Migogoro ni sehemu ya maisha, jifunze kuishi nayo, huwezi basi kaishi kaburini kwenye amani ya milele!
Denis Mpagaze!
Dunia ina tisha. Dunia ni hatari kuliko nyoka mwenye sumu kali. Ukizubaa unagongwa! Ukigongwa huamki. Dunia ni tambala bovu popote ukiigusa inachanika. Kuna watu walikuja kuifanya Dunia kuwa chungu, wasipokuvunja moyo watakuvunja miguu. Choko mchokoe pweza, binaadamu hutomuweza. Kezilahabi anaita Dunia Uwanja wa Fujo, maana kila mtu anakuja Duniani na fujo zake za mauaji, umalaya, uchawi, ubakaji, ulevi, ujambazi, wizi, usengenyaji na kisha anaondoka zake; ndo maana wazee wa zamani walisema migogoro ni sehemu ya maisha, kuizuia ni sawa na kuziba tundu la panya kwa mkate! Haiwezekani. Yaani ukifanya hivyo hata panya atakuona chizi.
Kumbe ujanja ni kukabiliana nayo kama ndege inavyokabiliana na upepo ikiwa angani. Life without battle is life without victory ni methali ya Kiafrika! Kama mbinguni walizinguana hadi shetani akatimuliwa wewe ni nani hadi useme hutaki mgogoro na mtu hapa duniani? Jipange kukabiliana na migogoro kabla hujapangwa!
Kukabiliana na migogoro unahitaji akili na hekima; siyo nguvu na hasira maana utaambulia kuua wakuue. Maana mwenye hasira anadhani kila tatizo ni msumari kwa sababu tu ana nyundo ya kugongea! Nguvu plus hasira ni hasara! Leo binti wa miaka 24 kamuua mpenzi wake wa miaka 25 kwa sababu Biblia inasema hasira hukaa kwenye kichwa cha mpumbavu. Unapambana kumkunja samaki aliyekauka!
Utatuzi wa migogoro unataka mtu mwerevu kama nyoka na mwenye hekima kama Mfalme Suleiman. Mfalme Suleiman alitumia akili na hekima kuumaliza ule mgogoro wa mwanamke aliyeua mwanaye kwa bahati mbaya na kuiba mtoto wa mwenzake akidai ni wake. Mgogoro ulivyopamba moto Mfalme alisema haya kateni huyu mtoto hai vipande viwili kila mmoja apewe kipande, mama wa mtoto akasema basi kuliko mwanangu achinjwe mpeni tu huyo mama yaishe. Mfalme akasema hakika wewe ndo mama halali, hebu chukua mwanao yaishe, yakaisha kweli!
Hekima humfanya mtu aonekane smart hata kama hakwenda shule. Watu smart wanapokutana na mgogoro hawahangaiki na habari za jino kwa jino maana Mahatma Ghandi alisema jino kwa jino litapelekea dunia nzima kuwa mapengo! Utasikia watu wakisema, kama angetumia akili tu kidogo asingeua! Wanasema ukitaka kumjua mtu mwenye akili mwambie huna akili, reactionnndo utajua hii njema zimo au hazima! Hebu jaribu,akikutoa meno mie simo!
Hata kupeleka mgogoro mahakamani ni ishara kwamba huna akili za kutosha kuumaliza hivyo unaomba wenye akili kukuzidi wakusaidie kuumaliza. Hiyo ndiyo maana ya mahakama kwa mtazamo wangu. Sikatazi watu kwenda mahakamani, nachosema unapokwenda mahakamani uwe tayari kwa lolote maana maamuzi yako hufanywa na waliokuzidi akili, unaweza kujikuta umefungwa na wakati ulikwenda kufunga mtu. Hapo ndo ujue siyo kila aliye jela ni muhalifu. Kule kuna walioshindwa kesi ikala kwako kama yule mama.
Mama yule alitandikwa na mume wake akaenda mahakamani, kesi iliposikilizwa vizuri wakagundua mama ndo mkosaji akageuziwa kibano, ni baada ya kuchukua mkopo benki kwa kuweka vitu vya ndani rehani bila mume kujua, akashindwa kulipa, benki wafika nyumbani na kupiga mnada vitu vya ndani hadi TV wakati baba anaangalia Yanga ikimenyana na Simba. Walipoondoka baba akasema leo wewe ni halali yangu. Akamkunja mke kidogo aue, mke akakimbilia mahakani ikala kwake!
Kwa sababu migogoro ni sehemu ya maisha, wenye akili walikaa chini na kuja na njia kuu tano za kutatua mgogoro wowote ule kabla hawajawaachia mahakamani kusaidia! Pengine ni baada ya kuona mahakama inavyowagharimu wengi. Imagine umemfunga mumeo, akitoka jela hapo kuna ndoa? Itoke wapi. Imagine umemfunga baba yetu tukashindwa kumaliza shule sasa tunabeba mizigo mtaani unadhani tukikutana chocho wawili itakuaje? Lazima nikukwide. Lakini kwenye mahakama kuna suala la kupigwa kalenda, kesi inaweza kuchukua miaka 10 na mwisho wa hukumu ukadunda. Hapo umepoteza muda na mali. Ndiyo maana hata mahakama inapenda mkayamalizie nje!
