambatana na Mkutano wa 32 wa Kamati ya Uongozi ya Eastern Africa Power Pool (EAPP) umefanyika jijini Kampala kuanzia tarehe 16 na 17 Aprili, 2025.
Eastern Africa Power Pool (EAPP) ni ushirikiano wa Nchi 13 za Mashariki mwa Afrika wenye lengo la kuungunisha Gridi za Taifa za Umeme za Mataifa husika kwa ajili ya kuwezesha kuuziana umeme ili kurahisisha upatikanaji wa umeme wa gharama nafuu katika kukidhi mahitaji yanayoongezeka na kufaidisha Nchi zote Wanachama.
Kwa sasa Nchi Wanachama wa EAPP ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Djibouti, Misri, Ethiopia, Kenya, Libya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania na Uganda.
Katika Mkutano huo, Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati huku akiambatana na viongozi wengine akiwemo Mhe. Dennis L. Londo (Mb.) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mawaziri mbalimbali kutoka Nchi Wanachama wa EAPP husuan Mawaziri wa Nistati, Makatibu Wakuu wa Nishati, Wakuu wa Mashirika ya Ugavi na Usambazaji wa Umeme na Maofisa Waandamizi kutoka Taasisi za Nishati.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umejadili masuala mbalimbali yanayohusu uratibu wa Soko la Pamoja la Nishati ya Umeme baina ya Nchi Wanachama wa EAPP. Aidha, Mkutano huo umepitisha Marekebisho ya Hati ya Makubaliano ya Uanzishwaji wa EAPP na Kanuni Mbalimbali za Uendeshaji na Uratibu wa Shughuli zake.











