
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishauri Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kuandaa Kalenda maalum ya kufanyika kwa Mashindano ya Kimataifa ya Marathon (Zanzibar International Marathon ) , ili kuwawezesha wadau wa sekta hiyo kuzitangaza mbio hizo katika Maonyesho ya kimataifa ya Biashara na Utalii, yanayofanyika kila mwaka.
Dk. Mwinyi ametoa ushauri huo katika Uwanja wa Amani jijini Zanzibar katika Mashindano ya Kimataifa ya Marathon 2021 (ZIM 2021) zilizoanzia Forodhani Jijini Zanzibar, na kuwashirikisha wanariadha kutoka ndani na nje ya Zanzibar pamoja na wananchi kwa ujumla.
Amesema uandaaji wa Kalenda hiyo utaendana na madhumuni ya msingi ya kurudishwa mbio hizo, sambamba na kuitumia njia hiyo kama moja ya vivutio vya kukuza sekta ya utalii, kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.
Alisema Serikali itatoa ushirikiano katika kuendeleza michezo mbali mbali pamoja na kuhakikisha mbio za Kimataifa za Marathon zinafanyika kila mwaka hapa Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kutoa wanariadha wenye vipaji na uwezo wa kushindana Kimataifa.