Sasa tuangalie njia moja baada ya nyingine kisha utaona inayokufaa maana imeandikwa za kuambiwa changanya na za kwako;
1 Unapoteze? (avoidance)
Hapa unagundua kabisa mkeo anakucheat, unaamua kupotezea, unajifanya as if hakuna kilichotokea! Lengo lako moyo wako usivunjike maana moyo hauna spea. Mkeo amekufumania kabisa lakini unapotezea, unafika nyumbani, unaoga, unakula, unalala badala ya kutoa maelezo ya kina kwa nini ulifanya vile lakini unakausha as if hakuna kilichotokea.
Hii njia ni nzuri tatizo unayemkaushia akihisi unamfanyia dharau utaumia.Ipo siku atakuletea mimba ya mwanaume mwingine ndoani. Omba Mungu asiseme unajifanya mjanja, tutaona! Hapo ndo utajua siyo kila anayekwenda baa alikwenda kunywa, wengine wanakwenda kuwanywea waliowazingua ili wazinguane.
- Unakubali yaishe? (compromise)
Umefunga ndoa na mtu usiyemjua halafu unataka umbadilishe tabia na yeye anataka akubadilishe tabia. Hapa mtakachokifanya ni kila mtu akubali kupoteza baadhi ya haki zake ili kumridhisha mwenzake hata kama ni kwa shingo upande. Kabla ya kuoa ulizoea kwenda disco, hiyo tabia mkeo haipendi inabidi uiache au upunguze, na wewe kabla ya kuolewa ulilala kwenye maombi sasa hiyo tabia mumeo haipendi itabidi uiache au apunguze. Unaachana na tabia fulani kwa utukufu wa mwenzako. 50 kwa 50. Lose some win some! Unasacrifice ulivyovipenda kumaliza mgogoro.
Tatizo la njia hii mmoja akiondoka mwingine anarudi kwenye tabia ya awali kwa sababu tabia ni kama ngozi, haivuliki kirahisi. Ndiyo maana ukisafiri mumeo analala disco.
- Mnakaa kuyamaliza (collaboration)
Hapa mnakaa pamoja kuyamaliza maisha yaendelee. Mnazungumza kwa kina hadi kila mtu anatoka ameridhika, mnashikana na mikono kabisa. Hii ni njia nzuri sana sema yataka moyo. Yaani nimekufumania na mke wangu halafu unasema tukae chini tuyajenge? Hivi una akili kweli?
- Vuta ni kuvute? (competitive)
Hii inaitwa jino kwa jino. Mauaji mengi yanatokea hapa. Bora tukose wote kulikokumuachia. Niko tayari kuuza kila kitu hadi nimfunge. Lazima nimtoe kwenye reli. I win – you lose.
Ntakufanyia kitu kibaya hutonisahau.
- Haya bwana umeshinda (accommodation)
Nikikutwanga utasema nimekuonea, nikikuacha nimekuogopa, anyway ngoja nikuache ili wajue nimekuogopa yaishe! Niko tayari kufanya unachotaka ili uridhike. “I lose – you win”. Kosa moja haliachi mke. Kuna mtu hapendi ugomvi. Nasamehe kwa ajili ya moyo wangu. Hii wanaitumia sana Wasukuma wa Geita, hawatakagi kesi. Wako tayari wakupe ng’mbe wote kuliko kupelekwa kwa askari.
Hata madereva wanaitumia sana hii wanapokamatwa na trafiki barabarani. Dereva yuko tayari kutoa za maji kuliko kupelekwa mbele. Kuendelea kufuatilia ntapoteza muda. Naacha kila kitu.
Wanandoa wanazinguana mmoja anaamua kumuachia kila kitu anaenda kuanza upya. Kuna askari huwa wanatumia hadi Biblia kupata kitu kidogo hasa Mt 5:25-37. Unasema hivi, Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.
Tuonane sehemu ya pili ya makala hii ambayo ni chanzo cha migogoro. Kula pozi kwa kurusha 5,000 nikurushie kitabu cha Viongozi wa Afrika Wanaoishi Baada ya Kufa. Mpesa 0753665484, ni softcopy, ukilipia nakurushia vyote kwa Whatsapp. Tangu tozo mpya zitangazwe watu wameanza kurudi benki kukutana na counta nne lakini moja tu ndo ina muhudumu nyingi ina jamaa liko busy, linaingia na kutoka!
Wako
Mwl. Denis Mpagaze
Muhenga wa Karne ya 21.
Whatsapp +255753665484!