1 0
Read Time:3 Minute, 15 Second

Na Abbas Mwalimu (0719258484).

Ijumaa tarehe 5 Novemba, 2021.

Kufuatia posti ya mdau mmoja Jamii Forums ya Alhamisi tarehe 4 Novemba, 2021 nimeona turejee kuelimishana kidogo kuhusiana na ADC wa Rais.

Mdau huyu aliyejitambulisha kama Escort 1 Jamii Forums aliandika kama ifuatavyo na hapa ninamnukuu:

“Watu wa itifaki ikulu naomba muwe mnaondoa aibu ndogondogo kama hii, inakuaje mpambe wa Rais Samia abebeshwe mzigo huu wa begi kubwa wakati Rais alipowasili airport ya Dar akitokea Scotland!”

“Hapo inamuondolea uwezo wa yeye kufocus katika mausala ya msingi, lakini pia hata kwenye suala la picha halileti muonekano mzuri, begi kubwa kama hilo wabebe wasaidizi wengine wa idara.”

“Naamini mtalifanyia kazi jambo hili nyeti, ahsanteni!”

Mwisho wa kunukuu.

Uhalisia wa alicholalamika ndugu yetu na kuomba jambo hilo lifanyiwe kazi upo hivi:

Kwa kawaida kila tumuonapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan nyuma yake huwa amesimama Afisa mwanamama wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) akiwa amevalia sare za jeshi kwa unadhifu mkubwa na huambatana nae kila aendapo.

Afisa huyu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye huwa amesimama nyuma ya Rais na kuambatana na Rais kila awapo akiwa na suti ya kijeshi ama kombati kiitifaki hutambulika kama ADC.

ADC ama A de C ni uteuzi (appointment) wa kijeshi ama heshima ya kuwa msaidizi wa kiongozi ambayo hutunukiwa Msaidizi Mkuu wa kiongozi wa Juu wa Nchi kama Rais, Mfalme ama Malkia.

Kirefu cha ADC ni Aide de Camp neno ambalo kwa Kiswahili hujulikana kama Msaidizi (wa Kambi). Neno hili limetoka katika mazingira ya kijeshi kwa kuwa nchi karibu zote duniani zimetokana na vita.

ADC wa Rais huweza kuwa afisa wa ngazi ya juu kuanzia cheo cha Meja, Luteni Kanali au Kanali kulingana na hadhi ya nchi kimataifa na anapofika cheo cha Brigedia Jenerali hupangiwa majukumu mengine.

Mara nyingi ADC wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huwa ni Afisa wa ngazi ya juu wa Jeshi mwenye cheo cha Kanali wakati kwa upande wa Tanzania Visiwani huwa ni Luteni Kanali. Hii ni kutokana na miongozo inayoongoza taasisi hiyo na hadhi ya Tanzania na hadhi ya nchi kimataifa.

Uwepo wa ADC kutoka jeshini ni kwa kuwa Rais pamoja na kuwa ni Mkuu wa nchi pia ni Amiri Jeshi Mkuu kwa hiyo ni “Mwanajeshi”.

Si Rais tu pekee huwa na ADC bali Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama CDF ana ADC wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP ana ADC wake na hata Mkuu wa Jeshi la Magereza CGP na Uhamiaji CGI huwa na maADC zao.

KAZI ZA ADC WA RAIS:

ADC wa Rais ana kazi nyingi sana kutokana na kuwa kwake Msaidizi Mkuu wa Rais, kazi hizo ni kama zifuatavyo;

(1) Msaidizi Mkuu wa kazi za kila siku ofisi ya Rais

(2) Huandaa kalenda, ratiba na safari za Rais.

(3) Huandaa masuala yote ya kiitifaki ya Rais

(4) Hupokea wageni wa Rais

(5) Hupokea zawadi mbalimbali kama ngao,mikuki n.k ambayo Rais hupewa kama zawadi akiwa ziarani

(6) Humbebea Rais Begi/Mkoba wake sambamba na diary na peni

(7) Huwaongoza na kuwaelekeza staff wengine

(8) Hufanya kazi mbalimbali kwa mujibu wa muongozo dawati la ofisi ya Rais.

(9) Husimamia e-mails sambamba na kuandaa na kupitia mawasiliano yote ya kiofisi ya Rais

(10) Husaidia kuandaa safari, kusalimia wageni, mabalozi na kusoma ramani.

Kazi hizi tulizoeleza hapa ni kazi za jumla za ma-ADC ulimwenguni lakini majukumu yao huweza kutofautiana kulingana na matakwa na miongozo mbalimbali.

Kwa hivyo basi, kwa muktadha wa nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi stahiki za ADC ni 2,5,6 and 8 tu, zilizobaki ni za Katibu wa Rais (KR).

Muundo huu wa Ikulu ndio unaotumika hata kwenye Ofisi za Marais Wastaafu ingawa wao ADC hatoki jeshini.

Hivyo ADC wa Rais si mlinzi wa Rais, walinzi wa Rais wapo na wataendelea kuwepo kama majukumu yao yanavyowaelekeza.

Wenu:

Abbas Mwalimu
(Facebook|Instagram|Twitter|Clubhouse).

+255 719 258 484.

Uwanja wa Diplomasia
(Facebook|WhatsApp).

Happy
Happy
50 %
Sad
Sad
0 %
Excited
Excited
0 %
Sleepy
Sleepy
25 %
Angry
Angry
25 %
Surprise
Surprise
0 %